Na MUSSA YUSUPH, Dodoma
AMIRI Jeshi Mkuu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameandika historia kubwa ya kukamilisha ndoto ya Hayati Julius Nyerere, baada ya kuzindua Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, ambayo ni ya kwanza tangu kuundwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 1964.
Uzinduzi huo, umeiweka Tanzania miongoni mwa nchi chache za Afrika, zilizowekeza ipasavyo kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama, ambapo sh. bilioni 121.5 zimetumika kwa awamu ya kwanza na sh. bilioni 318.7 zinatarajiwa kutumika kwa awamu zote tatu.
Rais Dk. Samia, alisisitiza makao makuu hayo yatumike kuimarisha, kusimamia ulinzi wa taifa, kituo cha fikra, uchambuzi wa kitaalamu na uratibu wa kisayansi wa shughuli za ulinzi zinazoendana na wakati.
Akizungumza katika uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa yaliyopo Kikombo jijini hapa, Rais Dk. Samia, alisema hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika nchini.
“Mazingira ya kiusalama katika dunia tuliyokuwa nayo hayalindwi kwa silaha peke yake, bali nyenzo muhimu, uchambuzi, matumizi ya taarifa, teknolojia, mifumo ya mawasiliano na mbinu za kisasa.
Alisisitiza: “Ujenzi huu ni msingi muhimu wa uhuru na maamuzi ya taifa letu. Tukilinganishwa na nchi zingine za Afrika, tutakuwa moja ya nchi zilizotoa kipaumbele katika shughuli za ulinzi wa taifa letu.
Alisema alipotembelea jengo hilo, alishuhudia uwepo mazingira bora na vitendeakazi vya kisasa, ambapo aliahidi serikali itahakikisha awamu mbili za ujenzi zilizosalia inakamilishwa.
UMUHIMU WA KULINDA AMANI
Rais Dk. Samia alisema Desemba 15 mwaka jana, alipewa heshima ya kufungua mkutano wa tisa wa Mkuu wa Majeshi na makamanda uliobeba kaulimbiu: “Ulinzi imara na amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yetu.”
Alisema kaulimbiu hiyo inakumbusha kila hatua ya maendeleo yaliyofikiwa, yamejengwa kupitia msingi wa utulivu, nidhamu na ulinzi thabiti kwa wananchi.
“Jinsi taifa letu linavyokuwa kiuchumi ni kiashiria hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika. Bila uimara wa ulinzi na usalama tusingefika hapa tulipofikia.
“Hakuna uwekezaji bila mazingira salama, hatuwezi kusimamia ustawi wa taifa bila amani. Juzi shirika bobezi linalofanya tathmini ya ukuaji hali ya uchumi duniani The moodies, limeipa nchi yetu alama ya B1 daraja ambalo ni kiwango kizuri kwa mustakabali wa ukuaji wa nchi yetu.
Aliongeza: “Tunapokuwa kiuchumi, uwekezaji katika sekta ya ulinzi ni suala lisiloepukika kutokana na umuhimu wake kwa mustakabali wa taifa kimaendeleo.”
Alisema serikali itaendelea kuliwezesha jeshi katika mazingira bora ya kazi ili wakati wote litekeleze majukumu kwa ufanisi.
Alibainisha taifa lolote duniani linalotaka kuheshimiwa, halina budi kuwekeza kwa kujenga taasisi imara, kulinda uhuru na usalama wa mipaka yake.
Alisema nguvu ya jeshi haitokani na majengo au vifaa peke yake, bali msingi wa jeshi imara ni moyo wa kizalendo, nidhamu, weledi, utii, dhamira safi, uadilifu na uaminifu wa askari wake kwa taifa na watu wake.
“Utii kwa mamlaka ya kikatiba na uaminifu kwa taifa ndiyo silaha ya kwanza ya jeshi linaloheshimika, hivyo muendelee kuishi kwa misingi ya kiapo chenu na kuepuka mienendo inayoweza kuharibu heshima ya jeshi letu.
“Taifa lina imani nanyi na imani hiyo ni dhamana kubwa mliyopewa na Watanzania. Ninatoa wito kwa Watanzania kuendeleza wajibu wao wa kikatiba katika kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisisitiza.
WAZIRI AELEZA HISTORIA
Awali, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dk. Rhimo Nyansaho, alisema baada ya kuanzishwa JWTZ Septemba Mosi mwaka 1964, wakati huo makao makuu yaliyokuwepo Upanga jijini Dar es Salaam, yalikuwa majengo ambayo Nyerere aliomba jeshi lihamie kwa muda.
Alisema mwaka 1974 mpango wa ujenzi wa makao makuu ya ulinzi ulianza, hata hivyo haukutekelezwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo vita vya Kagera.
Alisema mwaka 2014 wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Dk. Jakaya Kikwete, serikali ilipanga kujenga Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika kambi ya Lugalo jijini Dar es Salaam ambako jiwe la msingi liliwekwa.
“Mwaka 2019 baada ya kuhamia Dodoma tukawa na mpango ambao sasa ndani ya uongozi wako umeweza kutekeleza mipango iliyopangwa tangu mwaka 1964.
Kupanga ni kuzuri lakini kutekeleza ni kuweka alama.
“Jengo limetekelezwa kuendana na dhamira ya kuwa na jeshi la kisasa lenye miundombinu na silaha za kisasa. Tunayo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ambayo huwezi kutekeleza bila kuwa na amani kupitia ulinzi wa taifa.
Alisisitiza: “Hii inaonyesha dhamira yako ya dhati katika utekelezaji wa Dira 2050 unaoendana na ulinzi imara utakaowawezesha wananchi kufanya shughuli za maendeleo tukiwa imara.”
MCHAKATO WA UJENZI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Faraji Mnyepe, alisema ujenzi wa makao makuu hayo utatekelezwa kwa awamu tatu.
Alisema awamu zote inakadiriwa sh. bilioni 318.7 zitatumika na awamu ya kwanza zimetumika sh. bilioni 121.5.
Alibainisha kati ya fedha hizo za awamu ya kwanza, sh bilioni 70.9 zilitumika kujenga jingo, sh. bilioni 50.85 kununua samani, kujenga barabara za ndani, majengo ya huduma, maji na umeme.
“Awamu ya pili itagharimu sh. bilioni 107.59 ambazo zitahusika kujenga jengo la tawi la utawala, jengo la mahusiano ya kimataifa na makazi ya askari.
“Awamu ya tatu itagharimu sh. bilioni 90 ambazo zitatumika kujenga makazi ya maofisa, majenerali, huduma mbalimbali na nyumba za watumishi. Miradi hiyo itaanza pindi mchakato wa maandalizi kukamilika,” alisisitiza.
Aliongeza: “Wakati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, ujenzi wa makao makuu haya ulikuwa umefikia asilimia 10 na sh. bilioni 10 zilikuwa zimetumika. Uongozi wako (Rais Dk. Samia) umetoa sh. bilioni 111.49.”
KAULI YA MKUU WA MAJESHI
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, alisema ujenzi wa makao makuu hayo yalianza Machi 10, 2020, baada ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, kuweka jiwe la msingi.
Alisema Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa ni ya kwanza katika historia ya jeshi tangu kuanzishwa mwaka 1964.
Alisema mchakato wote wa ujenzi wa jengo hilo ambalo litakuwa na ofisi za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga na Makao Makuu ya Jeshi (Ngome), limejengwa kwa mfumo wa “force account” kuanzia usanifu, usimamizi, ushauri na ujezi.
Jenerali Mkunda alisema jengo hilo lina miundombinu ya ulinzi wa jengo na watu wanalolitumia,ambapo ujenzi umejumuisha jengo kuu, majengo saidizi, miundombinu wezeshi na samani.
UZINDUZI WAFANA
Viongozi mbalimbali, maofisa wa jeshi, askari, wageni waalikwa na wananchi walianza kuingia katika eneo la uzinduzi kuanzia saa moja asubuhi.
Msafara wa Amiri Jeshi Mkuu Rais Dk. Samia uliwasili saa tatu asubuhi, akiwa amevaa sare za jeshi ambapo alikwenda jengo kuu alikoandaliwa gwaride maalumu.
Rais Dk. Samia alikagua gwaride hilo na baada ya kukamilisha, helkopta mbili za jeshi zilipita angani zikiwa zinapeperusha bendera ya Taifa na ya JWTZ.
Baada ya tukio hilo, Rais Dk. Samia alikwenda jukwaa maalumu ambako wimbo wa taifa ulipigwa ukifuatiwa na mizinga 21.
Tukio hilo lilifuatiwa na ndege vita tatu ambazo zilikatisha juu ya anga, hatua ambayo ilinogesha zaidi uzinduzi huo wa kihistoria.
Saa 4:33 asubuhi gwaride liliingia katika kiwanja maalumu likijumuisha Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Kikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Kujenga Taifa na Kamandi ya Jeshi la Akiba.




