Na MWANDISHI MAALUMU, Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini ili kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga mbalimbali ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu, kuharibu mali na kurudisha nyuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa Juni 25, 2026 na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk. James Kilabuko, wakati akifunga Jukwaa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa lililojadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na Madhara ya El-Nino jijini Dodoma.
Amesema Tanzania imeendelea kukabiliwa na matukio ya maafa yanayosababisha athari kubwa kwa wananchi na uchumi wa taifa, hali inayolazimu kuwepo maandalizi madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo kabla hazijatokea.
“Nchi yetu imekuwa ikishuhudia matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii. Majanga hayo yamesababisha vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu,” amesema Dk. Kilabuko.
Ameeleza kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ya Aprili 28, 2026, kuhusu uwezekano wa kujitokeza kwa hali ya El- Nino, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa kuzuia madhara yanayoweza kutokea kuanzia Agosti 2026 hadi Juni, 2027.
Kwa mujibu wa Dk. Kilabuko, rasimu hiyo imejadiliwa na wadau mbalimbali kuiboresha kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana wakati wa matukio ya El-Nino yaliyowahi kutokea nchini, hususan mwaka 2023/2024.
Amesema ushirikishwaji wa wadau ni hatua muhimu itakayoiwezesha serikali kuwa na mpango shirikishi na unaotekelezeka katika kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali endapo maafa yatatokea.
“Ni vema kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yetu huku tukijielekeza kwenye athari tarajiwa na hatua za kuchukua kuwa na mpango thabiti utakaoiwezesha serikali na wadau kuchukua hatua stahiki za kuzuia au kupunguza madhara,” amesema.
Aidha, ameeleza imani yake kuwa jukwaa hilo litatoa mchango mkubwa katika kuimarisha ufanisi wa usimamizi wa maafa nchini na kuongeza uwezo wa taasisi mbalimbali kukabiliana na changamoto za majanga.
Dk. Kilabuko amesisitiza usimamizi wa maafa haupaswi kuonekana kama jukumu la taasisi chache pekee, bali unapaswa kujumuishwa katika mipango ya maendeleo na utekelezaji wa shughuli za kila siku za wizara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kujenga jamii yenye uwezo wa kuhimili majanga na kulinda maendeleo yaliyopatikana nchini dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na hali ya El-Nino na majanga mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, amesema jukwaa hilo ni muhimu na lipo kisheria hivyo litumike kwa manufaa na kuzingatia umuhimu wake.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuzikumbusha kamati za maafa ngazi kuendelea kujiandaa na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea kwa kuweka mipango madhubuti kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza hasa ya uharibifu wa miundombinu na kuepuka madhara mengine kwa jamii na taifa kwa ujumla.



