Na Ramadhani Semtawa
ILIKUWA ndoto sasa ni halisi. Ndicho kinachoshuhudiwa na kusikika leo, kwa taifa kuzindua mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere, ambao awali ulijulikana Stiegler’s Gorge.
Ni mradi wa kihistoria unaoendeleza msingi wa taifa kujitegemea, kwani unapunguza utegemezi wa ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani na kulifanya taifa kuwa na zaida ya kuuza nje.
SAFARI YA STIEGLER’S
Lilianza wazo lenye mchanganuo wa gharama za sh. bilioni 2.5, katika kulijenga na kuzalisha megawati za juu kabisa 800, hiyo ni enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Julius Nyerere.
Agosti 25, mwaka 1976, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Bonde la Rufiji (RUBADA), Simon Nkwera, aliwaambia Watanzania bwawa la kuhifadhi maji ya Mto Rufiji kwa matumizi ya kutoa umeme na uzalishaji wa maji mashambani, litajengwa kwa thamani hiyo ya sh. bilioni 2.5.
Alifafanua, kazi ya kupiga picha ramani mahali ambako bwawa lingejengwa ilimalizika, kazi iliyobaki ilikuwa upimaji na uchoraji, ambao ungeanza Novemba 1976.
Nkwera alisema bwawa hilo lingejengwa Stiegler’s Gorge, wilayani Rufiji, likiwa na eneo la kilometa 1,130.
Kwa mujibu wa Nkwera, pia lingekuwa na barabara kutoka Chalinze hadi Stiegler’s, ambayo ni sehemu ya mpango wa kuendeleza bonde la mto huo, ingejengwa kwa lami kwa thamani ya sh. milioni 130, ujenzi ungeanza mwaka 1978 na kuchukua miaka miwili.
Kuhusu safari yake Norway, Nkwera alisema akiwa na ujumbe wa watu watatu, ulioongozwa na Kamishna wa Fedha Hazina, Deogratius Mutalemwa, walizungumza na viongozi wa Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD).
Alisema waliwaeleza wakuu wa NORAD, hatua iliyofikiwa na serikali ya Tanzania katika kuendeleza Bonde la Rufiji ukiwamo ujenzi wa barabara.
Nkwera alisema serikali ya Norway ilikubali kufanya mazungumzo na Tanzania kuhusu gharama za awali za uendelezaji wa bonde, zikijumlisha wataalamu.
Mradi wa Stiegler’s ulitayarishwa na Shirika la Norconsult la Norway mwaka 1972, ukikadiriwa kuzalisha umeme megawati 620 hadi 800, kuendeleza kilimo, viwanda vidogo, uvuvi, na kurahisisha usafiri wa mitumbwi na ngalawa katika eneo la Rufiji.
HADI JULIUS NYERERE
Hata hivyo, Julai 2019, chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, jina la mradi likawa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), sasa linazalisha megawati 2,115.
Dk. Magufuli alikuwa ni Rais wa Awamu ya Tano, na sasa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali imekamilisha ujenzi wa bwawa hilo.
Wakati Rais Dk. Magufuli akiendeleza wazo hilo la Nyerere, Rais Dk. Samia alikuwa Makamu wa Rais, ambaye baada ya kuchukua uongozi Machi 19, 2021 aliendeleza ndoto hiyo ya waasisi kwa kasi kubwa.
FAIDA KUVUTIA UWEKEZAJI FDIS
Katika dunia ambayo huongozwa kwa ushindani, uwekezaji wa moja kwa moja wa miradi ya kigeni (FDIs), pamoja na mambo mengine hutegemea zaidi nishati ya uhakika ya umeme. Hali hiyo inaakisi maono na malengo makubwa ya Rais Dk. Samia kuifungua nchi kiuchumi na kibiashara.
Uhakika wa nishati ya umeme hupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji viwandani na sekta nyingine za ubunifu, biashara na mnyororo mzima wa kazi za kiuchumi.
Katika uchumi wa maendeleo (Development economics), uhakika wa nishati ya umeme huongeza kasi ya kuondoa umasikini ukiwemo wa vijijini; kwa kusisimua mnyororo wa kuyapa thamani mazao ya kilimo, ufugaji na kwa mijini wazalishaji wadogo wakiwemo wenye saluni za nywele na wajasiriamali wa vitu vya baridi.
Katika uchumi huo wa maendeleo, pia nishati ya uhakika ya umeme huchochea uzalishaji wa viwanda vya kati na vikubwa; hivyo kuongeza kasi ya taifa kufikia katika uchumi wa wakati wa juu.
Matumizi ya TEHAMA katika huduma za kisasa za jamii ikiwemo elimu, afya yanahitaji umeme wa uhakika. Kwa mfano, Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mawasiliano ya Jamii (WSIS), unaolenga maendeleo ya watu na kuunganisha huduma za kijamii na TEHAMA, unahitaji umeme wa uhakika.
Rais Dk. Samia amekuwa akifanya uboreshaji mkubwa wa huduma za kijamii.
Hivyo, leo Tanzania inaendeleza Dira ya Taifa ya Mwaka 2050, kwa kujenga uwezo wa uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo itapelekea maendeleo ya nchi kwa kasi na pia, kutekeleza itifaki mbalimbali za kimataifa ikiwemo ya WSIS na hata Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs), yakiwemo ya kukabili mabadiliko ya tabianchi na kuondoa umasikini.




