• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

SIFA KEMKEMU ZA LUKUVI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 28, 2026
in Habari, Kitaifa
0
SIFA KEMKEMU ZA LUKUVI
0
SHARES
5
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na FRED ALFRED, Dodoma

WAKATI mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, ukiagwa Jijini Dodoma, jana, viongozi mbalimbali wameeleza kwamba  alikuwa kiongozi mahiri, mchapakazi, msikivu, mzalendo na mwalimu wa siasa.

Sifa nyingine za Lukuvi zilizotajwa ni ukomavu wa kisiasa, uwezo mkubwa wa ushawishi, uratibu wa shughuli za serikali na kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa.

Hayo yalielezwa bungeni Jijini Dodoma katika shughuli ya kumuaga marehemu Lukuvi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ambaye alisema msiba wa Lukuvi umewaacha Watanzania wengi katika simanzi na butwaa kwa kuondokewa na kiongozi aliyekuwa nguzo muhimu serikalini.

“Katika uhai wake, Lukuvi alitoa mchango mkubwa kwa taifa. Alikuwa kiongozi mwenye busara, ukomavu wa kisiasa, aliyekuwa na uwezo mkubwa wa ushawishi na uratibu wa shughuli za serikali,” alisema.

Aliongeza kuwa: ”Marehemu Lukuvi atakumbukwa kwa uzalendo wake, weledi kazini pamoja na kujitolea kwake, mambo yaliyomfanya aaminiwe katika awamu zote za uongozi.”

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Lukuvi alikuwa mlezi na mshauri wa viongozi wengi, hususan wabunge na mawaziri, ambao aliwasaidia alipobaini changamoto au mwelekeo usio sahihi.

“Nilinufaika sana na busara zake tangu nilipoingia bungeni. Alikuwa tayari kutoa ushauri kwa moyo wa kujitolea na kuhakikisha kazi za serikali zinafanyika kwa ufanisi,” alisisitiza.

Alisema Lukuvi alikuwa na uwezo wa kipekee wa kuelezea masuala ya kikazi kwa lugha rahisi, hali iliyosaidia kuongeza ufanisi katika wizara mbalimbali.

 “Tutamkumbuka kama kiongozi, mwalimu na mlezi, siyo tu kwa viongozi wenzake bali pia kwa wananchi wake,” alieleza.

ASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO

Dk. Nchemba, alitoa wito kwa Watanzania kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, akisema baadhi ya watu wanaposhiriki mitandaoni huonekana kama wanajua yote, wakati kwa kweli hawana uhusiano wala ufahamu wa kweli.

“Siku hizi tunatumia vibaya mtandao. Sisi hapa mitandaoni, wapo wengine wakiandika utadhani ni Mungu kaandika, hivyo lazima tuwe makini na matumizi ya mitandao.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alisema Lukuvi alikuwa mbunge mkongwe ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 31.

Alisema maisha yake yalikuwa nguzo muhimu kwa watu mbalimbali na Taifa kwa ujumla.

“Kifo chake ni pigo kubwa si kwa familia pekee bali hata bunge, serikali na watanzania wote kwa ujumla. Nimefanya kazi na Lukuvi kwa muda mrefu alikuwa kiongozi bora aliyebeba maono, mnyenyekevu na moyo wa dhati katika kulitumikia Taifa.

Aliongeza kuwa:” Lukuvi alikuwa Mserikali kwa asilimia 100 tunamuombea mwenyezi mungu ampokee,” alisisitiza

SALAMU ZA FAMILIA

Akitoa salamu za Mdogo wa marehemu Mossy Lukuvi alisema wameondekewa na baba mwema ambapo katika maisha yake aliipenda nchi yake, serikali na chama chake.

Alisema wakati wote alitanguliza maslahi ya nchi mbele kuliko yake mambo mengine.

“Lukuvi alikuwa mwadilifu na mtiifu kwa nchi na viongozi wake. Alikataa siasa za uhasama na alijitihadi kuwaleta watu, hivyo kufanya aendelee kuaminiwa na viongozi wengi,” alisema.

VIONGOZI WAMLILIA

Viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa waliozungumza katika shughuli hiyo, walimtaja Lukuvi ni kiongozi aliyekuwa nguzo ya uongozi bora na mwalimu kwa wengi.

Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Philip Mpango, alisema Lukuvi alikuwa na sifa nyingi zilizomfanya kuwa hazina kubwa ndani ya serikali na Bunge.

Alisema alitumika kufunda mawaziri namna ya kuwajibika kwa wananchi.

“Alikuwa na lugha yake ya kurahisisha kazi, alikuwa nguzo kubwa kushauri wengine ili kurahisisha kazi kwa manufaa ya Taifa,” alisema.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju alisema Lukuvi alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga uhusiano.

SALAMU ZA CCM

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongela, alisema Lukuvi ni kati ya viongozi wachache ambao walipitia ngazi zote za uongozi ndani ya Chama.

Alisema Lukuvi alikuwa hazina kutokana na uzoefu wake ndani ya Chama na serikalini.

“Tumuenzi kwa kuiga mambo mema aliyoyafanya katika uhai wake kwa ajili ya kuijenga nchi yetu,” alisema.

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Hamis Juma alisema Lukuvi alipenda utu na maendeleo.

Alisema: “msiba huu umetustua tunaomba Mwenyezi Mungu ampokee na awape nguvu wafiwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Spika wa Bunge Mstaafu, Dk. Tulia Ackson, alisema Lukuvi hakuwa na uchoyo wa maarifa katika siasa na uadilifu.

“Hakuwa mtu ambaye angefurahia baya limkute mtu mwingine ndiyo maana hakusita kutoa ushauri pindi anapoona mtu anapotea. Kupitia hilo tuendelee kumuenzi katika jambo ambalo umejifunza kutoka kwake,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga alisema amekuwa naibu waziri wa Lukuvi kwa muda mrefu na kwamba walifanya kazi nyingi kwa uzalendo.

Alisema Lukuvi alikuwa mtu wa kazi na alitanguliza mbele maslahi ya taifa.

“Nchi yetu imepoteza kiongozi mahiri ambaye alifanya kazi muda wote kwa maslahi ya nchi,” alieleza.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, alisema marehemu Lukuvi alifanya mambo mengi na makubwa ambayo yataendelea kuishi.

Alisema akiwa mkuu wa mkoa wa Dodoma ameacha alama nyingi ambazo haziwezi kufutika na ataendelea kukumbukwa.

WASIFU WA LUKUVI

Akisoma wasifu wa marehemu Lukuvi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenyeulemavu Dk. Jim Yonazi, alisema William Vangimembe Lukuvi alizaliwa Agosti 15 mwaka  katika kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi – Wilaya ya Iringa Vijijini, mkoani Iringa.

Alisenma marehemu Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri alieshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na aliesifika kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi, uzalendo, mwenye uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi na aliweka maslahi ya Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji washughuli mbalimbali za Serikali.

ELIMU

Alisema Lukuvi alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970.

Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) kuanzia mwaka 1974 –hadi 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa Cheti cha Ualimu. Mwaka 1982- 1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa .

“Alipata Shahada ya Masuala ya Kimatiafa na Diplomasia yaani Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy kutoka Washington International University kuanzia mwaka 1999 – 2001, na baadaye alijiendeleza kimasomo katika ngazi ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Huria Tanzania, ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa mwaka 2008 – 2011.

KAZI NA SIASA

Kuhusu safari yake katika siasa Dk. Yonazi alisema Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga na Chama cha TANU, akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora (TCC) na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika chuo hicho mwaka 1974 hadi 1975.

Alisema mwaka 1984 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Vikao vya Umoja wa Vijana wa CCM katika Ngazi ya Wilaya hadi Taifa.

“Lukuvi aliajiriwa kama Mwalimu katika Wizara ya Elimu kuanzia mwaka 1975 hadi 1980. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuanzia mwaka 1994 hadi 1995, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma 2006 – 2008 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam 2008 – 2010.

Aliongeza kuwa: “Katika uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa nchini uliofanyika mwaka 1995,  Lukuvi alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na hivyo kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo alilolitumikia kwa takribani miaka 30 hadi umauti ulipomkuta.

Kwa mujibu wa Dk. Yonazi akiwa mbunge aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuanzia Mwaka 2005 hadi 2010. 

Alifafanua kuwa katika maisha yake ya siasa, Lukuvi aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara kwanza alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira mwaka 1995 hadi 2000 na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu na Mnadhimu Mkuu wa Serikali hadi mwaka 2026.

“Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia Januari mwaka 2015 hadi mwaka 2022. mnamo Juni mwaka 2023 Rais Dk. Samia alimteua kuwa Mshauri wa Rais kuhusu Mahusiano ya Kisiasa na Kijamii.

FAMILIA

Dk. Yonazi alisema enzi za uhai wake, Lukuvi alifunga ndoa Julai 28, mwaka 1990 na Germina katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Jijini Dar es Salaam na kujaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Nobert William Lukuvi, Brown William Lukuvi na Anifisye Vanessa William Lukuvi.

Hadi umauti unamkuta Lukuvi ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwae Donovan.

UGONJWA NA KIFO

Dk. Yonazi alisema Lukuvi alifariki dunia Machi 25 mwaka huu  saa 1:00 asubuhi katika Hospital ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

Mwili wa Lukuvi leo unatarajiwa kuagwa Jijini Dar es Salaam ambapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza shughuli hiyo.

Previous Post

AZAM KUSAKA MAKALI KUIVAA SIMBA

Next Post

GAMONDI AITOLEA MACHO MACAU

Next Post
GAMONDI AITOLEA MACHO MACAU

GAMONDI AITOLEA MACHO MACAU

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MSAMAHA WA RAIS DK. SAMIA WAGUSA WAFUNGWA WAZEE, WENYE UJAUZITO

MSAMAHA WA RAIS DK. SAMIA WAGUSA WAFUNGWA WAZEE, WENYE UJAUZITO

4 months ago
DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

6 months ago

Popular News

  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YAFUTA LESENI 40 ZA UTAFITI  WA MADINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TIMU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, WIZARA YA MAJI KUCHUANA MEI MOSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, FOUNTAIN GATE SIKU YA HESHIMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AKAGUA MJI WA AFCON FUMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?