Na NASRA KITANA
KLABU za Yanga na Simba zimeanza kupigana vikumbo kuwania saini za baadhi ya nyota wanaowataka katika dirisha dogo la usajili.
Timu hizo, zimeanza kusaka wachezaji wapya watakaoongezwa ndani ya timu hizo kwa kuboresha vikosi vyao ambavyo vinashiriki michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
YANGA
Hadi sasa, tetesi zinaeleza kuwa kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, ametaka kuongeza wachezaji watatu wapya.
Yanga wapo katika harakati ya kusaka saini ya nyota wa timu ya Taifa ya Uganda (Cranes), Allan Okello.
Okello anaichezea timu ya Vipers ya Uganda amekuwa na kiwango cha juu msimu huu.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, kocha Pedro anamuhitaji Okello na nyota kutoka Angola, Laurindo Dilson Maria Aurélio, kuongeza nguvu katika kikosi chake.
Pia, imeelezwa kwamba Yanga imevutiwa na uwezo wa mchezaji wa timu ya TRA United, Emmanuel Mwanengo.
Uhuru ilimtafuta Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ambaye alisema tayari wamepokea ripoti kutoka kwa mwalimu wao.
“Tumeona wachezaji wengi wanatajwa kuhusishwa na timu yetu, siyo wachezaji wabaya ni wazuri na wenye viwango vikubwa, tuwe na uvumilivu kwa kuwa kila mchezaji ambaye atasajiliwa tutamuweka wazi dirisha litakapofunguliwa,” alisema Kamwe.
Alisema kuwa watafanya usajili mapema zaidi kukimbizana na muda.
SIMBA
Uongozi wa klabu ya Simba umepanga kusajili wachezaji watatu pekee kuimarisha kikosi chao.
Simba ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya kumtangaza kocha mpya muda wowote, kuchukua mikoba ya Dimitar Pantev.
Wekundu hao wa Msimbazi wapo katika rada ya kuwania saini ya mchezaji kutoka Stade Malien, Ismaïla Simpara.
Pia, kuna taarifa kuwa Clatous Chama anataka kurejea ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa Simba unasubiri kutoa uamuzi wa kocha atakapokuja kama Jean Ahoua na Rushine Reuck atawahitaji au vinginevyo.
Tayari Ahoua anatakiwa na timu moja ya nchini Morocco huku Rushine anaweza kurudi Mamelodi Sundowns.
Lakini viongozi wa Simba wanataka kumpa mkataba wa kudumu beki huyo ambaye alikuja kwa Wekundu wa Msimbazi kwa mkopo.
Uhuru ilimtafuta Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema kuhusiana na kumrudisha Chama ndani ya kikosi chao na kumsajili Ismaïla Simpara hilo ni suala la muda kwa kuwa Simba wakimuhitaji mchezaji yeyote hawawezi kumkosa.
“Chama bado ni kipenzi cha Simba, kama viongozi wataona anafaa kurejea kikosini hapa hakuna atakayepinga, niwaambie tu kaeni mkao wa kula kwa sababu kuna wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa watasajiliwa kurudisha makali yetu,” alisema Ahmed.




