Na MWANDISHI WETU, Kyerwa
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kuanza utaratibu wa kuvunja mkataba wa kampuni ya ujenzi kutoka China ambayo imekuwa ikisuasua kujenga barabara ya Omurushaka – Kyerwa yenye urefu wa kilomita 50.
Pamoja na agizo hilo, Ulega amezitaka mamlaka zinazohusika na utoaji kazi za ujenzi wa barabara kuiweka kampuni hiyo, Shandong Luquiao Group, katika orodha ya kampuni zisizotakiwa kupewa kazi za ujenzi wa barabara hapa nchini kwa sababu rekodi yake kwa kazi ilizopewa hairidhishi.
“Natoa maelekezo kwa TANROADS na Mkurugenzi wa barabara kutoka wizarani mpitie taratibu za kuvunja mkataba kwa mkandarasi huyu ndani ya mwezi mmoja, tuweze kumchukulia hatua za kisheria, hatuwezi kuona fedha za wananchi zinachezewa kwa namna hii,” alisema Ulega.
Ulega ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani, alitoa maelekezo hayo katika mkutano na wananchi wa Kyerwa mara baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Katika mkutano huo, Ulega alitoa maagizo kwa wataalamu wa sheria kuwa, wanatakiwa kufuata vigezo vyote vya kisheria, baadaye serikali isiingie katika kesi ambazo zitaigharimu fedha nyingi kwa sababu ya kushauriwa vibaya na wataalamu.
Awali, katika taarifa zao kwa waziri, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Kyerwa, Khalid Nsekela, walieleza kutofurahishwa kwao na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo, licha ya rekodi yake kusuasua, ameendelea kupewa kazi mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa ya TANROADS, mkandarasi huyo, tayari amelipwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tisa, ingawa alitakiwa kuwa, amefikia walau asilimia 50 ya lengo, hadi sasa yuko katika asilimia tano ya utekelezaji wa mradi.
Katika hotuba yake hiyo, Ulega aliitaka TANROADS, kutafuta suluhisho la haraka kwa kumtafuta mkandarasi wa ndani mwenye uwezo, atakayeikarabati barabara hiyo ndani ya siku 30 ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Alitoa rai kwa wasimamizi wa miradi kutoka TANROADS, kuhakikisha wanasimamia vyema miradi kwa mujibu wa mkataba.
Pia, alisema wasimamizi wa mradi huo, wachunguzwe endapo kama wamehusika katika uzembe wa ucheleweshaji mradi huo ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwasa alisema kwamba, mkandarasi huyo, amekuwa akisuasua katika utekelezaji wa miradi mingine, ikiwemo ya TARURA katika mkoa huo na kushauri serikali kusitisha mikataba hiyo na kutompa zabuni tena mkandarasi huyo.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Ulega, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Kagera, Mhandishi Joel Mwambungu, alisema kuwa, mradi huo kwa sasa, umefika asilimia 5.43, unafadhiliwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 94.
Aliongeza kuwa, huo upo nyuma kwa asilimia 46.26 ambapo ni tofauti kati ya maendeleo yaliyotarajiwa ya asilimia 51.69 huku uhalisia uliofikiwa ukiwa asilimia 5.43 pekee.





