Na LILIAN JOEL, Arusha
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amepiga marufuku wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, kubebeshwa vidumu vya maji.
Badala yake, Dk. Mwigulu aliitaka Wizara ya Maji kuhakikisha inachimba visima katika shule zote za msingi, sekondari, zahanati, vituo vya afya na hospitali.
“Sitaki kusikia wanafunzi wanakwenda na vidumu vya maji shuleni,”alisema Waziri Mkuu.
Dk. Mwigulu alitoa maagizo hayo jijini Arusha, alipozungumza katika Mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini.
Aidha, kupitia mkutano huo, aliwataka Wajumbe wa Bodi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Nchini kusimamia kwa ufanisi sekta ya maji kuwaondolea wananchi adha ya maji.
Alisema siyo vyema bodi badala ya kutimiza majukumu yake wanageuka kuwa wasaidizi wa mtendaji wa taasisi, hivyo alizitaka kupitia upya kazi zao, ikiwemo kusimamia, kutoa uongozi na kuchukua hatua.
“Baadhi ya maeneo yana upotevu mkubwa wa maji, pia kuna watu wamejiunganishia maji kinyemela.
“Baadhi ya mikoa unakuta kuna 50 kwa 50, yaani asilimia 50 ndiyo wanapeleka maji kwa wananchi na asilimia 50 inapotea, wakati asilimia 50 yote tungeigawa kwa wananchi, na wakati huo huo bodi ipo tu pale na tunaona ni kawaida tu kwamba maji yanapotea asilimia 50,”alisema.
Aliongeza: “Twendeni tukakague miundombinu yetu, tukomeshe kitu kinaitwa upotevu wa maji.
“Hebu tujiulize, hii asilimia 50 nayo ingeenda kwa wananchi ni lazima tungekuwa mbali kwenye suala zima la upatikanaji wa maji. Ingekuwa ni biashara ya mtu binafsi, tungeruhusu hali hiyo iendelee?”
Dk. Mwigulu alimtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuanza kuwapima wajumbe wa bodi hizo watakavyomaliza suala la upotevu wa maji.
Kuhusu watu wanaojiunganishia maji holela na hawalipi bili, Waziri Mkuu, aliagiza wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua, kwa kuwa, siyo haki wananchi masikini wanalipa bili wengine watumie maji bure.
Pia, alionya tabia ya baadhi ya wafanyakazi kufanya kazi kwa mazoea na alizitaka Bodi kuhakikisha zinasimamia vyema utendaji wa wafanyakazi ili kuleta matokeo chanya.
Naye Jumaa Aweso, alisema wizara yake, imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vijiji vyote 1,575 ambavyo havina maji vitakuwa vimeunganishwa na huduma hiyo.
Alisema kati ya vijiji 12,333, kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wamefikisha maji vijiji 10,758 na vijiji 1,575 havijapata huduma hiyo.
”Waziri Mkuu, mimi Jumaa Aweso na timu ya Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa Watanzania katika kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama,”alisema.
Pia, alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zaidi ya sh. trilioni tatu zimewekezwa katika miradi ya maji mijini na vijijini.
Aweso alisema huduma ya maji safi na salama vijijini inapatikana kwa asilimia 85.2, mijini asilimia 92.5 na kuna miradi ya miji 28 ambayo inaendelea, itakamilika na watavuka lengo la asilimia 95.
Waziri huyo alisema miradi zaidi ya 878 eneo la mjini inaendelea na itakapokamilika watavuka lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.




