Na MWANDISHI WETU
TANZANIA imetangaza azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, huku ikiahidi kupeleka katika chombo hicho sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.
Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unaofanyika jijini New York, Marekani.
Ndejembi amesema Tanzania ikichaguliwa itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijawa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
Tanzania imesema dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.
Katika hotuba ya Makamu wa Rais, Tanzania imeweka wazi msimamo kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, badala ya mfumo wa kimataifa kuendelea kuakisi zaidi nguvu na ushawishi wa mataifa machache.
Tanzania imesisitiza kuwa mageuzi hayo ni muhimu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba (AI), pamoja na changamoto za usalama wa nishati.




