NA MUSSA YUSUPH
RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amewatolea uvivu wanaopotosha kwa kudai kwamba uteuzi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) haukufuata Katiba ya chama hicho.
Akihutubia maelfu ya wanachama wa CCM katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam, Dk. Kikwete alisema mchakato huo umefuata utaratibu wa chama ambao pia ulitumika kwa marais waliopita walipotaka kugombea awamu ya pili.
“Hao wanaosema huenda hawafahamu utaratibu wa chama, au wanajifanya hamnazo.
Tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza, ndani ya CCM tuna utaratibu kwamba Rais aliyepo madarakani akimaliza kipindi cha kwanza anapewa nafasi ya kuendelea awamu nyingine.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mkapa, kwangu na Magufuli.
Kwanini iwe nongwa kwa Samia?” alihoji huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Dk. Kikwete alibainisha kuwa mwangwi wa kauli mbiu ya “Samia mitano tena” ulitokana na azimio la mkutano mkuu wa CCM mapema mwaka huu, baada ya wajumbe kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho chini ya uongozi wa Rais Dkk. Samia.
Alisema Dk. Samia alipokea nchi katika kipindi kigumu baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, ambapo hofu ilitanda juu ya hatma ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Hata hivyo, alisema baada ya miaka minne Rais Dk. Samia amedhihirisha uwezo, ubunifu na maono ya mbali katika kuliongoza taifa.
Kikwete alitaja falsafa ya 4R, usimamizi wa mahusiano ya kidini, kuimarisha haki za binadamu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na miundombinu kama mifano ya mafanikio ya Rais Samia.
Aliongeza kuwa matumizi ya fedha za UVIKO-19 kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi ni uthibitisho wa ubunifu na uongozi wenye kulenga maendeleo ya watu.
Alisisitiza kuwa CCM kimeweka utaratibu wake na ni muhimu heshima ikatolewa kwa taratibu hizo, huku akihitimisha kuwa kauli mbiu ya chama “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” ni kielelezo cha dhamira ya Rais Samia katika kuendeleza taifa.