Na MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limemchagua Rais wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA), Mhandisi Hersi Said, kuwa miongoni mwa wataalamu watakaofundisha katika Kongamano la Kimataifa la Mpira wa Miguu Duniani litakalofanyika leo jijini Doha, Qatar.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, katika ratiba ya kongamano hilo, Hersi amepangiwa na FIFA kufundisha mada inayojikita mfumo wa mabadiliko na mafanikio kwa klabu za soka duniani.
Alisema kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha wadau, viongozi na wataalamu mbalimbali wa mpira wa soka kutoka pande zote za dunia, ambapo watatoa mada na uzoefu wao.
Baadhi ya viongozi katika tasnia ya soka duniani ambao watahudhuria katika kongamano hilo ni kocha wa zamani wa Arsenal, Arsène Wenger, Roberto Di Matteo, Dennis Wise, Alexandre Pato, Eric Abidal na wengine.
“Hersi ameteuliwa na FIFA kuwa mmoja wa wataalamu ambao wamebobea katika soka kwenda kutoa mada katika kongamano hilo na atakutana na wadau mbalimbali,” alisema.
Hersi anakuwa mtaalamu pekee wa soka kutoka Afrika aliyepata fursa ya kuchaguliwa na FIFA kufundisha katika kongamano hilo.
Hatua inayotafsiriwa kama heshima kubwa kwa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla ikiwemo kutambua mchango wake katika maendeleo na uendeshaji wa klabu za mpira wa miguu kwa viwango vya kimataifa.




