Na LILIAN JOEL,
Arusha
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira, amesema amevunja makundi ndani ya Chama katika mikoa ya Arusha na Manyara.
Amewataka wabunge waliomaliza muda wao na waliotia nia kuomba nafasi hiyo, lakini hawakuteuliwa, wajitokeze kuwanadi wagombea waliopitishwa.
Amesema mikutano ya hadhara ya kampeni ya mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, inajaa mamia ya wananchi kusikiliza sera zake, kutokana na Ilani nzuri iliyoandaliwa na Chama kwa sababu inagusa maisha ya wananchi.
Pia, amewataka wanachama hao, ambao hawakuteuliwa na Chama, kutambua nafasi ya ubunge, siyo kazi ya kudumu, bali ya muda, hivyo ni vyema wakaendelea kuwa wanachama waadilifu kwa sababu, ndani ya CCM kuna nafasi nyingi za kuteuliwa ambazo wanaweza kuendelea nazo tofauti na ubunge.
Wasira amesema hayo jana jijini Arusha, katika mkutano wake na waandishi wa habari, baada ya kuhitimisha ziara yake katika mikoa ya Arusha na Manyara, iliyolenga kuvunja makundi na kuzindua kamapeni za ubunge kwa baadhi ya majimbo ya mikoa hiyo.
“Baada ya kuwasili jijini Arusha, Agosti 31, mwaka huu nilianza kazi ya kuvunja makundi Jimbo la Arusha Mjini, tulikutana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Arusha, jimbo hilo kwa sasa, lina kundi moja tu la CCM litakaloiwezesha kupata ushindi wa kishindo.
“Tulikuwa na viongozi wote wa CCM, kuanzia ngazi ya kata katika Jimbo la Arusha Mjini na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, alikuwepo na tukakubaliana makundi sasa basi, tunakwenda kumuunga mkono mgombea ubunge sanjari na kutafuta kura za ushindi za mgombea urais kwa tiketi ya CCM Dk. Samia,” amesema.
Kuhusu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mrisho Gambo, kumuunga mkono mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, Wasira amesema licha ya kutokuwepo katika mkutano huo, anajua Gambo ni mwanachama wa CCM, atashiriki kampeni za ubunge.
“Gambo ni mwanachama wetu wa CCM. Gambo ninamfahamu sana, hawezi kufanya makosa hayo ya kutoshiriki. Ana uzoefu mkubwa, alikuwa mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wa Arusha, hivyo ninaamini anaweza kufanya kazi nyingine yoyote tofauti na ubunge,” amesema.
Kwa upande wa Mkoa wa Manyara, amesema aliyekuwa Mbunge wa Mbulu Mjini, Flattey Maasay, hakuteuliwa kugombea jimbo hilo, hivyo alighafirika na kwenda Chama cha ACT Wazalendo, lakini baada ya kufanya vikao vya kuvunja makundi alikata shauri na kurejea CCM, hivyo kuachana na dhamira yake ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya ACT.
“Pale Mbulu Vijijini, tulikutana na viongozi wote wa CCM kuanzia ngazi ya kata sanjari na wagombea ambao hawakuteuliwa akiwemo Maasay ambaye baada ya mazungumzo, alisema alighafi rika akaamua kwenda upinzani baada ya kupatwa na msongo wa mawazo, lakini nilipomfanyia ‘counselling’ (ushauri nasaha), akaelewa na kuamua kurudi nyumbani CCM, tumekubaliana atashiriki kampeni za mkoa mzima wa Manyara kuwanadi na kuwaombea kura madiwani, wabunge na mgombea wetu wa urais Dk. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Amesema atanzunguka mkoa mzima kwa sababu kada mzoefu ndani ya CCM ambaye alianzia ngazi ya chipukizi, mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa akiwakilisha wilaya ya Mbulu, mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa na baadaye kuwa mbunge wa jimbo la Mbulu kwa miaka 10, hivyo kukimbilia upinzani kulitokana na kughafirika.