Na MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema anataka kuona kila fedha inayotolewa kwa miradi ya maendeleo, inatumika kama ilivyokusudiwa.
Amesema serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wenye dhamana, hawafuatilii matumizi ya fedha na kusababisha miradi kushindwa kutekelezwa kwa viwango na ubora kwa manufaa ya wananchi.
Dk. Mwigulu, alisema hayo, alipozungumza na wananchi baada ya kuzindua mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Waziri Mkuu, aliwasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha anatekeleza majukumu yao ipasavyo na si vinginevyo.
“Tunataka watu wasilale ofisini, ninyi ni watumishi wa serikali, fedha zikiletwa zikafanye kazi iliyokusudiwa,” alisema.
Dk. Mwigulu, alisema hayo wakati akihoji kukosekana ubora na viwango vya majengo, risiti za malipo, kutofanyika kwa kodi ya zuio, kukosekana cheti cha ubora wa mabati, matofari na saruji katika baadhi ya shule za msingi wilayani humo.
Mradi huo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, uliogharimu sh. milioni 526.8, una uwezo wa kuzalisha mitungi 120 ya kilo 50 kwa siku.
Mitambo hiyo imeiwezesha halmashauri hiyo kutolazimika kusafirisha mitungi ya oksijeni hadi jijini Tanga, umbali wa takribani kilometa 175 kwa ujazaji.
Hadi sasa, mtambo umezalisha mitungi 1,440 ya hewa tiba (oksijeni) ya kilo 50 na mitungi 200 ya kilo 15.
Aidha, Waziri Mkuu alionya tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali kuwa na utaratibu wa kuzoea matatizo ya wananchi.




