Na FRED ALFRED, Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi mji wa serikali, Mtumba jijini Dodoma Oktoba 30, mwaka huu.
Serikali imewekeza kiasi cha sh. bilioni 700 katika ujenzi wa majengo na miundombinu ya mji huo wa kisasa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo jijini hapa jana, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema ujenzi wa mji huo, ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhamishia makao makuu ya serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma mwaka 2016.
Alisema baada ya ujenzi wa awali wa majengo ya wizara na kuhamia rasmi jijini Dodoma, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia, iliendeleza jitihada zilizoanzishwa na mtangulizi wake, hayati Dk. John Magufuli kwa kujenga majengo makubwa ya kisasa.
Alisema mji huo, umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya utoaji huduma kwa wananchi na kuwekwa mazingira bora ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
“Serikali imewekeza katika miundombinu ya kisasa, zikiwemo barabara za lami zenye urefu wa kilometa 59 na mifumo ya mawasiliano inayowezesha shughuli za serikali kutekelezwa kwa njia za kidijitali,”alisema.
Aliongeza kuwa, majengo na miundombinu ya mji wa serikali Mtumba, yameanza kuvutia mataifa mengine ambapo zaidi ya nchi 10, zimefika nchini kujifunza namna Tanzania ilivyotekeleza mradi huo.
UFAFANUZI FEDHA ZA EL NINO
Katika hatua nyingine, Msigwa alikanusha upotoshaji unaoendelea katika jamii kuhusu makadirio ya sh. bilioni 730 yaliyotajwa katika Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Nino kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Alisema fedha hizo, siyo bajeti mpya iliyochukuliwa kutoka mifuko ya wananchi au iliyotengwa upya na serikali kuu pekee kwa ajili ya kugawanywa, bali ni jumla ya makadirio ya rasilimali zilizopo tayari katika taasisi za serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.
Alisema taasisi za umma na sekta binafsi, vikiwemo viwanda na wafanyabiashara, hutumia bajeti zao za kawaida zilizoidhinishwa kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na El Nino.
Vilevile, alisema wananchi wanaweza kutumia rasilimali zao kujenga na kuimarisha makazi yao.
Alisema maandalizi hayo ya dharura, yanazingatia utabiri rasmi uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), unaoonesha uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu kubwa inayoweza kusababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi na milipuko ya magonjwa.
Alieleza kuwa, serikali imeendelea kuweka kipaumbele cha kulinda maisha, usalama na mali za wananchi kwa kuchukua hatua za tahadhari na kuimarisha mifumo ya utayari dhidi ya majanga.
MIRADI YOTE ITAKAMILIKA
Pia, Msigwa aliwahakikishia Watanzania miradi yote iliyoanzishwa na serikali, inaendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali na ile ambayo haijakamilika, itakamilishwa ili kuimarisha huduma kwa wananchi.
Alisema ipo miradi iliyokamilika, inayokaribia kukamilika, iliyo katika hatua za mwisho za utekelezaji na mingine ambayo bado inaendelea kutekelezwa.
Hata hivyo, alisema pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi wa Tanzania, serikali haina uwezo wa kutekeleza mahitaji yote ya maendeleo kwa wakati mmoja kutokana na ufinyu wa rasilimali ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.
“Takwimu zinaonesha uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 6.3 mwaka huu, huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia 3.4, lakini miradi ya maendeleo lazima itekelezwe kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine,” alisema.
AWATAKA WATANZANIA
KUKATAA UCHOCHEZI
Msigwa aliwasisitiza Watanzania kujiepusha na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, kwa kuwakataa watu wanaowahamasisha kufanya vitendo vinavyokiuka sheria kwa lengo la kufanikisha ajenda zao.
Alisema Watanzania wanapaswa kupuuza hamasa zinazochochea uvunjifu wa sheria na zisizo na manufaa kwa taifa, zikiwemo shughuli zinazokiuka taratibu, sheria, maadili na utamaduni wa nchi.
Alisema matukio yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana ni ushahidi kuwa, Watanzania wanapaswa kulinda amani na kutokubali kuchochewa kuharibu nchi yao.
“Pakichafuka hapa hakuna mjomba atakayekuja kutusaidia Watanzania. Tutajisaidia sisi wenyewe. Na bahati nzuri yaliyotokea mwaka jana, mwezi Oktoba tarehe 29, Watanzania wote ni mashuhuda. Ni sisi wenyewe ndiyo tulirudisha nchi yetu kwenye mstari.
Aliongeza: “Serikali inarudi kwenu kuwaambia tusikubali vitendo vyovyote vya kutuvuruga, kuharibu amani yetu, kuharibu misingi ya umoja wetu ambavyo tukivifanya hakuna wa kuja kutusaidia.”
Msigwa alisema serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, viko imara kusimamia amani, usalama wa wananchi, mali zao na ulinzi wa mipaka ya nchi.
Msigwa alionya hakuna mtu atakayevumiliwa kufanya vitendo vya vurugu au kuvunja sheria kwa kisingizio chochote, akisisitiza kila mtu anapaswa kuwajibika kwa matendo yake.




