Na FURAHA OMARY
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefungua dirisha la udahili awamu ya pili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza mwaka wa masomo 2025/2026, kuanzia leo Septemba 4 hadi 21, mwaka huu.
Hatua hiyo, imetokana na kukamilika kwa awamu ya kwanza ya udahili huo, ambapo waombaji 116,596, sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote waliomba, wamepata udahili katika vyuo walivyoomba.
Pia, imesema waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja, wanapaswa kuthibitisha udahili wao chuo kimojawapo kuanzia leo hadi Septemba 21, mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alitangaza hayo, jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamilika kwa awamu ya kwanza na kufunguliwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
“Tume inatangaza kuwa, awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026, imeanza leo (jana) hadi Septemba 21, 2025.
“Tume inawaasa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali, watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili vyuo wanavyovipenda,” amesema.
Aidha, alivielekeza vyuo vya elimu ya juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi na waombaji wa udahili na vyuo kuzingatia utaratibu wa udahili wa awamu wa pili kama ilivyooneshwa katika kalenda ya udahili iliyopo tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).
Profesa Kihampa, aliwakumbusha waombaji udahili shahada ya kwanza kuwa, masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja, yawasilishwe moja kwa moja katika vyuo husika.
Alisema kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha vyuo vyote, vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na utaratibu uliowekwa.
KUKAMILIKA AWAMU YA
KWANZA YA UDAHILI
Akizungumzia awamu ya kwanza ya udahili, Profesa Kihampa, alibainisha jumla ya waombaji 146,879, walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza.
Aliongeza jumla ya programu 894, zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 856 mwaka 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la programu 38 za masomo.
Katibu Mtendaji huyo, alibainisha mwaka huu kuna jumla ya nafasi za udahili 205,652, ikilinganishwa na nafasi 198,986 mwaka uliopita.
“Hili ni ongezeko la nafasi 6,666 sawa na asilimia 3.3 katika programu za shahada ya kwanza,” alisema.
Profesa Kihampa, alisema katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 116,596 sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote waliiomba udahili, wamepata udahili katika vyuo walivyoomba.
“Idadi ya waombaji wa udahili na watakaodahiliwa inatarajia kuongezeka katika awamu ya pili ya udahili,” alisema.
WALIODAHILIWA VYUO
ZAIDI YA KIMOJA
Akizungumzia waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja, Profesa Kihampa aliwataka kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia jana hadi Septemba 21, mwaka huu.
Katibu Mtendaji huyo, alisema jumla ya waombaji 67,576 wamepata udahili zaidi ya chuo kimoja.
“Uthibitisho huu unafanyika kwa kutumia namba maalumu ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.
“Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia katika mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalumu ya siri kujithibitisha katika chuo husika,” alisema.
Aidha, alisema uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo mwombaji alitumia wakai wa kuomba udahili.
Alitoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu kuachilia majina ya waombaji wa udahili waliopata na kukosa nafasi.