• ePaper
Sunday, April 5, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

AMANI NI LULU – RAIS DK. SAMIA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 22, 2026
in Habari, Kitaifa
0
AMANI NI LULU – RAIS DK. SAMIA
0
SHARES
4
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na WAANDISHI WETU

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema ni muhimu kutambua, siyo kila mtu anafurahi kuona Tanzania ikiwa katika hali ya amani, umoja na utulivu.

Hivyo ni vyema kuzidisha mshikamano na upendo katika taifa kuendelea na sifa ya Tanzania ya amani.

Rais Samia aliyasema hayo, jijini Dar es Salaam, alipohutubia Baraza la Idd el-Fitri, lililofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Aliwaeleza viongozi wa dini kuwajenga waumini kiimani na kimaadili kama vitabu vya dini vinavyoelekeza, hatua hiyo itaendelea kujenga taifa lenye amani, mshikamano, utulivu na ustahimilivu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Alisema serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha uhuru wa kuabudu unaendelea kuwepo.

Aliwataka waumini kufahamu mipaka ya uhuru huo kwa kuheshimu sheria za nchi na haki za wengine.

Rais Dk. Samia alisema uhuru huo usigeuke chanzo cha chuki, mgawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano wa taifa.

Aliwashukuru viongozi wa dini kwa mchango wanaoutoa katika kuimarisha maadili.

“Ni ukweli usiofichika dini inapojenga maadili mema katika jamii, taifa hujenga jamii bora na maendeleo yake.

Bila kuwepo maadili, tukiendelea kuyaacha ya kutukanana katika mitandao ya kijamii, yanayotengenezwa kwa AI (akili mnemba), ya kuwakashifu viongozi wa serikali, watoto wetu wakiyaona wanajifunza,” alieleza Rais Samia.

Alionya hayo yakiachwa yaendelee, nchi haitakuwa salama wala kutulia na maendeleo yatakosekana kutokana na vurugu.

Rais Samia alisema viongozi wa dini wamekuwa sauti ya matumaini na mwongozo kwa waumini katika nyakati za changamoto za kijamii na kimaadili.

Pia, alisema wamekuwa wafariji kwa waliokata tamaa na kuwatia moyo walio katika dhiki.

Alieleza katika nyakati hizi inaposhuhudiwa mivutano na migogoro duniani, nchi imeendelea kubaki salama na amani.

“Ni muhimu tukatambua siyo kila mtu anafurahi kutuona katika hali ya amani, umoja na utulivu, hivyo ni vyema tukazidisha mshikamano na upendo, katika taifa letu, tuendelee na sifa yetu ya Tanzania ya amani,” alisema Rais Samia.

Alieleza Waislamu na Wakristo wana wajibu wa kutekeleza kwa vitendo maamrisho mema ya vitabu vitakatifu, siyo tu katika vipindi vya mfungo wa Ramadhani na Kwaresma, bali siku zote.

“Mwezi Mtukufu wa Ramadhani haikuwa tu kipindi cha toba na ibada, ni wakati ambao mioyo yetu ilikumbushwa kuwaonea huruma wenye uhitaji,” alisema.

Aliongeza: “Kusaidiana na kuimarisha mshikamano katika jamii kama kitabu cha Quran kinavyosema ‘wema siyo kuelekeza nyuso mashariki na magharibi, bali ni imani ya kweli, kuamini Mungu yupo, kuamini siku ya kiama, kuamini kitabu chake kitukufu na kuamini mitume wake.”

“Ni kutoa mali uipendayo kwa jamaa, yatima na masikini na wenye uhitaji, katika mifumo tofauti ikiwemo sadaka au zaka na wema na kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu,” alisema.

Alisema Biblia inaeleza dini safi ni kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Alimshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, kwa kumwalika katika baraza hilo na kuwapongeza Waislamu kwa kutimiza funga.

Aliwapongeza viongozi wa BAKWATA wakiongozwa kwa kuimarisha huduma za afya nchini, kwa ujenzi wa vituo vya afya kila mkoa na baadhi ya wilaya, pamoja na mkakati wa kujenga hospitali ya rufaa, Dar es Salaam.

Alisema uamuzi huo, unaunga mkono jitihada za serikali za kuimarisha huduma za afya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na kuwaahidi ushirikiano wa vitendo. 

 MUFTI ATOA WITO WA HESHIMA 

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, aliwasihi Watanzania kuheshimu viongozi na kuwaombea kwa Mungu wafanikishe utekelezaji wa majukumu yao.

“Pamoja na kupiga makelele wanaombewa kwa nini, tunachozungumza ni mistari, tunazungumza vitabu, hatuzungumzi vitu juu juu tu,” alifafanua.

Mufti Zuberi aliwataka Waislamu kutokubali kuchokozeka na jambo la uongo halijifichi, hubainika mara moja.

“Jambo lingine ni kuwa na heshima kwa viongozi, siku hizi kila mtu anaweza kumsema mtu yeyote, haogopi Mungu wala sheria, wala uislamu, mtu anatukana anavyotakana,” alisema.

KATIBU WA BAKWATA

Akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Alihaji Nuhu Mruma, alisema amani na utulivu katika nchi ni kigezo cha maendeleo kwa jamii.

“Pamoja na masikitiko makubwa tuliyopata mwisho wa mwaka uliopita, tunamshukuru Mungu kwa kutuvusha salama kama taifa na kusonga mbele,” alisema.

Alisema kuna mihimili ya kimaadili yenye kuchangia kujenga usalama na amani ndani ya jamii; moyo wa kupendana, kuhurumiana, upole na maadili mema.

“…usalama na amani ni jukumu letu sote na si la serikali pekee yake, bali ni kila mtu,” alisema.

Alitoa wito kwa Waislamu kulinda amani, kwani ndiyo mtaji muhimu kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla, huku wakiepuka hila za kuivuruga.

Alisema BAKWATA inampongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kulinda amani baada vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu.

“Tumeshuhudia yaliyotokea kipindi cha uchaguzi ambayo hayakuwa na taswira nzuri kwenye nchi yetu, pongezi ziende vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha  amani na usalama kurejea kwa kipindi kifupi,” aliongeza.

Alisema baraza hilo linaamini tume iliyoundwa na Rais Dk. Samia ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29, mwaka jana, itabainisha wazi nini chanzo cha matukio hayo na kutoa njia sahihi ya namna ya kupatikana suluhisho.

“Tume itafanyia kazi matokeo yake kwa haki, na baadaye kutupeleka kwenye maridhiano yatakayoleta mustakabali wa taifa letu  tuendelee kuishi kama jamii moja katika nchi yetu,” alisema Alihaji Mruma.

Alisema kila mmoja anapaswa kujifunza kwa kile kilichotokea Oktoba 29 na kuhakikisha anaepuka migogoro inayosababisha mifarakano na kuathiri uslama na amani.

Katika baraza hilo viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo, Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.

Dk. MWIGULU

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka Waislamu na Watanzania kuyaenzi na kuyaendeleza mema waliyojifunza katika mwezi wa Ramadhani.

Alitaja mazuri hayo ni upendo, huruma, kusaidia, kuimarisha maadili na mshikamano katika jamii.

Dk. Mwigulu alieleza hayo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, alipowatakia Waislamu na Watanzania sikukuu njema ya Eid el–Fitri.

“Naungana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwatakia Waislamu na Watanzania sikukuu njema ya Eid-el-Fitri,” aliandika.

Previous Post

SIMBA KUIUA TRA UTD

Next Post

SERIKALI YAIFANYA MWANZA KITOVU KIKUU CHA KIUCHUMI

Next Post
SERIKALI YAIFANYA MWANZA KITOVU KIKUU CHA KIUCHUMI

SERIKALI YAIFANYA MWANZA KITOVU KIKUU CHA KIUCHUMI

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MKWASA, MOGELLA, PAWASA WAIPA MCHONGO YANGA

MKWASA, MOGELLA, PAWASA WAIPA MCHONGO YANGA

2 months ago
STARS: TUNISIA INAKAA

STARS: TUNISIA INAKAA

3 months ago

Popular News

  • CHAMUDATA YAZUNGUMZIA AMANI

    CHAMUDATA YAZUNGUMZIA AMANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MCHENGERWA ASHUSHA MAAGIZO KWA WAGANGA WAKUU WA MIKOA, WILAYA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AELEZA FAIDA YA KULINDA TUNU YA AMANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • UTEUZI WA PROFESA KABUDI GUMZO NCHINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • VIONGOZI WA DINI WAHUBIRI AMANI 

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?