Na JACQUELINE LIANA, Kampala
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, amekataa ombi la kupiga marufuku mchele wa Tanzania kuuzwa katika soko la Uganda.
Rais Museveni alisema hayo jijini Kampala, alipohutubia kongamano la kimataifa lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Roho Mtakatifu na Matengenezo Makuu’, bila kuwataja waliopeleka ombi hilo kwake.
“Kuna watu wamenifuata wanataka nipige marufuku mchele wa Tanzania, lakini mchele wa Tanzania ni mzuri sana, pia bei yake ni nafuu,” alisema Museveni katika kongamano hilo lililoshirikisha wageni kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Tanzania walioshangilia kauli hiyo.
Rais Museveni alisema hawezi kumdhoofisha mkulima wa mchele wa Tanzania kwa ‘kuwabeba’ wakulima wa zao hilo nchini kwake ambao hawazalishi kwa tija.
“Kupiga marufuku maana yake ni kudhoofisha maendeleo; Waganda watalazimika kununua mchele mbaya kwa gharama kubwa,” alisema na kusisitiza:”Siwezi kuwapendelea watu ambao hawawezi kushindana sokoni.”
Alisema ni muhimu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea kuimarisha soko la pamoja na Waganda kama mchele wa Tanzania ukipigwa marufuku, Tanzania nayo itafanya hivyo kwa bidhaa za Uganda zinazouzwa katika soko lake.
“Hiyo maana yake ni kuua Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Museveni na kuongeza, Waafrika hawana budi kushirikiana kwa kuuziana bidhaa na huduma zinazozalishwa katika bara hilo.
Aliwapongeza waliokuwa Marais; Ali Hassan Mwinyi na baadaye Benjamin Mkapa wa Tanzania na Daniel Arap Moi wa Kenya kwa kushirikiana kuifufua Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokuwa imevunjika mwaka 1977 ikiwa ni miaka 10 tangu ilipoanzishwa.
Jumuiya hiyo ilifufuliwa rasmi Novemba 30, 1999 na kuanza kazi rasmi mwaka 2000 kwa dhumuni la kuimarisha ushirikiano wa biashara, soko la pamoja, sheria za forodha, na maendeleo ya kisiasa na kiusalama kwa nchi wanachama.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa Uganda, kwa sasa idadi ya watu barani Afrika ni bilioni 1.5 na miaka 30 ijayo itakuwa robo ya watu wote duniani, hivyo wingi huo ni fursa nzuri ya kufanya biashara miongoni mwa mataifa ya bara hilo.
Alieleza umoja wa Waafrika ndiyo nguvu yao katika kujenga bara tajiri kupitia rasilimali zake.
Kongamano hilo limeandaliwa na taasisi ya Miracle Centre ya Uganda inayoongozwa na Mchungaji Robert Kayanja, ambapo ukiacha washiriki kutoka nchi mwenyeji Uganda, wengine ni Kenya, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.
Pia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Malawi, Zimbabwe, Zambia, Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, China Uingereza, Marekani, Pakistan, Myanmar na Ufaransa zimeshiriki.
Awali, Mchungaji Kayanja alipomkaribisha Rais Museveni kuhutubia maelfu ya watu katika kongamano hilo, alimuomba kuzungumzia umuhimu wa utengamano miongoni mwa nchi za Afrika.
SOKO LA GHANA
Agosti 3, mwaka huu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alisema Ghana wanahitaji mchele mwingi kutoka Mbeya, lakini changamoto namna ya kufikisha bidhaa hiyo nchini humo, hivyo aliisisitiza sekta binafsi kuchangamkia fursa hiyo.
Rais Dk. Samia alisema hayo alipozindua nyenzo ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kushiriki mkutano wa mazungumzo maalumu na sekta binafsi kuhusu utekelezaji wa dira hiyo, Ikulu, Dar es Salaam.
“Mkae sekta binafsi mchemshe kichwa tunapeleka vipi bidhaa katika nchi jirani ambazo hakuna uunganishwaji wake, sisi serikali tunajitahidi kwa upande wetu, hiyo reli ya kati inakwenda hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tunajitahidi kwa upande wetu,”aliagiza Rais Samia.




