Na SUPERIUS ERNEST
KATIKA Kampeni za Uchaguzi Mkuu, uliofanyika mwaka Oktoba 29 mwaka jana, Chama Cha Mapinduzi kiliahidi siku 100 za mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali.
Kupitia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye aligombea nafasi hiyo, aliahidi kufanya mageuzi makubwa, ikiwemo sekta ya afya kwa kuimarisha huduma za matibabu na kuwasaidia watu wasiojiweza.
Wananchi walikuwa wakikabiliana na changamoto ya kuzuiwa miili ya ndugu zao wanaopoteza maisha, kwa kudaiwa gharama za matibabu licha ya kutokuwa na uwezo wa kulipa kwa mara mgonjwa anapofariki akiwa hospitalini.
Suala hilo, limeingia katika utekelezaji na mengine ya kuboresha huduma za matibabu, ikiwemo kutoa huduma bure kwa watoto chini ya miaka mitano na wazee wa zaidi ya miaka 60.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ni mojawapo ya zile zinazo fanyakazi kubwa kutimiza ahadi ya Rais Dk. Samia ya kuboresha matibabu katika siku 100 tangu kuapishwa kwa kiongozi huyo wa nchi.
Akielezea mafanikio waliyoyapata katika siku 100 za Rais Dk. Samia, Mkurugenzi wa JKCI,Dk. Peter Kisenge, alisema wagonjwa waliopatiwa msamaha kuanzia November–Januari 22, mwaka huu ni 122.
Alisema watu wazima ni 52 na watoto 70 walionufaika na huduma hiyo.
“Fedha ambazo Serikali imechangia kugharamia matibabu ya wagonjwa 122 waliopata msamaha ni sh. 698,448,760.
“Wagonjwa waliopata msamaha wa huduma zinazotolewa katika kliniki ya moyo walikuwa 177, ambapo kati yao wanawake ni 76 na wanaume ni 101,”alisema.
Alisema gharama ambazo serikali imechangia kwa wagonjwa hao kupata huduma za kliniki zilikuwa sh. 2,670,000.
Alieleza kuwa msamaha uliotolewa kwa watu waliopoteza maisha ni sita kutokana na gharama za matibabu walizokuwa wanadaiwa ni sh. 22,059,331 na kuruhusu maiti kuchukuliwa mochwari.
Mkurugenzi Kisenge alisema kufanyika upasuaji wa moyo ujulikanao kwa jina la TAV Procedure, kwa mgonjwa mmoja.
Alisema upasuaji huo uligharimu kiasi cha sh. 55,000,000, ambapo serikali ilichangia kiasi cha sh. 35,000,000.
“Kusogeza huduma za ubingwa bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo karibu na wananchi kuwapunguzia gharama ya kuzifuata Dar es Salaam:
“Kuanzia Desemba 15 hadi 21, mwaka huu kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika Michuano ya Chipukizi CUP yaliyofanyika jijini Arusha,”alisema.
Alisema wananchi walioonwa ni 450, watoto walikuwa 440 na watu wazima 10. Watoto watatu walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI, Dar es Salaam.
Desemba,21 mwaka huu,waliweka kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa mashabiki wa timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa katika kambi hiyo, watu walioonwa na kupata vipimo ni 175 ambapo rufaa zilitolewa kwa watu 12 ambao walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
“Desemba,29 hadi Januari tisa mwaka huu, Kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC),ambapo wananchi 3,053, wakiwemo watu wazima 2,602 na watoto 451 walichunguzwa,”alisema.
Alisema wananchi 63 walikutwa na magonjwa ya moyo, watu 11 walihitaji upasuaji wa moyo na watu 111, ambapo kati yao watu wazima ni 89 na watoto 12 walipewa rufaa ya kwenda JKCI kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.
Dk. Kisenge alisema mafanikio hayo yalitizwa na kufanikishwa na uwezeshaji mkubwa wa serikali ya Rais Dk. Samia, kwa dhamira yake ya dhati ya kuboresha matibabu kwa wananchi.
Alisema Rais Dk. Samia ameedelea kuboresha maslahi ya watumishi na kuwapatia fursa za kwenda kusoma nje ya nchi.
Alisema pamoja na mafanikio hayo ya siku 100 za Rais Dk. Samia zimekwenda na mafanikio ya miaka 10 ya taasisi hiyo, ambayo imekuwa na tija kubwa
“Tunajivunia hatua kubwa tuliyofikia katika kipindi hiki cha miaka 10 kazi ambayo inafanywa na Rais Dk. Samia, akitoa fedha kufanikisha utoaji huduma bora kwa wananchi kupitia taasisi hii ya moyo.
“Serikali imetoa mabilioni ya fedha kununua mashine na mitambo ya kisasa ya kufanya upasuaji mkubwa kwa njia za kisasa za bila kufungua kifua kama tulivyokuwa tukifanya miaka ya nyuma, hatua hiyo ndiyo imewezesha mafanikio makubwa tuliyofikia,”alisema.
Alieleza kuwa, katika miaka 10 tangu kuanza kutoa huduma wamefanikiwa kufanya upasuaji mpya zaidi 30 ambazo zilikuwa hazifanyiki nchini na wagonjwa walikuwa wakipelekwa nje nchi, lakini kwa sasa zinafanyika nchini.
Alisema katika mwaka huu, wamefanikiwa kufanya visa vipya vya upasuaji zaidi ya saba, ambazo zilikuwa hazifanyiki nchini na Afrika Mashariki na Kati, hivyo kuifanya JKCI kuwa ni kituo bora cha matibabu Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Kisenge alisema mafanikio hayo ya uwekezaji mkubwa wa serikali ndiyo yanayowezesha maendeleo hayo makubwa kwa kuvutia wataalamu bingwa wakimataifa kufika nchini kuwajengea uwezo madaktari wa JKCI.
Alisema mafanikio yamevutia wananchi wa mataifa mengi ya Afrika na ulaya kufika hospitalini hapo kupata matibabu ya moyo.
Alieleza kuwa, mara kwa mara wamekuwa wakifanya visa vipya vya upasuaji, ambavyo awali zilikuwa hazifanyiki ikiwemo kufanya upasuaji bila kufungua kifua.
Alitaja baadhi ya matibabu mapya waliyoyafanya mwaka huu, ni kuzibua mishipa ya moyo kwa watoto wadogo, upasuaji wa mishipa mikubwa ya Aota inayopeleka damu sehemu mbalimbali za mwili.
PRESHA ULIOSHINDIKANA
“Wiki mbili zilizopita tulifanikiwa kuanza kutoa matibabu ya presha zilizoshindikana, ambazo mgonjwa hupewa dawa zote za presha pasipo mafanikio, huku ikiendelea kuwa juu,”alisema.
Alisema wamefanikiwa kuanza matibabu hayo ya kuchoma sindano mishipa ya fahamu inayopeleka damu katika figo.
Dk. Kisenge alisema mishipa hiyo ndiyo inachangia presha kuwa juu, kusababisha mtu kupata shinikizo la juu na kutotibika kawaida hivyo wamefanikisha kuitibu.
Alieleza kuwa, matibabu hayo mapya yalifanikishwa na madakatari bingwa kutoka Misri kushirikiana na wale wa JKCI, ambapo walitibu wagonjwa saba kupitia kambi hiyo.
“Hiyo ilikuwa ni njia ya kuwajengea uwezo madaktari wetu na kwa sasa wana uwezo mkubwa wakushughulikia changamoto hiyo na kuifanya JKCI kuwa ya kwanza Afrika Mashariki na Kati katika kutoa matibabu hayo makubwa,”alisema.
Alieleza kuwa, kabla ya hapo matibabu hayo yalikuwa yanatolewa katika mataifa makubwa ya ulaya hususan ni India na Marekani na kwa Afrika yalikuwa yakifanyika mataifa ya Misri, Moroco na Algeria.
Alisisitiza kuwa, gharama ya kutibu tatizo hilo ni kubwa kwani mgonjwa mmoja ni sh. milioni 29, hivyo huduma hiyo kupatikana nchini itakuwa msaada mkubwa sana.
KUTIMIZA AHADI
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kupitia hotuba zake mbalimbali amekuwa akisisitiza utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. Samia alizoahidi katika kampeni za uchaguzi.
Aliipongeza JKCI, kupitia kwa Mkurugenzi Dk. Kisenge kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuimarisha huduma za afya hususan matibabu ya moyo.
Alisema kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya JKCI, kwa kuwafuata katika maeneo yao imekuwa na tija ikilenga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Kazi inayofanywa na JKCI ni miongoni mwa utekekezaji wa ahadi za serikali ya CCM kwa wananchi huku akiipongeza kwa kuingia makubaliano ya kiundeshaji na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) na kufungua vituo vingine jijini Dar es Salaam na mipango mizuri waliyonayo na kufungua matawi katika mikoa mingine.
Alitaja huduma zingine ni kutozuia miili ya wagonjwa waliofariki wakipatiwa matiabu hospitali.
“Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia kwa Dk. Samia kiliahidi kutozuiwa miili ya maiti, hilo limeendelea kutekelezwa.
Mgonjwa anapofariki kwanza ndugu wapewe kibali cha kuchukua mwili, ndipo taratibu zingine zifuate,”alisema.
Alisema huduma za afya zinaendelea kuboreshwa kila kukicha kwa kununua vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo mashine na mitambo ya kisasa kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma bora za kibingwa.
Dhamira ya serikali ni kuhakikisha hakuna mwananchi, anayekosa huduma ya afya ndiyo maana imeendelea kushughuliki bima ya afya watanzania wote wapate matibabu bora.
MFUMO WA MAWASILIANO
Akizungumzia mfumo aliouzindua katika siku 100 za Rais Dk. Samia, Mchengerwa alisema unalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi kuzungumza na waziri moja kwa moja kupitia simu janja.
“Hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma kwa kisingizio cha kutokuwa na simu janja, serikali italeta teknolojia itakayopanua haki ya kupata huduma za afya,”alisema.
Alieleza kupitia teknolojia hiyo, mwananchi aliyeko Kituo cha Afya cha Longido au eneo la mpakani Namanga, atazungumza moja kwa moja na waziri, kuuliza maswali, kuwasilisha malalamiko au kutoa mrejesho kuhusu huduma anazopata.
“Mfumo huu utawawezesha wananchi kuzungumza na Waziri wa Afya, kuuliza swali lolote kuhusu sekta ya afya, kutoa maoni, hali ya huduma aliyoipata au malalamiko ambayo yatafanyiwa kazi mara moja,” alisema.
Akizungumzia matumizi ya Akili Mnemba (AI), katika utoaji huduma za afya, Mchengerwa alisema serikali itaitumia kwa uangalifunakuzingatia utu.
“Teknolojia hiyo itasaidia kubaini hatari mapema, kuongeza uchambuzi wa taarifa na kuboresha uamuzi wa kitabibu,” alisema.
Kama hiyo haitoshi, CCM, Kupitia Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, ilisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora.
Alisema serikali ya Rais Dk. Samia, imeendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ndiyo maana inajenga Zahanati kila kata na vituo vya afya karibu na makazi ya wananchi kuwaondolea umbali wa kutembea kufuata huduma za afya.
Alieleza kuwa, hospitali hizo zimepata vifaa tiba vya kisasa, huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo na watumishi wa afya kutunza vifaa tiba kuwezesha wananchi kupata huduma bora wakati wote bila manung’uniko.




