Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa maagizo kadhaa kwa watendaji, kuhakikisha kunakua na usimamizi mzuri wa masoko yaliyojengwa kwa lengo la kuwawekea mazingira bora wafanyabiashara.
Dk. Mwinyi, amewataka watendaji kutoza kodi ndogo na kiwango kidogo cha tozo ya usafi kwa wafanyabiashara watakaokua wakifanya biashara zao katika masoko hayo.
Ameyasema hayo jana wakati akizundua soko la kisasa na kituo cha mabasi cha Chuini, kilichopo Magharibi A, Unguja.
Pia, ameagiza uendeshwaji wa masoko hayo, kufanywa na kampuni zenye uzoefu na uwezo wa kufanya usafi na kuepuka kutafuta kampuni ambazo hazina uwezo.
“Tusitafute kampuni ambazo hazina uwezo baada ya muda mfupi, tukakuta masoko machafu, sitofurahia hali hiyo, nataka masoko haya wapewe watu wenye uwezo mkubwa wa kusafisha na kuhakikisha yanadumu katika hali kama tunavyoiona,” amesema.
Pia, ameagiza wafanyabiashara kuingizwa haraka katika soko hilo, waanze kufanya biashara kabla ya kuchelewa.
“Nimeingia humu ndani, nimekuta wapo wafanyabiashara wachache, wakiendelea kubaki hivyo, maana yake, watu wanaoingia, watapungua na tutaharibu biashara.
“Nataka wote wanaotakiwa kuingia humu, wasichukue muda, baada ya siku chache, wawe wameingia ndani na hiki kituo cha mabasi, kianze mara moja, tupate watu wengi waingie hapa na kufanya biashara,” amesema.
Dk. Mwinyi, aliagiza barabara inayozunguka soko hilo, kuwekwa lami haraka, asingependa kuona matope yanaingizwa katika soko hilo.
“Hakuna haja ya kuwa na barabara za udongo katika nchi hii, hili tulishaliamua, hivyo tunachosema ni kwamba, barabara hii fupi inayoingia humu ndani, nikipita hapa baada ya muda mfupi sana, nikute ina lami,” amesema.
Amesema soko hilo ni zuri, lina nafasi kubwa na kwamba, kama litapangwa vizuri, litaingiza wafanyabiashara wengi sana, wafanye shughuli zao katika mazingira mazuri.
Amesema madhumuni ya kujengwa kwa masoko hayo ni kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, alipowauliza wafanyabiashara wanachohitaji, walijibu kwamba, wanataka mazingira mazuri ya kufanyia biashara, mikopo na unafuu wa kodi.
“Niliwaambia nimepokea maombi yenu, ninachowaomba, mnichague na mimi nitatimiza hayo mnayoyataka, leo namshukuru Mungu kwamba, ametuwezesha kujenga masoko mazuri sana,” amesema.
Pia, amesema serikali imejenga masoko matatu makubwa yakiwemo ya Mwakwerekwe, Jumbi na Chuni na itaendelea kujenga mengine kama vile soko la kisasa maeneo ya Mombasa, eneo la Kibandamaiti.
“Napenda niseme kwamba, tumeahidi na tumetekeleza kwa hivyo, huko tunapokwenda ndugu zangu yanayokuja ni neema zaidi,” amesema.
Amesema baada ya kufunguliwa kwa masoko hayo, hakutakuwa na sababu mtu kufanya biashara katika sehemu isiyo rasmi.
“Nisingependa kuona watu wako pembezoni mwa barabara, ningependa tufanye biashara zetu katika maeneo rasmi na mazuri.
“Tumeyajenga maeneo haya kwa sababu ya watu wafanye biashara zao katika maeneo mazuri,” amesema.
ASISITIZA AMANI
Pia, Rais Dk. Mwinyi amewaasa wananchi kufanya uchaguzi kwa amani, na kuwa yeyote anayezungumza jambo lolote kinyume na kuhubiri amani basi mtu huyo haitakii mema nchi.
“Kila mwanasiasa, kiongozi wa dini, mwanahabari kwa sasa, akizungumza jambo lolote ambalo linaashiria uvunjifu wa amani, basi mtu huyo hatufai, hivyo tuwe makini ndugu zangu,” amesema.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Issa Mahfoudh, amesema ujenzi wa soko hilo ni moja ya ahadi ya Dk. Mwinyi aliyoitoa kwa wajasiriamali ya kuwapatia maeneo salama ya kufanyia biashara.
Amesema ujenzi wa soko hilo, ulianza Novemba 05, 2022 na kumalizika Machi 31, 2025 ambapo mkandarasi ni kikosi cha Zimamoto na Uokozi na mshauri elekezi ni Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA).
Amesema soko hilo, linatarajiwa kutoa ajira kwa 4,000 ndani ya soko na eneo la mabasi, ambapo mradi huo hadi kukamilika kwake, umegharimu sh. bilioni 43 zilizotokana na mapato ya ndani ya serikali.
Amebainisha kuwa, mradi huo unajumuisha sehemu ya mnada, magodauni 20 stoo za baridi sita, milango ya maduka 98, vizimba 481, sehemu ya machinjio ya kuku, vyoo vya kawaida 26 vikiwemo vya watu wenye mahitaji maalum vinne, stoo na maeneo mengine.
Pia, amesema soko hilo, lina sehemu ya maegesho ya magari na lina uwezo wa kutoa huduma ya gari 400 kwa wakati mmoja.
Kwa upande wa kituo cha mabasi, amesema kina stendi tano zenye vibanda 21 vyenye uwezo wa kuchukua mabasi 110 na huduma za milango ya maduka 24.