Na NASRA KITANA
KIKOSI cha Simba leo kinashuka dimbani katika mchezo namba mbili, kumenyana na Pamba Jiji katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba itakuwa ugenini kupepetana na Pamba Jiji katika mechi itakayopigwa dimba la CCM Kirumba, Mwanza kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.
Timu hiyo yenye maskani yake Mtaa Msimbazi, Dar es Salaam, itajiuliza kwa Pamba huku ikiwa na kumbukumbu nzuri baada ya kuanza ligi msimu huu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, wakati Pamba Jiji ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji.
Katika msimamo, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tatu wakati Singida Black Stars inaongoza kwa pointi tatu sawa na Yanga, inayoshika nafasi ya pili zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema timu yake inahitaji ushindi wa hali na mali kwa lengo la kutengeneza mazingira ya kuwa katika nafasi nzuri katika msimamo.
Barker alisema anaamini kikosi chake kitaingia dimbani kusaka pointi tatu kwa kucheza kwa utulivu huku kikisawazisha makosa madogo madogo yaliyojitokeza katika mechi ya awali.
“Pamba ina kikosi ambacho kimekuwa kikitoa upinzani mkali kinapocheza nyumbani, itailazimu kupambana, kucheza kwa kujihami na kutengeneza nafasi za kupata mabao,” alisema Barker.
Nyota wa timu hiyo, Kevin Nashon, alisema maandalizi waliyofanya yanawapa sababu ya kujiamini kuwa wana uwezo wa kupata ushindi katika mchezo huo.
Alisema kila mchezaji anamorari ya kutosha, kuhakikisha timu yao inaendeleza wimbi la ushindi.
Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji, John Waw, alisema timu yake imefanya maandalizi kwa ajili ya michezo yote ya ligi na si kuikabili Simba pekee.
Waw alisema anajua Simba ina timu bora, yenye uchu wa ushindi lakini atahakikisha anawaongoza wachezaji wake kupambana dakika zote 90.
Pamoja na Simba, Pamba kutoshana nguvu, michezo mingine ya ligi itazikutanisha Mbeya City na Dodoma Jiji zikipepetana Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati Kagera Sugar itacheza na Singida zitacheza Kaitaba.
Ligi Kuu msimu wa 2026/27, ilianza kutimua vumbi wiki iliyopita ambapo Yanga ilianza kwa kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC huku Singida Black Stars ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate FC huku Polisi Tanzania ikipata sare ya bao 1-1 ilipocheza na Azam FC.
Geita Gold yenye maskani mjini Geita ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City wakati Mashujaa FC ikipata ushindi wa bao 1-0 ilipoumana na Coastal Union huku JKT Tanzania ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya TRA United.



