HANIFA RAMADHAN Na
KHATIB SULEIMAN, Zanzibar
KWAHERI Bibi Fatuma Karume. Ndivyo tunavyoweza kusema kwa sasa, baada ya maziko kufanyika jana, Zanzibar, ambapo umauti ulimfika juzi usiku.
Bibi Fatuma, alikuwa mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh, Abeid Amani Karume.
Safari yake ya mwisho imehitimishwa katika makaburi ya familia, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Bibi Fatuma Karume alizaliwa mwaka 1929 katika kijiji cha Bumbwini, wilaya ya Kaskazini B, Unguja na alipata elimu ya msingi katika Shule ya kijiji hicho kabla ya kuolewa na hayati, Abeid Amani Karume mwaka 1944, ambaye baadaye alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Atakumbukwa daima, kwani katika kipindi cha uhai wake alishiriki kikamilifu katika harakati za mapambano za kudai uhuru wa Zanzibar, kutoka kwa watawala wa Sultani wa Oman kwa kushirikiana na mumewe ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Chama Cha African Association.
Bibi Fatuma Karume (97), anatajwa kuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa na ushawishi mkubwa katika harakati za siasa za ukombozi wa Zanzibar, ambapo alishiriki kikamilifu katika kuanzishwa kwa Umoja wa wanawake wa ASP, mwaka 1959.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi, Khadija Jabir, alisema Bibi Fatuma, alifanya kazi kubwa na hatimaye kuishawishi serikali ya Uingereza kubadilisha sheria na kuruhusu wanawake kupiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1959.
Itakumbukwa katika uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1957 wanawake hawakuruhusiwa kupiga kura.
Jabir alisema ushawishi huo ulitokana na ujumbe wa hayati Mwalimu Julius Nyerere kufika Zanzibar ukiwa safarini kwenda Tanga kukitangaza Chama Cha TANU, ambacho wakati huo ndiyo kinazaliwa kutafuta uhuru wa Tanganyika.
Alisema katika ujumbe aliofuatana nao, Mwalimu Nyerere alikuwepo mwanamke mmoja kutoka Marekani, ambaye alishangazwa katika mkutano wa kisiasa kutowaona wanawake.
”Bibi Fatuma Karume, alifanya mawasiliano na mazungumzo moja kwa moja na serikali ya Uingereza na kuitaka kubadilisha msimamo wake kuruhusu wanawake kushiriki katika harakati za kisiasa ombi ambalo lilikubaliwa,” alisema Khadija Jabir.
Kwa mara ya kwanza, wanawake wa Zanzibar walishiriki katika uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1959 na hivyo kuwa nguzo na tegemeo katika siasa hadi leo.
Aidha, Bibi Jabir alisema Bibi Fatma alitumia nafasi yake kuwa karibu na wanasiasa mbalimbali wakati huo, ambapo alitakiwa na Mzee Karume kujiandaa kuanzisha Umoja wa wanawake nchini UWTZ.
Alishirikiana na wanasiasa maarufu kutoka TANU akiwemo, Bibi Titi Mohamed na Lucy Lameck, kuanzishwa kwa umoja wa wanawake wa ASP, ambao ulishiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa na baadaye Zanzibar kupata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Kisultani wa Oman.
”Tulifanikiwa kuunda umoja wa wanawake wa ASP na kuanzia hapo tulifanya kazi za kuwaunganisha wanawake wote waliopo mjini na vijijini kujiunga na umoja huo, huku Bibi Fatma akiwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja huo,” alisema.
Kada wa CCM, Baraka Shamte alimtaja, Bibi Fatuma Karume, alikuwa nguzo imara aliyesimama kidete kuona kwamba wanawake wanasimama mstari wa mbele katika uongozi bila ya kuonewa.
Shamte alisema yeye akiwa katibu wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa ASP, alifanya kazi bega kwa bega na Bibi Fatuma, kuona kwamba wanasimamisha jumuiya hizo ambazo zilikuwa tegemeo katika harakati za ukombozi wa mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa mfano, alisema Bibi Fatuma, alitumia nafasi ya kuwa mke wa rais na kuimarisha umoja wa wanawake wa ASP, ambao baadaye uliungana na Tanganyika na kuzaliwa Umoja wa Wanawake wa Tanzania uliopo sasa UWT.
”Akiwa mke wa rais wa Zanzibar, Bibi Fatma Karume, hakuuacha umoja wa wanawake licha ya kujiondoa katika nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja na kubakia kuwa mlezi…alituunga mkono kwa kiasi kikubwa hadi kusimama kikamilifu kwa umoja,” alisema.
Baada ya kifo cha mumewe hayati Karume, Bibi Fatma Karume, aliamua kurudi kijijiji kwao alipozaliwa Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B na kuishi na wananchi wa kawaida katika maisha yake.
Mbunge wa Jimbo la Bumbwini Mwinyi, Jamal Ramadhan, alisema wameondokewa na miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho ambaye aliwapenda wananchi na kushirikiama nao katika harakati za maendeleo na kisiasa.
Kwa mfano, Bibi Fatma, siku zote alikuwa akishiriki katika mikutano ya maendeleo ya jimbo la Bumbwini, ikiwemo kuona miradi ya maendeleo ya ujenzi wa shule, hospitali wajawazito na watoto inatekelezwa kikamilifu.
”Tumepata pigo kubwa la kuondokewa na mwanakijiji ambaye alikuwa akiishi hapa, huku akifuatilia ujenzi wa miradi ya maendeleo ya sekta tofauti ikiwemo elimu na miradi ya ujenzi wa hospitali kwa wajawazito na watoto,” alisema.
Aidha, aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Bumbwini Mtumwa Peya, alisema marehemu Bibi Fatma Karume, alifurahishwa na kipindi cha miaka kumi kwa jimbo hilo kupata mwakilishi mwanamke.
“Kwa mfano, katika mikutano ya hadhara ya kisiasa ya kampeni tukipata nafasi ya kuamwalika yeye husisitiza na kuwataka wanawake kusimama kidete katika nafasi za uongozi wa kisiasa,”alisema.
Aidha, alitoa mfano wa Rais Dk. Samia, kushika nafasi ya juu ya urais na kusisitiza hayo ndiyo malengo ya mapinduzi ya Zanzibar ya kuona wanawake wanashika nafasi za uongozi na siyo kubaki mkiani.
”Bibi Fatma Karume alikuwa akipenda sana kuona wanawake wanashika nafasi za juu za uongozi wa kisiasa, huku akimtaja Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kama dira ya kuigwa na wanawake wengine, ”alisema.
Aidha, mjukuu wa Bibi Fatma ambaye alipewa jina la bibi yake Fatma Amani Abeid Karume, alisema walimpenda sana bibi yao kwa sababu na yeye alikuwa na upendo mkubwa na wajukuu zake wote bila ya kuwabagua.
”Bibi alikuwa kipenzi chetu kwa sababu na yeye alikuwa akitupenda sana, huku akitusaidia kwa hali na mali katika mambo mbalimbali ikiwemo ya kifamilia,”alisema Fatma ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Aidha, mwandishi wa habari mkongwe, Enzi Talib, ambaye alipata kuwa mwandishi wa rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume, alisema Bibi Fatma alikuwa mwanamke jasiri mwenye uthubutu mkubwa, ambaye daima alitaka kuona mwanamke anakuwa mbele na siyo nyuma.
”Mimi nilikuwa mwandishi wa habari wa Rais Karume, kwa hivyo katika baadhi ya safari tulikuwa tukisafiri na Bibi Fatuma ambaye alikuwa jasiri na kiongozi wa kupigiwa mfano aliyefanikiwa kuanzisha Umoja wa Wanawake wa ASP na kusaidia katika harakati za mapambano ya kisiasa ya kudai uhuru,”alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taifa UWT, Zainab Shomari, alitoa masikitiko yake makubwa ya kifo cha hayati, Bibi Fatma Karume, ambaye alikuwa nyota na mwasisi wa umoja wa wanawake kutoka ASP na baadaye kuwa umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi.
”Tumepoteza kiongozi shujaa, jasiri aliyeacha alama nyingi za uongozi katika kuona wanawake wanapata safari nzuri ya maendeleo ya kushika uongozi,”alisema Shomari.




