• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

WANASIASA WAELEZA IMANI YAO TUME YA JAJI CHANDE

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 30, 2026
in Habari, Kitaifa
0
WANASIASA WAELEZA IMANI YAO TUME YA JAJI CHANDE
0
SHARES
18
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na ELIZABETH JOHN

BAADHI ya wanasiasa wamesema wanaamini majibu sahihi ya chanzo cha vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, yatapatikana kupitia Tume Huru ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Wameshauri taarifa itakayotolewa na tume hiyo iliyotangazwa Novemba 8, mwaka jana chini ya Mwenyekiti wake, Mohammed Chande Othman, ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu, inapaswa kupokewa na kuheshimiwa na Watanzania.

JOHN CHILIGATI

Akizungumza na UHURU mwishoni mwa wiki, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Manyoni na waziri mstaafu, John Chiligati, alisema Rais Dk. Samia alifanya jambo la busara na kistarabu kuunda tume ya kuchunguza vurugu hizo.

Chiligati alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kutafuta ukweli na suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.

“Tukio hilo lililotokea ndani ya nchi linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa ndani ya nchi yenyewe,”alisema.

Alibainisha Watanzania wana uwezo wa kujadili na kupata majibu ya changamoto zao bila kuhitaji shinikizo au uamuzi kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Chiligati, tume halisi ni wananchi wenyewe, hivyo watanzania wawe na kutulia kusubiri matokeo ya uchunguzi huo ambao utaweka wazi chanzo cha vurugu na kupendekeza kitu cha kufanya kuepuka tatizo hilo kujirudia.

Alisema vurugu zina madhara katika ustawi wa taifa, hivyo alishauri changamoto zinapotokea njia sahihi ni kukaa mezani na kujadiliana kupata suluhisho la amani badala ya kutumia nguvu.

Chiligati alisisitiza vurugu husababisha hasara kubwa kiuchumi na kuharibu uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi na washirika wake, hivyo mazungumzo na maridhiano ndiyo njia bora ya kujenga mshikamano na kulinda maslahi mapana ya taifa.

Akizungumzia vurugu za Oktoba 29 zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi, Chiligati alisema hazitakiwi kutokea kwa jamii inayohitaji maendeleo na mshikamano, huku akitoa wito kwa wananchi na viongozi kushirikiana kulinda amani na utulivu.

Chiligati alisema siasa ni mfumo unaogusa kila nyanja ya jamii na kutoa mwelekeo wa maisha ya wananchi na ustawi wa taifa kwa ujumla.

Alifafanua mazingira ya kisiasa huathiri moja kwa moja namna watu wanavyoishi na kufanya uamuzi wa kila siku.

Mbunge huyo mstaafu alisema siasa bora hujenga mazingira rafiki ya kiuchumi, kijamii na kiutawala kuchochea ustawi wa wananchi.

GAUDENCE MILANZI

Balozi mstaafu, Meja Jenerali, Gaudence Milanzi, alisema tume iliyoundwa inapaswa kuachwa ifanye kazi kwa uhuru.

Alisema wananchi wanapaswa kuiamini tume hiyo, akieleza kazi yake inahitaji utulivu na muda wa kutosha kufikia hitimisho lenye tija kwa taifa.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Milanzi, siasa safi hupimwa kwa matokeo katika kuleta maendeleo ya nchi, akisisitiza lengo kuu la uongozi ni kuhakikisha wananchi wananufaika na sera pamoja na uamuzi unaofanyika.

Alieleza siasa haipaswi kuwa maneno matupu, bali chombo cha kuboresha maisha ya watu kwa vitendo vinavyoonekana na kugusa mahitaji halisi ya jamii.

Balozi huyo mstaafu alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma muhimu za miundombinu, afya na elimu zinapatikana kwa usawa wananchi wa maeneo ya vijijini nao wapate fursa sawa na walioko mijini.

Alisema siasa siyo suala la kumridhisha kila mtu, bali ni kufanya uamuzi sahihi wa kustawisha taifa na wakati mwingine uamuzi mgumu kwa nia ya kuleta maendeleo ya kudumu.

DOYO

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, alisema wananchi wanatakiwa kuipokea kwa utulivu na umakini taarifa itakayotolewa na tume.

Doyo alisema matokeo yake yanapaswa kuonekana fursa ya kujifunza na kujitathmini kama taifa.

Alisema anaamini lengo la kuundwa tume kuweka wazi ukweli utakaosaidia kuboresha mifumo na kuimarisha mshikamano katika jamii.

Katibu huyo wa NLD alisema matokeo ya tume hiyo yanapaswa kuwa chachu ya kutatua matatizo yaliyokuwepo muda mrefu, kwa kuchukua hatua stahiki kulingana na mapendekezo yatakayowasilishwa.

Alisema wananchi na viongozi wanatakiwa kutumia matokeo hayo kama mwongozo wa kujenga mustakabali bora zaidi wenye amani, uwajibikaji na maendeleo endelevu.

Doyo alieleza kupitia siasa, jamii hupata nafasi ya kuchambua sera, kuibua changamoto na kupendekeza mambo ya kuleta suluhu kwa ustawi wa taifa.

Aliongeza mazingira ya kisiasa yanapokuwa tulivu na shirikishi, hutoa fursa kwa kila mtu kushiriki bila hofu, jambo ambalo huimarisha demokrasia na kuongeza uwajibikaji wa viongozi.

Kiongozi huyo alisema ghasia za Oktoba 29, zimeharibu taswira ya siasa kwa kiwango kikubwa na kusababisha baadhi ya wananchi kudhani siasa ni uadui.

Alishauri umuhimu wa kurejesha heshima ya siasa kwa kujenga utamaduni wa majadiliano ya amani na kuheshimiana, kuwafanya wananchi kuendelea kuamini siasa ni chombo cha kuchagiza maendeleo katika nchi.

HAMADI RASHID

Naye, mwanasiasa mkongwe nchini, Hamad Rashid, alisema ana matarajio makubwa na tume hiyo kwa sababu ina watu makini na wazalendo ndani ya taifa.

“Ni wazi kabisa tume itatoa majibu ya kutufariji na itatueleza umuhimu wa kutunza taifa letu,” alisema Hamad.

WAJUMBE WA TUME

Wajumbe wa tume huru ya uchunguzi ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, IGP mstaafu, Said Mwema na Dk. Stargomena Tax, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Paul Meela, mwanadiplomasia na Luteni Jenerali wa Jeshi mstaaafu.

Novemba 20, mwaka jana, Rais Dk. Samia, aliizindua tume hiyo na kuipa siku 90 kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti ya yaliyojiri.

Hata hivyo, Februari 21, mwaka huu, tume iliongezewa muda wa siku 42, huku taarifa ya uchunguzi ikitarajiwa kuwasilishwa mwezi ujao.

MJUMBE WA UN

Machi 11, mwaka huu, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, alikutana na Rais Dk. Samia alipowasilisha salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.

Onanga-Anyanga alisema umoja huo unatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania, baada ya matukio ya Oktoba 29, mwaka jana.

Pia, ulipongeza kuundwa tume hiyo na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa pamoja na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya kikatiba.

Mjumbe huyo alikuwepo nchini kusikiliza maoni ya wadau na kutathmini hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani ya kabla na wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana.

Katika mazungumzo yao, Onanga-Anyanga alisema UN inaendelea kuitambua Tanzania ni nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa na kuthamini mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.

Vilevile, alikutana na kuzungumza na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na vyama vya siasa.

Aidha, alikutana na kuzungumza na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi na wadau wengine wa kisiasa, kijamii kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu masuala yaliyotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali.

Onanga-Anyanga alisema ushirikiano huo utawezesha umoja huo kupata taswira halisi ya matukio ya Oktoba 29 na jitihada zinazofanywa na serikali katika kutatua changamoto zilizojitokeza.

RAIS DK. SAMIA

Rais Dk. Samia alituma salamu za shukrani na kupongeza hatua ya Katibu Mkuu wa UN, Guterres ya kutuma ujumbe maalumu Tanzania kupata uelewa wa kina baada ya kusikiliza maoni ya wadau.

Rais Dk. Samia alisema serikali imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki, ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao umekuwa msingi wa maendeleo ya nchi.

Alieleza serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume ya Uchunguzi baada ya kukamilisha kazi yake.

Rais Dk. Samia alisema mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kuimarisha maridhiano ya kitaifa na marekebisho ya katiba.

Alisisitiza Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi.

Previous Post

RAIS DK. SAMIA ASISITIZA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI

Next Post

TAASISI ZINAZOFANYA VIBAYA KUANIKWA

Next Post
TAASISI ZINAZOFANYA VIBAYA KUANIKWA

TAASISI ZINAZOFANYA VIBAYA KUANIKWA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

RAIS DK. SAMIA APOKEA UJUMBE WA RAIS PUTIN

RAIS DK. SAMIA APOKEA UJUMBE WA RAIS PUTIN

5 months ago
 WAZIRI GWAJIMA AANIKA MIZIZI YA UKATILI NCHINI

 WAZIRI GWAJIMA AANIKA MIZIZI YA UKATILI NCHINI

4 months ago

Popular News

  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YAFUTA LESENI 40 ZA UTAFITI  WA MADINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TIMU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, WIZARA YA MAJI KUCHUANA MEI MOSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, FOUNTAIN GATE SIKU YA HESHIMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AKAGUA MJI WA AFCON FUMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?