Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amevitaka vyama vya siasa kuepuka kufanya siasa za chuki, ubaguzi na kugawa watu kipindi cha kampeni.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Mjini Unguja, akizungumza na wananchi katika viwanja vya Mau, baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo, awamu ya pili katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Zanzibar (ZEC) Amesema wanasiasa wanatakiwa kuepuka siasa za matusi, badala yake, wajinadi kwa sera zao nzuri na kuwa, CCM itafanya siasa safi za kuwaleta watu pamoja.
“Sisi tusizungumzie watu, bali tuwaambie wazanzibari tutawafanyia nini, sina shaka kwamba wazanzibari watatuchagua sisi.
“Ndugu zangu, tutafanya kampeni za kistaarabu, tutafanya kampeni ambazo hazijawahi kutokea, shaka hata kidogo na wananchi wa Zanzibar wataendelea kutuunga mkono,” amesema.
Pia, amewataka wana CCM kuwa wamoja kwa sababu, wamemaliza mchakato ndani ya Chama na sasa, wanatakiwa kushirikiana kunadi ilani yao, CCM ishinde kwa kishindo iendelee kushika dola.
“Tufanye kazi za kuwanadi wagombea wetu katika nafasi za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani, tuhakikishe katika nafasi zote hizo Chama kinaibukia kidedea,” amesema.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29, mwaka huu kwa kukipigia Chama cha Mapinduzi kwa nafasi zote.
Amesema hana shaka kuwa, ilani wameitekeleza kwa kishindo na kiwango kikubwa na kuwa, sasa hivi wanaenda na mambo mapya ya kuibadilisha Zanzibar kuwa kama nchi iliyoendelea.
Pia, amekishukuru Chama kwa kumpitisha kwa kura za kishindo kugombea tena nafasi ya urais kwa awamu ya pili na kuwa, atahakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo.
DK. DIMWA
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed (Dimwa), alisema haa hiyo ni ishara ya kuelekea demokrasia na hatua muhimu ya ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema uongozi wa Dk. Mwinyi ni wa kupigiwa mfano, ndiyo maana wapo kumuunga mkono na kuhakikisha anashinda kwa kishindo.
“CCM itasimama imara kuhakikisha kuwa, Dk. Mwinyi anapata ushindi kubwa sana katika uchaguzi mkuu kwani amefanya makubwa ambayo yanawapa matumaini wananchi wamchague tena,” alisema.
Aliahidi kufanya kampeni za kistaarabu wakati ukifika kuleta umoja na mshikamano ndani ya nchi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini, Talib Ali Talib, alisema Chama kina kila sababu ya kupata ushindi wa kishindo kutokana na mambo makubwa yaliyofanywa na Dk. Mwinyi.
Alisema anaamini maendeleo yaliyofanywa kwa visiwa vya Unguja na Pemba wananchi wanaendelea kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu aendelee kuwatumikia tena miaka mitano inayokuja.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati Kuu ya CCM, Mohammed Aboud Mohammed, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kutekeleza ilani ya CCM ya 2020/2025 kwa zaidi ya asilimia 100.