Na NASRA KITANA
WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama kwa muda kupisha mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), hadi sasa mabao 104 yamshafungwa katika mechi 62 zilizochezwa huku kadi za njano zikiwa zimetolewa 162 na nyekundu sita.
Yanga na JKT Tanzania ndiyo timu ambazo zimefunga mabao mengi zaidi hadi sasa ligi hiyo ikiwa imesimama katika raundi ya 12 zikifuatia Simba na Pamba Jiji huku KMC ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi.
Kwa mujibu wa takwimu, Yanga imefunga mabao 12 baada ya kushuka dimbani mara sita sawa na JKT Tanzania ambayo imeshuka dimbani mara 10 huku Simba akifunga mabao 11 baada ya kucheza mechi tano sawa na Pamba jiji ambaye imeshuka dimbani mara tisa huku KMC ikiruhusu mabao 14 katika mechi tisa.
Pia Yanga imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja pekee ikiwa ndiyo timu iliyofungwa mabao machache zaidi hadi hivi sasa huku Azam ikifungwa mabao mawili huku Simba ikiruhusu mabao matatu.
Kwa upande wa Mbeya City imefungwa mabao 13 na Fountain Gate FC ikifungwa mabao 12.
Kwa upande wa wafungaji, hadi hivi sasa kinara wa mabao ni Paul Peter aliyefikisha mabao matano, akifuatiwa na Salehe Karabaka (manne) wote wanatokea JKT Tanzani.
katika orodha ya wafungaji, nafasi ya tatu inashikiliwa na Jonathan Sowa wa Simba mwenye mabao matatu sawa na Peter Lwasa wa Pamba Jiji na Fabrice Ngoy wa Namungo FC.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa msimu huu ligi ni ngumu kwani hata wao hadi sasa wahafikirii suala la kuwa mabingwa.
“Tuongee tu ukweli ligi imekuwa ngumu kila timu imejipanga vizuri kuhakikisha inapata matokeo, hatuwezi kusema sisi Yanga tutakuwa mabingwa msimu huu kutokana na ubora wa kila timu,” alisema Kamwe.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema msimu huu hakuna kupumzika kwani kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri, hivyo inabidi kupambana.
“Tuna msimu mgumu, hadi sasa hutujui mpinzani anakujaje kinachotakiwa kwa hivi sasa ni kupambana na kupata pointi tatu kila mchezo,” alisema Ahmed.
Naye mchambuzi soka, Kennedy Mwaisabula alisema kuwa ameona mechi za msimu huu ushindani ni mkubwa tofauti na ilivyokuwa awali, hivyo timu kiukweli ni msimu mgumu tofauti na uliopita hivyo kila timu inatakiwa kuchanga karata zake vizuri.
“Msimu huu ni tofauti na uliomalizika, kila timu imejipanga vyema kuhakikisha inapata ushindi kikubwa ambacho ninataka kuwaambia kila timu inatakiwa kuchanga karata zake vizuri ili kuhakikisha wanapata ushindi na kufikia malengo,” alisema Mwaisabula.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, JKT Tanzania inaongoza ikiwa na pointi 17 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 16 sawa na Pamba Jiji, nafasi ya nne ikishikiliwa na Mashujaa FC yenye pointi 13, Simba nafasi ya tano na kujizolea pointi 12 huku KMC wao ikiburuza mkia ikiwa na pointi nne.




