NA HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira yake ni kuhakikisha anapoondoka madarakani, haachi deni lolote kwa serikali ambalo alikopa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema hilo litawezekana kwa kuwa serikali yake imeweka mfumo wa kulipa madeni kwa kuanzisha akaunti maalumu na kila mwezi inaweka dola za Marekani milioni 15 kulipa madeni.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Mjini Unguja qlipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema kuwa, serikali imeiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha kila mwezi fedha hizo zinaingia katika akaunti maalumu kulipa mikopo, ndio maana inapata nguvu ya kuendelea kukopa kwa maendeleo ya Zanzibar.
“Nitaondoka katika uongozi siachi deni hata la senti tano. Ndani ya nafsi yangu nitahakikisha siachi deni ambalo serikali imelikopa,” amesema.
Dk. Mwinyi ameweka wazi siri ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi cha uongozi wake huku amani ikiwa jambo kubwa zaidi.
SIRI YA MAFANIKIO SERIKALI YA AWAMU YA NANE
Mambo mengine ni utulivu uliopo, usimamizi mzuri katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi..
Aidha, amesema umoja na utulivu wa wananchi hata katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakionekana yana rabsha sasa kumetulia hivyo kutoa fursa ya kuleta maendeleo.
“Namshukuru Mungu, tangu nilipoingia madarakani nimekuta wananchi ni wamoja, hata zile zehemu ambazo zilikuwa na mtafaruku mkubwa sasa zimekuwa tulivu kabisa,” amesema.
Ameeleza kuwa, jambo hilo limeipa nafasi serikali kufanya mambo ya maendeleo ikiwemo kujenga shule, hospitali, barabara, miradi ya maji, umeme, viwanja vya ndege na bandari.
Pia, amesema mafanikio yaliyopatikana yamechochewa na ukusanyani mzuri wa mapato ambayo yameipa nguvu serikali yake kufanya mambo makubwa kwa kuwa fedha zipo.
“Wakati naingia madarakani ZRA wakati ule ZRB (Mamlaka ya Mapato Zanzibar) ilikuwa ikikusanya sh bilioni 20 kwa kwa mwezi lakini sasa inakusanya sh. bilioni 80, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ilikuwa ikikusanya sh. bilioni 20 hadi 25 kwa mweli, sasa inakusanya sh. bilioni 50,” amesema.
Mbali na hayo, Dk. Mwinyi amesema mafanikio yanayoonekana sasa ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake yametokana na usimamizi thabiti wa matumizi ya serikali.
WITO KUELEKEA UCHAGUZI
Akitoa ujumbe kwa wananchi kuelekea, amesisitiza kuimarisha, umoja amani na mshikamano.
“Natumia fursa hii kuwasihi wananchi tujitahidi kufanya uchauzi wa amani. Mtu yeyote anayeitakia mema nchi hii atangulize amani.
“Kila mtu ahubiri amani, viongozi wa dini wahubiri amani, wanasiasa wahubiri amani, waandishi wa habari wasisitize amani,” ameeleza.