Na AMINA KASHEBA
BINGWA wa zamani wa ngumi za kulipwa duniani, Manny Pacquiao kutoka Ufilipino, anatarajiwa kuja nchini kuhamasisha mchezo wa masumbwi na kushiriki shughuli za kijamii.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Rais wa BFT, Lukelo Wililo ambaye pia aliweka wazi kwamba mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 47, atawasili kati ya Machi au Aprili mwaka huu.
Wililo alisema shirikisho hilo linafanya mawasiliano ya karibu na bondia huyo kuhakikisha anakuja katika muda uliopangwa.
Rais huyo alisema ujio wa Mfilipino huyo utakuwa fursa kubwa kwa mabondia nchini hasa katika kuwaongezea ujuzi wa mchezo huo.
“Ujio wa Pacquiao utaongeza chachu na hamasa ya mchezo wa ngumi hapa nchini, nina imani kuja kwake kutaongeza nguvu kwa mabondia kuwa na bidii zaidi katika mazoezi wapate mafanikio,” alisema.
“Watanzania na wadau wa ngumi wategemee ujio wa bondia huyo mashuhuri, nina imani itakuwa fursa nzuri kwa mabondia kupata elimu na kuongeza maarifa katika mchezo wao,” alisema.
Pacquiao maarufu PacMan ambaye anasifika kwa kurusha masumbwi yenye kasi kubwa, amepigana mapambano 73, akishinda 62, sare nane na kupigwa matatu.
Mkongwe huyo amewahi kushinda mikanda mbalimbali ya dunia katika uzito tofauti ikiwemo mikanda ya WBO,WBC na IBF.




