ABDUL DUNIA Na NASRA KITANA
WAKATI michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 ikitarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco, wadau mbalimbali wa soka nchini wametoa maoni tofauti nini kifanyike timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, ifanye vizuri katika fainali hizo kubwa.
Twiga Stars ni miongoni mwa timu 16 zitakazoshiriki katika fainali za WAFCON zitakazofanyika Machi 17 hadi Aprili 3, mwakani.
Timu hizo ni Tanzania, Zambia, Morocco, Malawi, Algeria, Nigeria, Ghana, Burkina Faso, Kenya, Afrika Kusini, Cape Verde, Senegal, Cameroon, Ivory Coast, Mali, Misri.
Hata hivyo katika WAFCON yake hiyo ya tatu katika historia, Twiga Stars haijawahi kutinga hatua ya mtoano, mara zote mbili zilizopita ikiishia makundi na kuburuta mkia.
Katika michuano hiyo, Tanzania imewahi kufuzu mara tatu ikianza hivyo mwaka 2010, 2024 na 2026.
Katika mara yake ya kwanza mwaka 2010, Tanzania iliburuta mkia katika kundi A bila ya pointi ikifungwa mechi zote dhidi ya Afrika Kusini (2-1), Mali (3-2) na Nigeria (3-0).
Pia katika fainali za mwaka 2024, Tanzania iliburuta mkia katika kundi C kwa alama moja, ikifungwa dhidi ya Mali (1-0), Ghana (4-1) na sare ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini.
Kuhusu nini kifanyika ili timu hiyo kwa mara ya kwanza itinge hatua ya mtoano, wadau mbalimbali wa soka wametoa maoni tofauti huku wengine wakielekeza macho yao kwa benchi la ufundi.
Mwandishi wa habari za michezo na mchambuzi wa soka la wanawake, Lilian Mukulu, alisema ili Twiga Stars ifanye vizuri ni muhimu wachezaji waandaliwe kisaikolojia na kufanya maandalizi ya mapema.
Alisema WAFCON ni mashindano makubwa hivyo benchi la ufundi la timu hiyo linatakiwa kuboresha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita kufanya vizuri katika mashindano hayo.
“Twiga Stars ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo endapo itafanya maandalizi ya mapema kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza, kufanya hivyo kutasaidia timu kuwa na ushindani mkubwa katika kila mchezo,” alisema Lilian.
Naye Salama Ngale ambaye pia ni mchambuzi wa soka la wanawake, alisema Twiga Stars inatakiwa kujipanga vizuri kwani timu inazokwenda kukutana nazo zina ubora mkubwa.
“Ujue ni mashindano makubwa lakini benchi la ufundi linatakiwa kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi chake na pia kuwanoa washambuliaji na mabeki kuwa bora,” alisema Salama.
Akijibu hoja hizo, Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime, alisema atahakikisha anaanza maandalizi mapema kikosi chake kipate muda mzuri wa kufanya mazoezi na kujifunza vitu vingi zaidi.
Alisema kila mchezaji aliyekuwa naye ni bora na yupo tayari kwa mashindano hayo, kwani wanajua ukubwa na umuhimu wa kupambana kupata matokeo mazuri.
“Tunakwenda katika mashindano makubwa, tunatakiwa kufanya maandalizi ya mapema, nitahakikisha timu yangu inaingia kambini mapema na kuanza maandalizi kwa mashindano hayo kwani muda huo utatusaidia kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita,” alisema Shime.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA), Somoe Ng’itu, alisema ana imani kubwa timu hiyo itafanya vizuri katika mashindano ya WAFCON mwakani.
“Sina hofu na kikosi chetu, tunakwenda katika mashindano makubwa kila aliyekuwa katika mashindano hayo ni bora lakini ninaamini timu itafanya vizuri na kuitambulisha vyema nchini yetu,” alisema Somoe.
Katika mechi za kufuzu, Twiga Stars ilianza kwa kuitoa Guinea ya Ikweta katika raundi ya kwanza kwa ushindi wa mabao 4-2 kabla ya kuifunga Ethiopia mabao 3-0.




