Na MWANDISHI WETU
PAMOJA na kupata ushindi wa mabao 3-1, timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 23 ya Tanzania (U-23), jana iliondolewa katika michuano ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-23) dhidi ya Kenya.
Tanzania jana ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Kenya, katika mchezo wa kufuzu kucheza AFCON U-23, uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Tanzania iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-1 dhidi ya Kenya katika mchezo uliofanyika ugenini.
Mchezo ulianza kwa kasi ambapo Tanzania ilipata bao la kwanza katika dakika ya 15 lililofungwa na Shekhan Khamis baada ya kupiga mpira wa faulo uliotinga wavuni.
Dakika ya 27, Tanzania ilipata bao la pili likifungwa kwa kichwa na Selemani Mwalimu kufuatia kupokea mpira wa krosi kutoka kwa Ashraf Kibeku.
Kenya walijibu shambulizi na kupata bao dakika ya 57 likifungwa na Andress Odhiambo kufuatia mabeki wa Tanzania kujichanganya.
Tanzania ilipata bao la tatu kupitia kwa Selemani Mwalimu kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 86 kufuatia Antony Mligo kufanyiwa madhambi eneo la hatari.
Kufuatia ushindi huo, Kenya imesonga mbele katika hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 5-4.




