ZIANA BAKARI Na NASRA KITANA
WAMETISHA aisee, baada ya klabu ya Yanga kufanya tamasha lao la Yanga Day kukonga nyoyo za wanachama na mashabiki wa soka nchini.
Yanga iliandaa tamasha hilo, lililofanyika katika Uwanja wa Uhru Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwatalimbusha wachezaji wao wa msimu ujao wa 2026/27.
Katika tamasha hilo, lililoanza asubuhi na ilipofika saa 12.30 jioni benchi zima la ufundi lilitambulishwa rasmi, likiongozwa na Kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi.
PACOME
Pia, Pacôme Zouzoua alituma ujumbe kwa wanachama, mashabiki, wachezaji wenzake ambapo Msemaji wa klabu ya Yanga, Ally Kamwe alisema jana mchezaji huyo alishindwa kufika kwa vile alikwenda hospitali.
Akisoma ujumbe mfupi wa Pacome, Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto aliwashukuru mashabiki na kueleza Pacome anawapenda sana.
Baada ya hapo, walianza kutambulishwa wachezaji ambapo alianza Max Nzengeli, Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’, Mudathir Yahya na wachezaji wengine.
Kivutio kikubwa katika utambulisho wa wachezaji wapya wa Yanga, kilikuwa nyimbo laini zilizokuwa zikitumbuizwa na wasanii wazungu.
Hata hivyo, furaha ya mashabiki wa klabu ya Yanga iliibuka baada ya kipa Djigui Diarra kuongeza mkataba mpya ambapo amesaini miaka miwili.
Awali, kulikuwa na tetesi kuwa Diarra alikuwa aondoke kitu ambacho kimezimwa rasmi jana.
Pia, Yanga imewapandisha nyota wawili kutoka kikosi cha pili na kuingia kikosi cha wakubwa kwa ajili ya msimu ujao na kuwatambulisha rasmi.
Wachezaji hao ni Salehe na Kazimoto ambao msimu ujao wataonekana wakifanya vitu vyao dimbani.
MMACHINGA, DOMAYO WATOA NENO
Mshambulaji wa zamani wa Yanga, Mohamed Mmachinga alisema amefurahi kuwa mmoja wa walioudhuria tamAsha hilo la kihistoria.
Alisema kitu anachojivunia kuwa hadi sasa rekodi yake ya kupachika mabao 26 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, imekuwa ngumu kuvunjwa.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Frank Domayo aliiupongeza uongozi wa klabu ya Yanga kwa kuandaa vizuri tamasha la Yanga Day.
WASANII
Katika tamasha la Yanga Day, waliongeza burudani kwa
kuwakutanisha mastaa mbalimbali wa muziki Tanzania, huku wasanii muziki wa Bongo Fleva wakipewa nafasi ya kupanda jukwaani.
Miongoni mwa wasanii waliopamba tamasha hilo ni Mwasiti, Chid Benz, T.I.D, Madee, Chege, Q Chilla na Mr Blue ambao kila mmoja alitumia muda wake jukwaani kutoa burudani na kuwafanya mashabiki kuimba na kucheza.
Pia, T.I.D alivutia hisia, kutokana na historia yake kubwa katika muziki wa Bongo Fleva.
Msanii huyo ni miongoni mwa majina yaliyowahi kutawala anga la muziki Tanzania na bado ana uwezo wa kuwakumbusha mashabiki nyimbo enzi zilizopita.
Burudani hiyo, ilifanya tamasha hilo la Yanga Day kuwa tukio linalounganisha soka, muziki na mashabiki.
Lakini nyota wa filamu nchini, Prince Jimmy alisema alikwenda uwanjani kuishangilia timu yake kwa vile yeye ni shabiki wa Yanga.
JEZI NYEUSI ZATAWALA
Katika Uwanja wa Uhuru, jezi nyeusi zilivaliwa sana na mashabiki wa Yanga ambapo wengi walivaa jezi rangi hiyo.
WAFANYABIASHARA
Wakizungumza jana, baadhi ya wafanyabiashara na wajasiriamali walisema biashara ilichangamka kutokana na mashabiki wengi kujitokeza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, wafanyabiashara hao walisema ujio wa mchezo huo umeongeza idadi ya mashabiki wanaofika kununua jezi,vyakula.
Muuza jezi, Karimu Ali, alisema kuwa tangu afungue biashara yake, kumekuwa na ongezeko la wateja wanaotaka kununua jezi mpya, hasa wale wanaojiandaa kwenda kushuhudia mchezo huo.
Mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, Neema Peter anayejishughulisha na shughuli za mama ntilie, alisema kuwa ujio wa tamasha hilo, umechangia kuongeza wateja na kuongeza kipato chake.
Muuza madafu, Juma Zorro, aliishukuru klabu ya Yanga kwa kuendelea kuandaa matukio yanayowakutanisha mashabiki yamesababisha kuongeza mtaji wake.




