Na AMINA KASHEBA
KOCHA wa timu ya taifa ya Soka kwa Watu Wenye Ulemavu ‘Tembo Warriors’, Ivo Mapunda, anatarajia kufanya mchujo wa wachezaji ambao watakwenda kuwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Wachezaji 25 watachujwa na kubakia 15 ambao watasafiri kwenda Burundi katika michuano hiyo itakayofanyika Septemba 6, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, Shaban Msangi amesema licha ya changamoto wanazopitia, Kocha Mapunda anatarajia kufanya mchujo wa kupunguza wachezaji ili kubaki na 15 watakakwenda nchini Burundi.
Amesema bado Kocha Mapunda anaendelea kuwanoa wachezaji wote, hivyo watakaoonyesha kiwango bora ndiyo watakaochaguliwa kuunda kikosi hicho.
“Wachezaji 25 watafanyiwa mchujo wiki ijayo kupata wachezaji 15 ambao watawenda Burundi kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo itakayoshirikisha nchi mbalimbali.
“Kocha anaendelea kuwanoa wachezaji wote, hivyo watakaoonyesha kiwango bora ndiyo watakaochaguliwa kuunda kikosi hicho,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema hivi sasa wanapitia changamoto ya fedha ya usafiri na malazi kipindi watakapofika nchini uko.
Msangi amesisitiza wanawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwapata sapoti kuhakikisha wanafikia malengo ikiwemo kubeba taji hilo msimu huu.
“Tunawaomba wadau wa michezo kuendelea kutushika mkono tunashukuru Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wametupatia usafiri.
“Bado tunakabiliwa na ukata wa fedha, hivyo tunawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kutupa sapoti ili tufikie malengo ikiwemo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo,” alisema.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Khalid Msabaha amesema malengo yao ni kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania ikiwemo kurejea nchini na ubingwa.
Amesema wachezaji wanafanya mazoezi kwa morali kubwa kuhakikisha wanafikia malengo ikiwemo kuonyesha kiwango bora.




