Na NASRA KITANA
WAKATI timu ya Azam FC, ikiivutia kasi Simba, Kocha wa timu hiyo, Florent Ibenge ameweka wazi mchezo wake dhidi ya Singida Black Stars , utakuwa moja ya maandalizi kuelekea katika mechi hiyo.
Azam FC inatarajiwa kuwa ugenini kupambana na Singida BS katika mchezo utakaochezwa Aprili Mosi, mwaka huu Uwanja wa Airtel, Singida.
Baada ya pambano hilo, Azam itapambana na Simba, Aprili 5, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuelekea katika mechi hizo mbili, Ibenge alisema kuwa maandalizi yao yanakwenda vizuri na licha ya kupitia changamoto ya kuwakosa baadhi ya nyota wake walioitwa katika timu za taifa na wengine majeruhi.
Alisema kuwa mara nyingi huwa anapenda kuona kikosi chake kikiwa na wachezaji wote wenye afya nzuri ili aweze kukijenga kiweze kuwa bora na chenye ushindani mkubwa.
“Nipo katika maandalizi ya mechi zetu mbili, nitaanza na Singida BS kwani mchezo huo utanipa nguvu na morari kubwa kuelekea katika mchezo wetu dhidi ya Simba.
“Hapa lengo langu ni kuhakikisha tunapata ushindi katika michezo hiyo yote miwili,” alisema Ibenge.
Ibenge alisema anaiheshimu Simba kwani ina wachezaji wazuri na bora, hivyo hawatakubali kuona wanapoteza kwani anahitaji pointi zote sita.
Naye mchezaji wa timu hiyo Lusajo Mwaikenda alisema kuwa wanahitaji pointi tatu katika mchezo dhidi na Singinda kabla ya kwenda kushushia kichapo timu ya Simba.
Aliongeza kwamba Simba wana timu nzuri na wamejipanga vyema, lakini wao pia wana kikosi bora chenye ushindani hivyo wataingia katika mchezo huo kwa kujiamini na kuonyesha uwezo mkubwa waliokuwa nao.
“Sisi tunaendelea na maandalizi yetu, tunakwenda kukutana na Simba iliyokuwa bora na yenye wachezaji wenye viwango vikubwa, hivyo tutapambana mwanzo hadi mwisho kuifunga na kupata pointi tatu muhimu,” alisema Mwaikenda.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29 baada ya kushuka dimbani mara 15 huku Simba ikishika nafasi ya pili na pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 14.




