Na NASRA KITANA
WAKATI ikijiandaa kuikabili Macau, Kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi amesema amejipanga vyema kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo.
Stars leo itashuka dimbani kumenyana na Macau katika mchezo wa pili wa michuano ya FIFA Series 2026 utakaochezwa katika Uwanja wa Pele, Kigali nchini Rwanda.
Timu hiyo ilikubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Liechtenstein uliochezwa uwanja huo huo.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Gamondi alisema kuwa amejipanga vyema ikiwemo kuongea na wachezaji wake ili kuwajenga kisaikolojia, kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo.
Alisema kuwa kila mchezaji anajua majukumu yake, hivyo ana imani kuwa watapambana mwanzo hadi mwisho ili kuweza kushinda mchezo huo muhimu.
“Japokuwa hatukuwa na muda mwingi wa kufanya maandalizi lakini, nimekaa na wachezaji wangu nimewajenga kiakili na kisaikolojia ili tuweze kufanya vizuri na kupata ushindi,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema kuwa anajua hautakuwa mchezo rahisi, lakini amefanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza katika mechi ya kwanza ili kuweza kushinda mchezo huo.
Naye kipa wa timu hiyo, Aishi Manula alisema kuwa walipoteza mchezo wa kwanza lakini watapambana ili kupata ushindi katika mchezo unaofuata.
Alisema kuwa ni aibu kubwa endapo watapoteza tena katika mchezo dhidi ya Macau, hivyo wachezaji wote wamekuwa wakihamasishana mazoezini kuhakikisha wanapata ushindi.
“Sisi wachezaji tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapambana kwa kila hali ili kupata ushindi katika mchezo huo muhimu, tulishapoteza mchezo wa kwanza lakini benchi la ufundi limefanyia kazi makosa kuhakikisha tunawapa raha Watanzania,” alisema Manula.
Manula alisema kuwa wanawaahidi Watanzania kwa ujumla kuwa watapambana kuhakikisha wanashinda mchezo huo muhimu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema kuwa wachezaji wote wapo vizuri na wana morari ya kutosha kuelekea katika mchezo huo.
“Tulipoteza mchezo wa kwanza lakini hatutakubali kupoteza mchezo wetu wa pili, tunawaomba Watanzania waendelee kuipa sapoti timu yao ili izidi kufanya vizuri zaidi,” alisema Ndimbo.
Hii ni mara ya pili Stars kushiriki michuano hiyo ambayo imekuwa ikisimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).




