Na NASRA KITANA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amefafanua utata uliojitokeza katika jezi mpya za Timu ya Taifa , zilizozinduliwa hivi karibuni na kampuni ya Sandaland na kusema ni mbaya.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Makonda amesema jezi ya timu ya taifa, ni sehemu ya utambulisho na nembo ya nchi, hivyo haipaswi kuzinduliwa au kutangazwa bila kushirikisha mamlaka husika.
Makonda amesema jezi hizo mpya hazina ubora hivyo anataka zibadilishwe.
“Mimi ukiniambia kuhusu jezi, jezi hizi ni mbaya, cha msingi hangaikeni kutafuta jezi nzuri, Tanzania tunahitaji jezi yenye ubora pamoja na mfumo mzuri wa kibiashara utakaowezesha mashabiki kuipata kwa urahisi.
“Timu ya Taifa ni mali ya nchi, siyo ya mtu binafsi wala kampuni, na sisi kama mamlaka tuliyonayo tumeikasimu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litusaidie kusimamia timu ya taifa, hivyo suala la jezi linapaswa kupewa uzito unaostahili kwa sababu linahusisha utambulisho wa taifa,” alisema.
Makonda amefafanua kuwa, Taifa Stars ni timu inayoiwakilisha nchi, hivyo hatua zote muhimu zinazoihusu zinapaswa kufahamika.
Amesema tangu Februari mwaka huu, kulikuwa na vikao vilivyohusu maandalizi ya jezi mpya ya Taifa Stars na mchakato huo unapaswa kuhusisha wadau na mamlaka zinazohusika.
Makonda amesema jezi ya Taifa Stars siyo vazi la kawaida, bali ni sehemu ya utambulisho wa Tanzania, hivyo mchakato wa kuitengeneza, kuitambulisha na kuiuza unatakiwa kupewa uzito unaostahili.
Waziri huyo ameitaka TFF kuhakikisha inakaa chini na mzabuni wa kutengeneza jezi ili kuboresha jezi hizo na endapo itashindikana serikali itaangalia utaratibu mwingine.
Ameongeza kuwa, alijiuliza maswali 22 kuhusu mkataba unaohusu jezi hiyo, akisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza zingeweza kuepukwa iwapo wadau wote wangekuwa na uelewa na kushirikishwa katika mchakato.
Amesema mjadala kuhusu jezi hiyo, haupaswi kuishia katika suala la mwonekano au ubora wake pekee, bali unapaswa kuangalia uwezo wa kampuni au mzabuni anayesimamia mauzo yake.
Pia, amesema mkataba kati ya TFF na Sandaland unaibua maswali kuhusu utekelezaji wake, ikiwamo mapitio yaulipaji wa kodi na mapato yanayopatikana kutokana na mauzo ya jezi ambapo TFF na mzabuni wanatakiwa kufanya mapitio kila mwaka.
Kwa mujibu wa Makonda, Sandaland amepaswa kutoa vifaa vya michezo na kushirikisha TFF katika faida inayotokana na vifaa vilivyotengenezwa, huku TFF ikitarajiwa kulipwa sh. milioni 300 kwa mwaka.
Amesema utaratibu huo haujaonesha ongezeko la mauzo wala faida inayotarajiwa kwa TFF na timu za taifa.
Makonda amesema kuna hali ya kupanda kwa bei ya jezi huku mapato kwa TFF hayaongezeki, licha ya timu za taifa kuendelea kufanya vizuri na kuongezeka kwa idadi ya timu.
Ameeleza ni muhimu kuhakikisha jezi hiyo inawafikia Watanzania kwa urahisi kupitia mkakati madhubuti wa usambazaji na mauzo.
Kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, amesema yanatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu.
Aidha, Makonda amesema viwanja vingi vitakavyotumika kwa maana ya mazoezi na kuchezea michuano hiyo, viko katika hatua nzuri.
Makonda amesema serikali inaendelea kusimamia kwa karibu kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo kuhakikisha miundombinu ya michezo inakidhi viwango vinavyohitajika.
Kwa upande wa Zanzibar, Makonda amesema ujenzi wa Uwanja wa Fumba umefikia asilimia 85, Uwanja wa Arusha nao umefikia asilimia 95 huku Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa umebaki sehemu chache kukamilika.
Waziri huyo amesema serikali imetoa sh. bilioni 104 kuandaa AFCON 2027 na kupata haki ya matangazo katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Amesema fedha hizo zimelipwa kama sehemu ya gharama za Tanzania kupata haki ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, akieleza kuwa serikali inalenga kuhakikisha nafasi hiyo inatumika zaidi ya michezo na kuwa fursa ya kuitangaza Tanzania duniani.
Akizungumzia maandalizi ya Miss World, Makonda amesema Wizara imetia saini mkataba na waandaaji wa Miss Tanzania na kwamba idara husika inaendelea kukamilisha mchakato wa kuunda kamati itakayoratibu maandalizi ya nchi kuwa mwenyeji wa shughuli hizo mwakani.
Amesema Tanzania inatarajiwa kupokea washiriki kutoka nchi 126, hivyo serikali inataka maandalizi yaanze mapema kuhakikisha fursa zitakazotokana na ujio huo zinawanufaisha Watanzania.
Makonda amesema matukio makubwa ya Miss World yatafanyika Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha, huku washiriki wakipelekwa katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii. Pia alisema Serikali inalenga kutumia mashindano hayo kukuza utamaduni wa Tanzania, ikiwamo kila mshiriki kutambulisha kabila moja la Tanzania.
Pia, amesema kutakuwa na juhudi za kukuza Kiswahili kupitia Miss World, ukiwamo wimbo wa mashindano hayo kutafsiriwa kwa Kiswahili na kupelekwa katika mataifa mbalimbali ili kusaidia kuitangaza lugha hiyo kimataifa.




