Na MWANDISHI MAALUMU
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amezitaka wizara zinazohusika na ajira, zisimamie utekelezaji wa sheria zinazotaka kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania zisifanywe na wageni.
Ameendelea kusisitiza kazi zinazohitaji utaalamu, ndizo zifanywe na wageni kama kuna upungufu, lakini siyo vinginevyo.
Pia, Waziri Mkuu alikemea tabia ya baadhi ya wenye nyumba kumpangisha raia mmoja wa kigeni na kumruhusu apangishe watu wengine ndani ya nyumba hiyo, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na halina tija kibiashara.
Dk. Mwigulu, alitoa agizo hilo, alipofungua Kikao cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta, kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
Agizo hilo, linalenga kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kufuatia kuwepo wimbi kubwa la wageni kufanya kazi au biashara ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.
“Kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, ziachwe wafanye, siyo kuruhusu wageni wafanye. Tusioneane aibu kama tumefungua milango au kulegeza wataalamu wafuatilie. Wageni wafanye kazi za kitaalamu ambazo nchi ina uhaba wa wataalamu,” alisema.
Alisema kwamba, lazima wataalamu wa ndani wasimamie sheria ipasavyo, kama kuna maeneo yanayokwamisha wayabainishe na yafanyiwe marekebisho.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu alitoa wito kwa Watanzania kuwa na wivu na nchi yao, kutoruhusu baadhi ya vitu kufanyika, alitoa mfano wenye nyumba kumpangisha raia mmoja wa kigeni ambaye naye kuweka wenzake wengi katika nyumba hiyo.
“Watanzania tuwe na wivu na nchi yetu, mfano mtu anamkodishia nyumba mgeni kwa dola 5,000 kwa mwaka na kisha mgeni huyo, anawaleta wenzake 60 na anawakodisha dola 500 hapo Mtanzania anapata hasara, hii siyo sawa hata kwa usalama,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaagiza wahusika wafuatilie suala hilo la makazi, wakae katika utaratibu ulio rasmi.
“Eneo hili liangaliwe, wageni wanarundikana na kufanya kazi ambazo Watanzania wangeweza kufanya, hatuwezi kuruhusu hili tunataka wawekezaji,” alisema.
Waziri Mkuu, aliziagiza wizara zinazohusika zifuatilie suala hilo na wasimamie utekelezwaji wa sheria, kwa sababu kila nchi ina sheria zake na Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria.
Alisema kwamba, sheria zimetungwa kusaidia kujenga kampuni za Watanzania na kuzikuza, hivyo wizara zinazohusika zihakikishe hazisajili kampuni za kigeni kabla ya kuzifanyia uchunguzi wa kina.




