Dodoma
Na MUSSA YUSUPH
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kulinda Hifadhi ya Taifa Ngorongoro kwa mustakabali wa wenyeji wa eneo hilo na taifa, kwa kuwa hifadhi hiyo ni urithi wa dunia yenye rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na baadaye.
Ameeleza kuwa, Ngorongoro ni mali ya Watanzania huku akisisitiza kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu masuala mbalimbali kwa kuzingatia uhuru, utamaduni, mila na heshima ya Watanzania.
Dk. Samia aliyasema hayo Ikulu ya Chamwino mkoani hapa, baada ya kupokea taarifa ya tume za rais alizoziunda kutathmini masuala ya mgogoro wa ardhi na utekelezaji wa uhamaji wa hiyari kwa wakazi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Niwaombe Watanzania wenzangu kulipa kipaumbele suala la uendelevu wa eneo la Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi. Ngorongoro ni almasi yetu Watanzania, ni mali yetu Watanzania, lakini pia ni urithi wa Dunia. Wote wanaoleta maneno kwa faida zao kwa wanayoyaona wao, sisi Ngorongoro Mungu ameishusha kwetu Tanzania.
Alisisitiza: “Hatuna budi kuienzi tunu hii kwa umoja wetu, tuna wajibu kuyalinda na kuyahifadhi maeneo haya (Ngorongoro) kwa mustakabali wa maslahi ya wenyeji wa eneo hilo, pia mustakabali wa taifa letu na dunia kwa ujumla.”
Rais Dk. Samia alisema kuundwa kwa tume hizo ni sehemu ya uongozi wa watu wenye kujali maslahi ya wananchi.
“Kama kuna malalamiko ya watu, tunatumia watu wenyewe (Watanzania) nendeni tukakubaliane nini tunafanya. Huko miaka ya nyuma zingetoka pesa nyingi kutafuta kamati za ushauri kutoka nje.
“Wametoka nje wanakuja kutoa huduma za ushauri kwa Ngorongoro ambayo ipo kwetu, tunaishi nayo. Kwa hiyo tulichokifanya ni Utanzania. Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kupata suluhu ya kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazotokea ndani ya nchi yetu. Tunafanya hivyo kulinda uhuru, utamaduni wetu, mila zetu na heshima yetu kama taifa,” alieleza.
SABABU ZA KUUNDA TUME
Rais Dk. Samia alisema miaka ya nyuma ziliibuka taarifa nyingi katika mitandao ya kijamii, mashirika, taasisi mbalimbali za kimataifa pamoja na malalamiko ya wananchi wa Ngorongoro, hivyo Desemba mwaka 2024 aliamua kukutana na viongozi wa kimila kutoka kabila la wamasai na wazee wa kimila kutoka Ngorongoro.
Alisema serikali ilisikiliza malalamiko yao kuhusu masuala ya ardhi, uhifadhi mazingira na utekelezaji wa operesheni ya uhamaji kwa hiyari kutoka Ngorongoro kwenda maeneo yaliyoteuliwa.
“Serikali iliona umuhimu wa kuunda tume hizo mbili baada ya kuwasikiliza wananchi hao kwa lengo la kufanya tathmini ya kina na shirikishi. Ndiyo maana wenyeji wa Ngorongoro walikuwepo katika tume hizo na hata wataalamu kutoka maeneo mbalimbali tuliwaweka,” alieleza.
Kwa mujibu wa Dk. Samia, serikali imechukua hatua hizo kwa sababu Ngorongoro ni urithi wa dunia ambao upo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Pia, alisema eneo hilo ni la pekee lenye kina cha mita 600 kwenda chini na ikaibuka kreta, ni eneo lenye baionuai nzuri, wanyama wa kila aina, kuna ndege wazuri, vivutio vingi ambavyo siyo rahisi kuonekana maeneo mengine katika bonde moja.
“Kuna ushahidi kuhusu uwepo wa historia ya mwanadamu miaka milioni tatu iliyopita maeneo ya Olduvai na Laitoi. Ngorongoro ni eneo lenye misitu ya aina nyingi, kuna maeneo ya volcano ambazo baadhi zingine zinaaminika bado zipo hai, ni eneo la kuhifadhiwa, la kunyenyekewa kwa faida ya taifa na dunia.
“Ni eneo la kufanyia ibada na tamaduni za watu, ni eneo la utalii wa shughuli nyingi, utalii wa kutembea kwa miguu, kuangalia ndege na kupiga picha,” alisisitiza.
Alisisitiza: “Tufanyaje?, watu ni wetu na mifugo tunaihitaji, Ngorongoro ni yetu na tunaihitiaji, tufanyaje? Tume zimetoa mapendekezo ambayo serikali tunakwenda kuyafanyiakazi.
Taarifa za tume zimeonyesha umuhimu wa kulinda mfumo wa ikolojia unaounganisha eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Pololeti na maeneo ya Ziwa Natroni.”
“Haya ni maeneo muhimu sana kwa nchi yetu. Kuna madini yanayotafutwa ulimwenguni yapo katika maeneo hayo. Ni maeneo muhimu ya kulindwa, sote tutakubaliana huu ni mfumo muhimu na endelevu kwa taifa letu. Taarifa hizo pia zimetupa taswira halisi ya changamoto za utekelezaji zoezi la uhamaji wa hiyari kwa wakazi wa eneo la Ngorongoro,” alibainisha.
Dk. Samia alisema ni matumaini kwamba mapendekezo yaliyopo katika ripoti hizo ambayo mengine yamekwenda kisera, kisheria, kiuchumi na kijamii, serikali itayafanyiakazi kupata namna bora ya kuyashughulikia kwa maslahi ya wananchi.
Aliwahakikishia wananchi wa Ngorongoro na Watanzania kwamba serikali itashirikiana nao hatua kwa hatua huku akitoa maagizo kwa ofisi ya waziri mkuu na katibu mkuu kiongozi, kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya kamati hizo.
“Mchakato wa utekelezaji mapendekezo yaliyotolewa na tume unaweza kuibua maoni tofauti katika jamii, pia taasisi nyingine ambazo zinafaidika na uwepo wa ngorongoro na maeneo yake wanaweza kuleta maoni tofauti.
“Niwaombe Watanzania wenzangu kulipa kipaumbele suala la uendelevu wa eneo la Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi. Ngorongoro ni almasi yetu Watanzania, ni mali yetu Watanzania,” alisisitiza.
TUME YA IYOMBE
Awali, tume iliyoundwa na Rais Dk. Samia kutathmini shughuli ya uhamaji wa hiyari wa wananchi kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, imetaja sababu tano za kukwama kwa shughuli hiyo.
Akiwasilisha taarifa yake mbele ya Rais Dk. Samia, Mwenyekiti wa tume hiyo, Mussa Iyombe, alizitaja sababu hizo ni kutoshirikishwa kwa wananchi, upungufu wa sheria na kanuni.
Alizitaja sababu zingine ni ujenzi wa nyumba moja kwa familia zenye wake zaidi ya mmoja, motisha kwa waliohama kupungua na mpango huo kuendeshwa kwa ushawishi badala ya utashi.
“Mheshimiwa Rais, shughuli hii haikufanikiwa, zimehama kaya 1,678 kati ya kaya 23,000 zinazoishi Ngorongoro na sasa kuna zaidi ya sh. bilioni 212.3 ambazo zipo tayari kujenga nyumba kwa watakaohama kwa hiyari,” alisema.
TUME YA JAJI NDIKA
Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Matumizi ya Ardhi katika Eneo la Ngorongoro, Jaji Dk. Gerald Ndika, alisema mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya utalii.
Alisema eneo hilo limeendelea kuwa la kipekee duniani huku idadi ya watalii ikiongezeka kutoka 592,498 mwaka 2015 hadi 884,484 Machi mwaka huu.
“Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka sh. bilioni 60 mwaka 2015 hadi sh. bilioni 223, Machi mwaka huu,” alieleza.
Hata hivyo, alisema ongezeko la watu ndani ya eneo hilo linaongeza shinikizo la mahitaji ya maendeleo ya jamii.
Aliongeza: “Idadi ya watu imeongezeka kutoka takribani 8,000 mwaka 1959 hadi kufikia 100,793 mwaka 2022, na inakadiriwa kufikia 276,651 ifikapo 2050.”




