Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
Hii ni baada ya mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, kuahidi mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo ambapo amesema pindi atakapoingia madarakani, serikali itanunua matrekta milioni 10 katika kipindi cha miaka mitano.
Mkakati huo, utaambatana na ununuzi wa zana zingine za kilimo ambazo zitasambazwa kanda maalumu kwa lengo la kumrahisishia mkulima kupata mazao bora ya chakula na biashara.
Dk. Samia, ametangaza mpango huo, alipozungumza na maelfu ya wananchi waliofurika kumsikiliza akiinadi Ilani ya uchaguzi wilayani Chemba mkoani Dodoma, alisisitiza matrekta hayo yatakodishwa kwa wakulima nusu ya bei.
“Tuna mpango wa kununua matrekta milioni 10 ifi kapo 2030, tutanunua na zana zingine, tuanzishe vituo katika kanda ambavyo pembejeo zote za kilimo zitapatikana.
“Lengo ni kumpunguzia mkulima adha ya kukodi vifaa na zana za kilimo kwa watu binafsi, ambao kwa ekari moja, wanalimiwa hadi sh. 80,000 ambazo wameanza kushusha kufi kia sh. 40,000 baada ya serikali kuanza kuweka vituo hivyo.
Alisisitiza: “Lakini kwa bei yoyote ambayo sekta binafsi itawatoza wakulima, serikali itatoza nusu ya bei hiyo.
“Sasa ndugu zangu, ili hayo yaweze kutimia, mlisema mtatoa kura kwa Rais, mbunge wetu na madiwani wetu. Naomba mfanye hivyo, kaipigieni kura CCM katika mafi ga matatu, safari yetu iendelee.”
Kuhusu zana za kilimo, alisema kuwa, serikali imeanza kuunda kanda za zana za kilimo, kwa Dodoma itaangaliwa eneo litakalofaa kuwekwa kanda hiyo.
“Kondoa na Chemba, tutaangalia uwezekano wapi kanda hiyo iwekwe, lakini suala la zana za kilimo, mara ya kwanza, tulianza na matrekta 500 na ‘pawatila’ 800,” alisema.
Pia, alibainisha serikali itaanzisha kongani za viwanda kila wilaya, hivyo kwa wilaya hiyo utafi ti utafanyika kubaini shughuli zipi kubwa zinazofaa kuanzishwa kongani za viwanda
“Lile ombi la kongani za viwanda, tutaangalia ndani ya Chemba kuna kitu gani cha uchumi, hicho ndicho tutakachokiwekea kongani ya viwanda.
“Kama ni mazao ya kilimo ni mazao gani, kama ni mifugo, tutaweka kongani ya mifugo.
“Kwa hiyo, inategemea Chemba kuna kitu gani cha uchumi, lakini tunajipanga kuanzisha kongani za wilaya za viwanda,” alisema.
AHADI ZA BARABARA
Akijibu maombi ya mgombea ubunge Jimbo la Chemba (CCM) Kunti Majala kuhusu ujenzi wa barabara, Dk. Samia, alisema barabara ya Chemba – Soya yenye urefu wa kilometa 32 ambayo imekuwa ikilalamikiwa muda mrefu, serikali imeichukua kuanza mchakato wa kuijenga.
Alisema barabara hiyo ni tegemeo kwa shughuli za minada inayofanyika kila Jumapili, ambayo inaingiza kiasi kikubwa cha fedha ndani ya halmashauri huku wafanyabiashara wadogo na wafugaji, wakiitegemea kiuchumi.
Kuhusu barabara ya Kwamotoro – Mpende – Kasakai – Ilahoda na zingine tatu za ndani ya wilaya hiyo, aliahidi kuangalia uwezekano Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuiboresha ili itumike katika kipindi chote.
“Kuna barabara ya Tanga – Handeni – Kiberashi tumemaliza upembuzi yakinifu na utekelezaji wake, utaanza mwaka huu, hii barabara itjengwa.
“Lakini kuna ahadi nyingine aliyoitoa mpendwa wetu Dk. Magufuli ya kujenga soko na stendi ndani ya Mji wa Chemba, hii nayo tunakwenda kuifanyia kazi kuhakikisha tunamaliza adha hii ya soko na stendi.
“Ujenzi wa Bwawa la Farkwa, unaendelea vizuri nasi tutaendelea kuhakikisha linamalizika kwa sababu, tunalitegemea kwa Mji wa Dodoma, ambao sasa ni mji mkubwa wa nchi yetu, uhamiaji umeongezeka, mahitaji ya maji ni makubwa mno.
“Bwawa kama hili, ndilo litakalotuokoa, tutahakikisha linamalizika ili tupate maji ya kutosha ndani ya Mji wa Dodoma,” alisisitiza.
Mgombea huyo wa urais kupitia CCM, alisema serikali itaendelea kuwatumikia wananchi katika jimbo hilo kwa kugusa kila hitaji lao la msingi.
“Hatutasita mpaka kila Mwanachemba awe anapata maji, hatutasita mpaka kila nyumba ya Mwanachemba iwake umeme, hatutasita mpaka kila mtoto wa Chemba awe anaingia darasani katika ngazi zote, tumewawekea utaratibu kutoka la kwanza mpaka kidato cha nne, anakwenda moja kwa moja.
“Atafanya mitihani kumpima kiwango chake kama amefanya vizuri, anakwenda kwa mseleleko, hakufanya vizuri anarudia mpaka afanye vizuri zaidi.
Alisisitiza kuwa: “Wakati nazindua kampeni nilisema tuna mpango maalum kuwafanya watoto wetu wa Kitanzania akifi ka darasa la tatu ajue kusoma kuandika na kuhesabu bila shinda, huo ndiyo mpango wetu ili aweze kufanya vizuri kwenye madarasa ya juu.”
Awali, akiwasalimia wakazi wa Chamwino, Dk. Samia, alisema serikali itaanzisha mashamba makubwa ya kilimo kwa vijana. Alisema mashamba hayo makubwa, yataanzishwa katika wilaya hiyo vijana wapate sehemu ya kujishughulisha kupitia sekta ya kilimo.
Pia, alieleza kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu katika wilaya hiyo, serikali yake itakwenda kuimarisha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya 10 na zahanati tano.
“Nikitembea Chamwino naona idadi ya watu inaongezeka, kwa hiyo naona bado kunahaja kujenga shule na vituo vya afya zaidi kukidhi mahitaji,” alifafanua.
Pia, alisema ataimarisha mtandao wa barabara kwa kujenga kilometa 10 za lami ndani ya Mji wa Chamwino na kuboresha barabara za pembezoni zipitike muda wote.
Dk. Samia, alisema anatambua uwepo wa shida ya maji, hivyo aliahidi kuhakikisha yanapatikana kwa urahisi.
“Sasa katika hili la maji, niwaahidi kwamba, tutahakikisha Chamwino yote inapata maji na kila Mwanachamwino, anapata maji kwa karibu zaidi, hilo tunawahakikishia.
“Wito wangu kwa ndugu zangu wa Chamwino, kawaambieni ndugu zenu, sisi wanachamwino tunaomba kura kwa Chama Cha Mapinduzi za Rais, Wabunge na Madiwani wa CCM ili kazi ya kuijenga Tanzania iendelee.
“Ni CCM ndiyo itakayoweza kusimamia maendeleo ya taifa letu, niwaombe mfanye kampeni ya kata kwa kata, mtaa kwa mtaa na nyumba kwa nyumba,” alieleza.
Aliwashukuru wananchi hao kwa kumpa baraka za kugombea na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya urais, aliwaomba waendelee kumwombea yeye na mgombea mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kwa kazi kubwa ya kampeni.