Na MWANDISHI MAALUMU
MAKAMU wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameeleza umuhimu wa kuvumiliana katika utoaji mawazo.
Amesema ni vyema kushauriana na kujenga utaratibu wa kukubaliana katika masuala yenye tofauti ya mawazo.
Dk. Nchimbi alisema hayo jijini Dar es Salaam, katika Tamasha la Usiku wa Mtanzania, zikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano, zilizofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Alisema kufanya hivyo ni kuwaenzi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume.
Alisema huo ni msisitizo wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa vijana Watanzania kuhusu kuwa na mshikamano kwa lengo la kulinda umoja na amani.
Aliwasihi Watanzania kutafakari na kujielekeza katika kujenga mshikamano kwa kuhakikisha Muungano unalindwa.
WAZIRI MASAUNI
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema tamasha hilo, linalenga amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Masauni alimpongeza Rais Dk. Samia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutatuliwa hoja 22 kati ya 25 za Muungano.
Pia, alimpongeza Makamu wa Rais, kwa kuongoza Kikao cha Kamati ya Pamoja na kutatuliwa kwa hoja ya uingizaji sukari katika soko la Tanzania Bara, hivyo kuufanya Muungano kuwa imara zaidi.
Waziri huyo, alisema shughuli mbalimbali zilizofanyika katika Maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano ukiwemo uzinduzi wa miradi ya maendeleo, makongamano na mijadala kuhusu Muungano, ikilenga kutoa elimu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Masauni, serikali zote mbili kupitia vyama vya michezo, zilishirikiana katika kuandaa mashindano ya mpira wa miguu inayofanyika Zanzibar.
Alisema elimu ya Muungano itatolewa katika Msafara wa Muungano (Muungano Caravan), ambao utazinduliwa Mei 3, mwaka huu, jijini Dar es Salaam na kuhusisha wilaya zote.
KONGAMANO LA VIJANA
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, juzi alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi imara yenye amani na utulivu.
Alisema hayo Tunguu Kusini Unguja, juzi katika Kongamano la Kuadhimisha Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), akawahimiza vijana umuhimu wa mshikamano.
Rais Dk. Samia alisema wanapoadhimisha Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ana fahari kubwa ya kutamka kwamba, Tanzania imekuwa ni nchi imara yenye amani na utulivu.
Alisema katika safari ya kuijenga Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kiteknolojia na kiusalama.
“Nchi yetu kwa sasa ni imara yenye amani na utulivu, nimeacha neno mshikamano na hapa ndipo nataka vijana tutafakari neno mshikamano, ambao unaanzia katika ngazi ya vijana,”alisema.
Akaongeza: “Vijana ninyi mnakuja na vimaneno vidogo vidogo vya kufanya mbaguane, muachane msishikamane, hili nalikemea, vijana wangu niwaombe rudini katika mshikamano, msiharibu nchi yenu, kamataneni, mshikamane.
Alieleza kuwa, wakishikamana adui hatapata nafasi ya kupita, wakikubali kutenganishwa watampa adui njia ya kupita.
“Kwa hiyo, vijana wangu tushikamane, Tanzania ibakie kuwa moja, twende na mshikamano na tupendane,”alisema.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia, jukumu la kuuendeleza na kuuimarisha Muungano, liko mikononi mwao, hasa vijana wa Chama.
Pia, Rais Dk. Samia alikemea tabia hiyo ya mfarakano na kuwataka kushikamana, adui kutompa njia ya kupita na Tanzania ikabaki kuwa moja bila kugawanyika.
“Mkishakamana adui hana nafasi ya kupita, mkikubali kutenganishwa adui mnampa njia apite kwa, hivyo vijana wangu tushikamane Tanzania ibaki kuwa moja,”alisema.
Alisisitiza kuwa, hatma ya nchi ipo mikononi mwa vijana wa CCM, kuwa kitu kimoja bila ya kubaguana au kutengana kati ya Wazanzibari na Watanzania bara.
Rais Samia alisema serikali inawejengea uwezo vijana wa kiuchumi na kuiweka jamii pamoja, kuwaandalia mazingira mazuri ya kisiasa kuwapa nafasi na fursa kuendesha serikali.
Aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele na kwamba, nchi ipo mikononi mwao, haiwezekani kila sekta kuunganisha mikononi mwa vijana na kila sekta itatekeleza miradi ya vijana iliyopo katika sekta hiyo.
Rais Samia alisema Muungano huo siyo wa serikali, bali wa wananchi wote na mwanzo ulianza Muungano wa serikali, halafu vyama vya siasa.
“Tulianza Muungano wa Serikali ya Tanganyika na Zanzibar, tukafanya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baadaye tukaja Muungano wa vyama vyetu kwa kujua kwamba, umoja ndiyo mshikamano,”alisema.
Alisema vyama vya Afro Shiraz Party na TANU, viliona umuhimu wa kuungana na kuwa Chama kimoja chenye nguvu zaidi ambacho ni CCM.
“Ingekuwa umoja hauna nguvu, basi wazee wetu wasingeungana huko nyuma, umoja na mshikamano una nguvu na unalinda nchi, ndiyo maana wazee wetu wakaungana, wakashikana nasi hatuna budi kwenda mwendo hui huo,”alisema.
“Sasa sisi tunamaliza muda wetu, tunawakabidhi ninyi hatma ya nchi hii ipo mikononi mwenu vijana wa Chama Cha Mapinduzi,”alisema.
Sanjari na hayo, Dk. Samia alisema Muungano huo hivi sasa umekuwa ni Muungano uliounganisha damu ambapo Bara na Zanzibar imetengeneza familia, watu wameoa na kuolewa katika pande zote mbili.
“Wangapi wameoa Zanzibar na wangapi tumeolewa Bara, sasa mnapotaka kutengana watoto mtawapasua? Tuwe na upande huyu anakwenda bara na huyu anakwenda Zanzibar,”alihoji.
Alisema huo ndiyo Muungano unaozungumzwa, siyo tena wa serikali bali ni wa wananchi wenyewe, hivyo ni lazima kuuenzi, kuudumisha na kuutukuza.




