Na AMINA KASHEBA
SIKU kadhaa baada ya Simon Msuva kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), magwiji wa soka nchini wamempongeza nyota huyo huku wakisisitiza nidhamu na juhudi ndizo sababu za kufikia mafanikio hayo.
Msuva aliweka rekodi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda katika mchezo wa pili wa kundi C wa AFCON 2025 uliopigwa Uwanja wa Al Medina, Morocco.
Katika AFCON, sasa Msuva ndiye kinara wa upachikaji mabao akiwa na jumla ya mabao matatu akifuatiwa na Thuweni Waziri mwenye mabao mawili, Mbwana Samatta, Makumbi Juma na Charles Mombwa kila moja akiwa na bao moja.
Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Tunisia, Taifa Stars ilifunga mabao manane katika AFCON kuanzia mwaka 1980 ilivyofuzu kwa mara ya kwanza.
Katika mchanganuo wa mabao hayo, Stars ilifunga mabao tatu katika fainali za mwaka 1980, mabao mawili katika fainali za 2019, bao moja mwaka 2023 na bao moja mwaka huu.
Msuva alipachika mabao matatu katika fainali tatu tofauti ambapo alifunga bao moja katika kila mechi dhidi ya Kenya (2019), Zambia (2023) na Uganda (2025) wakati Waziri akipachika mabao mawili katika fainali za mwaka 1980.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alimpongeza Msuva kwa kuweka rekodi hiyo huku akikiri juhudi na nidhamu ndiyo sababu ya mafanikio.
“Msuva alikuwa na malengo ndiyo maana ndoto yake imetimia, pia vijana wanapaswa kupambana na kuongeza bidii katika mazoezi kutimiza ndoto zao kama ilivyokuwa kwake,” alisema.
Aliyekuwa kiungo wa Yanga, Salvatory Edward, alisema wachezaji wengi chipukizi wanapaswa kujifunza mambo mengi kwa Msuva kupandisha viwango vyao katika madaraja mbalimbali ikiwemo timu ya taifa.
Alisema Msuva amekuwa akijituma na kuonyesha nidhamu uwanjani hatua ambayo imempa urahisi wa kuweka rekodi hiyo kubwa nchini.
“Msuva amekuwa akijitoa na kupambana mara nyingi timu inapata matokeo kutokana na jitihada zake kwa kushirikiana vyema na wachezaji wenzake, vijana ambao ndiyo wanachipukia wanapaswa kuiga mfano huo kama wanahitaji kuweka rekodi,” alisema.




