Na FRED ALFRED,
Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Maji, kuhakikisha inafikisha huduma hiyo katika vijiji vyote nchini kabla ya mwaka 2030, ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yalibainishwa na Waziri wa wizara hiyo, Juma Aweso, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo, ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia.
Alisema hadi sasa, wizara imepeleka maji katika vijiji 10,758 kati ya 12,333 huku maagizo ya Rais Samia ni kuhakikisha vijiji 1,575 vilivyobaki, vinafikishiwa huduma hiyo kabla ya mwaka 2030.
“Rais Dk. Samia, ameagiza kuwa anapomaliza muda wake, vijiji 1,575 ambavyo havina maji viwe vimefikiwa. Ndiyo maana ameendelea kutoa fedha za kukamilisha miradi ya maji nchini.
Aliongeza kuwa :”Wizara ya Maji, hatuna kisingizo cha kutokamilisha miradi hiyo, hivi sasa tuna miradi 878 ambayo tunaendelea kuitekeleza vijijini, sisi tutahakikisha inakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Aweso alisema ili kutimiza azma ya Rais Samia, wameanza kutekeleza mpango wa vijiji 9,00 ambapo utahusisha kila mbunge kuainisha vijiji ambavyo havina huduma ya maji, viweze kuwekwa katika mpango huo.
Waziri Aweso alieleza kuwa, kuna miradi zaidi ya miradi 200 ambayo inaendelea kutekelezwa mijini, lengo ni kuhakikisha inakamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
GRIDI YA MAJI YA TAIFA.
Kuhusu utekelezaji wa Gridi ya Maji ya Taifa, Aweso alisema tayari wameanza kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Dodoma, hadi sasa umefika Tabora.
Alisema tayari wamemaliza upembuzi yakinifu wa kutoa maji Tabora hadi Dodoma, hivi sasa wanatafuta mkandarasi.
“Tayari tumenza kutekeleza mpango wa kujenga gridi ya maji ya taifa ili kutatua changamoto ya upungufu wa maji nchini kwa kuunganisha miradi yote mikubwa na midogo.
Aliongeza kuwa:”Mpango huu, unalenga kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakikisha maeneo ya mijini na vijijini, ikiwa na lengo la kukamilisha ifikapo mwaka 2030 kama alivyoahidi Rais Samia.
MAAGIZO DAWASA
Katika hatua nyingine, Aweso alimwagiza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire, kuhakikisha wananchi wanalipa bili kulingana na upungufu uliojitokeza katika kipindi cha Desemba mwaka jana.
“Tulipitia changamoto ya kutokuwa na maji kwa wananchi wa Dar es Salaam, itashangaza sana kuona wananchi wanapata bili kubwa kama ana kiwanda.




