Na NASRA KITANA
RAIS wa Heshima na mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameweka wazi kuwa ana mpango wa kuweka uwekezaji wa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kujenga uwanja wa mechi na viwanja sita vya mazoezi.
Aliyasema katika Uwanja wa Uhuru,Dar es Salaam, katika kilele cha Simba Day, kuwa mpango huo unalenga kwa ajili ya timu za Simba, Simba Queens, vijana na kuboresha miundombinu ya klabu kuwa ya kisasa.
“Ninaendelea kuahidi kuwa nitajenga uwanja na viwanja sita vya mazoezi kwa ajili ya Simba, Simba Queens, Simba vijana na vituo vya mazoezi ya ndani vya kisasa, yaani gym, kambi ya malazi na ofisi za kisasa,” alisema.
Mo alifafanua kuwa uwekezaji huo, umelenga kuweka msingi imara wa programu ya vijana ndani ya Simba, huku akisisitiza umuhimu wa klabu kuwa na mfumo wa kulea vipaji.
Mwekezaji huyo alisema tayari amepeleka pendekezo la uwekezaji huo katika Bodi ya Wadhamini ya Simba na sasa anasubiri majibu ili kuanza utekelezaji.
“Nimeweka mezani pendekezo la uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 30, nimefikisha kwa Bodi ya Wadhamini ya Simba na nasubiri majibu yao, mimi niko tayari hata kesho,” alisema Mo.
Wakati huo huo, nyota wa Simba Selemani Mwalimu amewatoa hofu mashabiki wa Simba kuhusu hatma yake ndani ya timu na kuthibitisha kuwepo msimu wa 2026-2027.
Mwalimu, ambaye msimu uliopita aliitumikia Simba kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, amekuwa katika sintofahamu baada ya klabu hizo mbili kutofautiana.
Baada ya msimu wa 2025-2026 kumalizika, Simba ilitangaza kuwa imefikia makubaliano ya kuendelea na Mwalimu, lakini Wydad baadaye ilikanusha taarifa hizo.
Akizungumza kupitia video ilionyeshwa Uwanja wa Uhuru katika kilele hicho, Mwalimu aliwatumia ujumbe mashabiki wa Simba na kuthibitisha kuwa bado ni sehemu ya kikosi hicho.




