Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaomba viongozi wa dini, kupaza sauti kuwakumbusha wanasiasa kuacha kuhubiri siasa za chuki, mifarakano, ubaguzi na matusi hususan kipindi cha kampeni.
Dk. Mwinyi, ameyasema hayo mjini Unguja katika kongamano la baraza la Maulid Zanzibar, lililofanyika ukumbi wa Polisi Ziwani, mjini Unguja.
Amesema yapo maneno yameanza kutolewa na baadhi ya viongozi wa siasa, yanayoashiria uvunjifu wa amani, hivyo ni wajibu wao, kukemea kauli hizo ambazo zinaweza kuipeleka nchi pabaya.
Aidha, amesema siyo vyema kulinyamazia jambo hilo kwa kuwa kuvunjika amani, hakuanzi na bunduki, bali huanza na viashiria vikiwemo vitisho kutoka kwa baadhi ya wanasiasa.
“Tuendelee kufanya hivyo, wanaohimizwa kutoka kwenda kuvunja amani, wasikubali maana haitakuwa faida yoyote,” amesema.
Dk. Mwinyi, amesema ni wajibu wa kila mmoja kuwa mstari wa mbele, kuilinda amani kabla na baada ya uchaguzi kwa kujiepusha na kila kitu kitakachovunja amani.
“Viongozi wa dini, wananchi, masheikh, wanahabari na viongozi wa siasa, tujitahidi kuwa walinzi wa amani yetu na kuhakikisha, kila mmoja anahubiri hilo, tujiepushe na viashiria vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani katika nchi yetu,” amesema.
Amebainisha kuwa, taifa lolote, haliwezi kuwa salama wala kuendelea bila amani, hiyo inaonesha wazi amani ni moyo wa mafanikio ya mtu na jamii kwa ujumla.
“Haya ameyathibitisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kitabu chake kitukufu cha Quraan kwa aya mbalimbali na kusisitizwa na kuhimizwa katika hadithi za Mtume Muhamad (S.A.W),” amesema.
Akizungumzia mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo, vikiwemo viashiria vya uvunjifu wa amani, amesema zinaendana na wakati uliopo kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Amesema kongamano hilo, limeakisi moja kwa moja hali halisi ya taifa na haja ya kudumisha amani ili wazidi kupiga hatua za maendeleo na kupita salama katika kipindi cha uchaguzi.
“Nimefarijika kuona wengi wetu tunazugnumza kauli moja ya kuhimiza amani katika taifa, hatua hiyo ni dalili ya kila mmoja wetu kutambua umuhimu wa kuienzi na kuidumisha neema hii ambayo ni msingi wa mafanikio,” amesisitiza.
Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman, amewasisitiza waumini kufuata mafundisho na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo ya Mwenyezi Mungu.
Awali, Katibu Mtendaji Ofi si ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amesema maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), lazima yaingizwe katika maisha ya kila siku kwa kuwa kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na maamrisho na mafundisho mema.
Amempongeza Dk. Mwinyi kwa kulisimamia jambo hilo na amekuwa mfano katika uongozi wake na watu wengine wanatakiwa kujifunza kwake. Mwenyekiti wa Baraza la Maulid Zanzibar, Abubakar Mohammed Mussa, amesema shughuli hiyo sio ya kujijenga kiimani tu bali pia imelenga kuendeleza utamaduni wa Uislaam na jamii katika mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W).