Na MUSSA YUSUPH,
Iringa
“IRINGA mmefunika”, ndivyo alivyoeleza mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya kufurahishwa na maelfu ya wananchi waliofurika Uwanja wa Samora, mjini Iringa, jana, kusikiliza mkutano wake mkubwa wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Katika mkutano huo, Dk. Samia alisema mikoa mingine inapaswa kujipanga katika mikutano yao ijayo ya kampeni kuhakikisha inaipiku Iringa.
“Kwa wingi huu na ‘vibe’ (msisimko) hili, wengine wanawatizama wajipangeje wawapiku, lakini mmetisha sana wana Iringa.
Dk. Samia pia amewaeleza wananchi wa mkoa huo namna ambayo Serikali ya Awamu ya Sita ilivyotimiza ahadi zake kwa kuwaletea maendeleo katika kipindi cha miaka mitano.
Amesema miradi iliyotekelezwa imelenga kumkomboa mwananchi katika changamoto zinazomkabili, ajiimarishe kiuchumi.
“Katika safari hii tumesikia mengi yaliyofanywa na ambayo tumepanga kuyatekeleza. Katika hayo nikiwa hapa Iringa Mjini nataka kusema tuliyofanikiwa,” amesema Dk. Samia.
MAFANIKIO KILIMO
Mgombea huyo wa urais kupitia CCM alisema alipofanya ziara mkoani Iringa Agosti 22, 2022, kuna mambo aliyoahidi kwa wananchi.
Miongoni mwa mambo hayo ni ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ikiwemo miradi tisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yenye thamani ya sh. bilioni 104.4.
Dk. Samia amesema miradi hiyo imeanza kutekelezwa, ambapo imewanufaisha wakulima 64,800.
“Tumefanya mradi wa umwagiliaji maji wa Mtula uliopo mji wa Mafinga uliojengwa kwa sh. milioni 566. Mradi huu umewezesha shughuli za kilimo kuendelea kwa muda wote.
“Jitihada hizi zote zinalenga kuwezesha wakulima kuzalisha na kunufaika zaidi kupitia kilimo wanachokifanya, lakini vilevile serikali imeendelea kutoa pembejeo na mbolea kwa ruzuku ambayo imewezesha wakulima kuzalisha kwa wingi,” amebainisha.
Dk. Samia alitaja mafanikio yaliyopatikana katika zao la kahawa mkoani Iringa, ambapo hivi sasa uzalishaji umefikia tani zaidi ya 300 kutoka tani 109 mwaka 2020.
Upande wa mahindi, alisema baada ya upatikanaji pembejeo na mbolea ya ruzuku, mwaka huu Tanzania imekuwa nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo.
Amebainisha mafanikio hayo yamepatikana baada ya Tanzania kuzalisha tani milioni 10 za mahindi.
“Hivyo basi mkitupa ridhaa tutaendelea kutoa ruzuku ya mbolea kote nchini pamoja na pembejeo.
“Pia tutajenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao ya parachichi, tutajenga vituo vingine vya baridi kuhifadhia mazao ya mbogamboga,” amesisitiza.
Ameongeza: “Tutajenga maghala ya kuhifadhia mazao ya chakula na biashara, tutaanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo wakulima wapate huduma za kilimo kwa bei nafuu.”
NEEMA YA UMEME
Katika mkutano huo, Dk. Samia alieleza namna alivyotekeleza ahadi kwa upande wa nishati ya umeme.
Amesema aliahidi kufikisha miundombinu ya nishati hiyo katika vijiji vyote 360 vya mkoa wa Iringa.
Amesema vitongoji vingi vya mkoa huo vimeshafikishiwa huduma hiyo huku kazi ikiendelea katika maeneo mengine ya Iringa.
“Hapa Iringa Mjini tumefikisha umeme katika mitaa yote 189 kati ya 192 na michache iliyobaki wakandarasi wapo wanaendelea na kazi.
“Pamoja na kusambaza umeme, Tanzania nzima mijini, vijijini na vitongoji tuna kazi ya kuongeza uzalishaji umeme wa kutosha. Amebainisha:
“Tumetoka megawati 1,600 mwaka 2020 na hadi mwaka huu tupo megawati 4,000 na hivi sasa tunajipanga kufikisha megawati 8,000 kwa kutumia vyanzo anuwai ikiwemo upepo na jotoardhi.”
Amesema serikali imejipanga vyema umeme uwe ndiyo msingi au kichocheo cha maendeleo ya nchi.
MIUNDOMBINU
Dk. Samia alisema ahadi nyingine ilikuwa kuboresha Uwanja wa Ndege Nduli ambao hivi sasa mashirika kadhaa yanatoa huduma ikiwemo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ameahidi barabara ya mchepuko kupunguza msongamano ndani ya mji, ahadi ambayo imetekelezwa.
Ameeleza ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia tano huku fedha yote ya mradi imeshatoka na ujenzi unaendelea.
“Ahadi ya daraja la Kitwilu hadi Isakuliko, daraja hili tumeliweka katika mpango wa Tactic na mtakapotupa ridhaa mradi wa Tactic utakwenda kujenga daraja hili,” ameeleza.
Amesisitiza: “Kwa kawaida kila safari moja ya maendeleo huanzisha nyingine, ukijenga barabara moja ya lami watu wakionja raha ya lami wanadai na nyingine.
“Nataka niwaambie ujenzi wa kilometa moja ni sawa na sh. bilioni 1.2 sawa na vituo viwili vya afya lakini hatutaacha.
“Tutaendelea kujenga barabara za lami, tutajenga barabara za kokoto zipitike muda wote na tutafungua barabara nyingine na kila miaka inavyokwenda tutaendelea kujenga barabara,” ameongeza.
WAFANYABIASHARA WADOGO
Kwa upande mwingine, Dk. Samia alisema serikali yake haijawasahau wafanyabiashara wadogo ‘Wamachinga’.
Alisema aliwaahidi kuwajengea soko la kisasa, ambapo eneo la ujenzi limeshapatikana.
“Eneo limeshatengwa ambalo lilikuwa stendi ya mabasi na tumeanza utaratibu wa kutafuta fedha kujenga Machinga Complex ndani ya mji wa Iringa.
“Nataka niwaambie hii ni ahadi, lengo langu nimalize kabla sijamaliza muda wangu wa kazi. Nataka nimalize Machinga Complex ndani ya Iringa na wanangu wamachinga, mama lishe na wengine wote wafanye biashara zao,” alieleza.
Vilevile alisema Manispaa ya Iringa imejenga ofisi ya Machinga, baada ya kutoa fedha za ujenzi wa ofisi hizo nchi nzima.
“Niliahidi nitatoa fedha kujenga ofisi za machinga nchi nzima, nilitoa fedha na TAMISEMI wakajazia zikaenda halmashauri wakasimamia ujenzi.
Ninaambiwa ofisi imejengwa inayowawezesha kuratibu kazi zao vizuri.
“Niwahakikishie kuhusu dhamira yetu kuwaboreshea mazingira ya kufanya biashara zenu, nitakwenda kufanya hivyo,” alifafanua.
Mbali na mafanikio hayo, Dk. Samia alisema serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha huduma za kijamii, elimu, afya na maji.
UKUZAJI UCHUMI
Katika kukuza uchumi na ajira kwa vijana, alisema mkoa wa Iringa umeongeza viwanda vikubwa.
Alisema wakati anaingia madarakani mkoa huo ulikuwa na viwanda vikubwa 24, ambapo hivi sasa vipo 40 ambavyo vimechangia ongezeko la fursa za ajira kwa vijana.
Aidha, alisema anatambua nafasi ya ushirika katika maendeleo ya kilimo nchini kwa sababu hiyo, serikali imechukua hatua za makusudi kufufua na kukuza uchumi kwa kuanzisha benki ya ushirika na kuimarisha usimamizi kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Dk. Samia alisema lengo ni kuwezesha vyama vya ushirika kupata mahitaji au mitaji nafuu.
“Kujitegemea na kujiendesha kibiashara kama ilivyo kwa chama cha Iringa Farmers Cooperative Union, kilichoanzishwa mwaka 1993 ambacho ni moja ya vyama vikuu mkoani hapa.
“Mwaka huu 2025/26 chama hiki kinatarajia kusambaza pembejeo na mbolea ya ruzuku kwa wanachama wake, tumewakuza wamekua kiasi ambacho wanaweza kufanya hivyo,” alisema.
“Nataka niwahakikishie tumejipanga vyema kuvilea vyama vya ushirika ndani ya nchi yetu, lengo ni kumwezesha mkulima kufaidi nguvu na jasho lake. Huku ndiko kumuinua mkulima.
“La muhimu katika vyama vya ushirika tunalifanyia kazi ni kuhakikisha tuna watu mahiri wenye kuelewa jinsi ya kuongoza ushirika, pia matumizi ya TEHAMA kuongeza uwazi hususan katika mahesabu.
hususan katika mahesabu. Mapato na matumizi ya ushirika huko ndiko kunaleta vurugu hadi ushirika unavurugika,” alisema Dk. Samia.
KIHONGOSI ASHUKURU
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, alitumia mkutano huo wa kampeni kumshukuru Dk. Samia kwa kumteua kushika wadhifa huo.
“Nikuahidi nitakuwa mwaminifu kwako na CCM, nitakutii na usiache kunionya na kunielekeza kwa sababu bado ni kijana. Nashukuru kwa kuniamini katika nafasi mbalimbali ndani ya Chama na serikali,” alibainisha.
MRATIBU WA KAMPENI
Mratibu wa Kampeni za CCM, Nyanda za Juu Kusini, Salim Abdi Asas, alimhakikishia Dk. Samia kura za kishindo katika ukanda huo.
“Wema hulipwa kwa wema kwa hiyo wema wetu ni kukupa kura za ndiyo uendelee kutupa neema,” alieleza.
AFUNGUKA CHAMWINO
Baada ya kutoka mkoani Iringa, Dk. Samia alihutubia mkutano wa kampeni Kata ya Mlowo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM, Dk. Samia aliwajibu wanaodai Chama kinatumia nguvu kubwa katika uchaguzi mkuu pamoja na udhaifu wa wapinzani.
Dk. Samia alitumia usemi wa waswahili usemao: “Mdharau mwiba mguu huota tende” akimaanisha CCM haitavidharau vyama pinzani hata kama havina nguvu.
Mgombea urais huyo alieleza maelfu ya watu wanaohudhuria mikutano ya CCM ni ishara Chama kinakubalika ikiwa ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 2025.