Na MWANDISHI WETU, ARUSHA
UPO usemi unasema kuwa ‘maji kupwa, maji kujaa’ ambapo mabingwa watetezi Yanga, wameendelea kutokuwa na mazuri kama ilivyokuwa msimu uliopita, baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya TRA United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Matokeo hayo, yanaifanya Yanga kufikisha alama 19 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kusuka dimbani mara nane.
Wananchi wameshindwa kupunguza kikamilifu pengo la pointi dhidi ya vinara wa ligi, Simba ambao wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 24.
Ikumbukwe kuwa Yanga ilichapwa mabao 2-1 na Simba na kuondolewa katika kilele cha kuongoza ligi hiyo, kutokana na matokeo ya jana, timu hiyo ipo nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi tano.
Katika mchezo wa jana, licha ya Yanga kutawala umiliki wa mpira kwa takribani asilimia 66, timu hiyo haikufanikiwa kupenya ngome imara ya ulinzi ya TRA United inayonolewa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi huku timu zote zikionesha kupambana ili kupata ushindi, dakika ya 32 ya mchezo Albert Kangwanda alikosa bao baada ya kupiga shuti kali na mpira kupaa juu.
Timu hizo ziliendelea kufanya mashambulizi kwa zamu na dakika ya 44, Yanga ilikosa bao baada ya mchezaji wake, Kangwanda kupiga shuti kali nje ya 18 na mpira ulitoka nje ya lango.
TRA walikosa bao dakika ya 55 baada ya Ayoub Lyanga, kupiga shuti kali na mpira ulitoka nje ya lango.
Dakika ya 66, Housseine Zakouani wa Yanga alifumua shuti kali na mpira ukaingia kambani lakini mwamuzi alikaa bao hilo.
Katika dakika ya 87, Yanga ilikosa bao kupitia kwa mchezaji wake, Maxi Nzingeli baada ya kupiga mpira wa adhabu na kipa wa TRA kuokoa mpira huo.
Yanga: Abutwalibu Mshery, Mohamed Hussein/Tshabalala, Ibrahim Bacca, Maxi Nzengeli, Fred Ngoma/Mzize, Cheikh Toure/Shalulile dk 67, Albert Kangwanda, Mudthir Yahya, Seleman Mwalimu, Oumar Komara na Ibrahim Kazimoto.
TRA United: Daniel Mgore, Nassry Kombo, Sharif Majabe, Salmin Hoza, Ani Elijah, John Lazarus, Ayoub Lyanga, Suwed Juma, Geryson Gwalala, Tobias Omondi na Steve Belobo.




