Na MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania inalenga kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa chakula duniani kutokana na uwekezaji ambao umefanyika kwenye sekta ya kilimo.
“Matarajio yetu ya muda mrefu yameelezwa katika Dira ya Maendeleo Tanzania ya 2050. Chini ya lengo la kwanza, Tanzania inalenga kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na miongoni mwa wazalishaji 10 bora wa chakula duniani,” amesema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo akati akitoa mada kuu kwenye mjadala kuhusu Mustakabali wa Kilimo barani Afrika katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue) unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Iowa, jijini Des Moines, Marekani.
Kutokana na jitihada hizo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imefanikiwa kufikia kuwa na utoshelevu wa chakula wa asilimia 130. Alisema na kuongeza: “Mauzo yetu ya nje ya kilimo yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2021/2022 hadi kufikia dola bilioni 3.7 mwaka 2024/2025.”
Amesema nchini Tanzania, kilimo kinabaki kuwa nguzo ya mageuzi ya kiuchumi kwa kuwa hivi sasa inachangia asilimia 24.6 ya Pato la Taifa, inaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi na inazalisha takriban asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje na malighafi kwa viwanda nchini.
Akizungumzia kaulimbiu ya mjadala huo isemayo “Kabla Njaa Haijatushinda”, Waziri Mkuu alisema inahitaji uharaka, lakini uharaka lazima uambatane na matumaini. “Afrika siyo tu bara linalokabiliwa na changamoto za usalama wa chakula bali pia ina uwezo mkubwa wa kuwa mchangiaji mkubwa wa usalama wa chakula duniani. Na Tanzania inakusudia kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” alisisitiza.
“Acha tuwekeze kwa wakulima, na tuwekeze pia katika sayansi. Tuwekeze kwa vijana na wanawake. Tuwekeze katika mifumo thabiti ya chakula. Na zaidi ya yote, tuwekeze katika uwezo wa kilimo barani Afrika. Kwa kweli, kabla ya njaa haijatushinda, tuchukue hatua, tuwekeze na tuvumbue pamoja. Tujenge mifumo ya chakula inayoweza kulisha vizazi vya sasa na vijavyo,” amesisitiza.



