Na NASRA KITANA
WAKATI homa ya pambano la Ligi Kuu kati ya Simba na Yanga imezidi kupanda, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker ametamba kuipepeleza Yanga.
Akizungumza Dar es Salaam, Barker alisema kuwa ameiangalia Yanga vizuri na kujua udhaifu, uzuri wao.
“Nimeiangalia sana Yanga,ninajua udhaifu wao, uzuri wao kila kitu chao ndani ya dimba na nje ya dimba,” alitamba.
Barker alifafanua kuwa hana hofu na wala haihofii Yanga kuelekea katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Jumamosi kuanzia saa 1:00 usiku.
Katika pambano hilo, Simba itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa dabi ya Kariakoo.
“Kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huo, ndio maana tunaendelea kufanya maandalizi ya kutosha, nina imani tutapata pointi tatu muhimu.
“Kiukweli sina hofu na mchezo huo japokuwa mara nyingi umekuwa na presha kubwa, lakini kutokana na kikosi nilichokuwa nacho nina imani kuwa tunashinda,” alisema Barker.
Wakati huo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema ujio wa kocha Barker umeongeza hali ya kujiamini ndani ya kikosi hicho.
“Niseme ukweli kwamba kocha wetu, Steve Barker ana kiburi cha kujiamini, kwani tangu amefika katika kikosi chetu, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa na wachezaji wamekuwa wakijiamini tofauti na ilivyokuwa mwanzoni,” alisema.
Ahmed alisema hali hiyo si jambo jipya kwa Barker akieleza kuwa hata alipokuwa akiifundisha Stellenbosch ya Afrika Kusini, alikuwa na ujasiri wa kushindana na Mamelodi Sundowns, moja ya timu yenye mafanikio ya soka barani Afrika.
Hata hivyo, Ahmed alitangaza viingilio vya mchezo huo ambapo kiingilio cha chini ni Shilingi 20,000 kwa mzunguko huku VIP ikiwa ni Sh. 50,000.
Ahmed alisema maandalizi yote ya kiufundi na kiutawala yamekamilika kuelekea mchezo huo na ana imani watapambana vizuri kupata matokeo.
Timu hizo zinaenda kukutana katika mchezo huo huku wote wakiwa na rekodi ya kushinda michezo sita ya mwanzo ya Ligi Kuu na zina alama 18 kila mmoja kwenye msimamo wa michuano hiyo.
Simba na Yanga zilikutana mara ya mwisho katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam tarehe 3 Mei, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya 2-2.




