NA MUSSA YUSUPH
NI VIBE la Mama hiyo ndiyo habari ya mijini kwa sasa ambapo wasanii mbalimbali wameendelea kuteka majukwaa ya burudani katika mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Miongoni mwa burudani hizo ambazo zimeendelea kuwakonga mioyo wananchi, wapenzi, mashabiki na wanachama wa CCM ni ile Sebene la Mama, Oktoba Tunatiki, Selfie ya Mama, Michano ya Kihongosi, muziki wa Singeli na Kapu la Mitano tena.
Tukianzia na Sebene la Mama, burudani hiyo inayotikisa wapenda burudani, imeporomoshwa na mwanamuziki wa Bongo Flava, Raymond Mwakyusa maarufu kama Rayvan akishirikiana na bendi ya Tanzania One Thiatre (TOT).
Wakati wimbo huo ulipopigwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa ndege wa zamani jijini Mbeya, ulimfanya mgombea Urais kupitia CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuungana na mashabiki kucheza wimbo huo.

Vibe lingine linalotikisha katika mikutano hiyo ni kundi la waigizaji wa tamthilia ya maarufu ya Jua Kali iliyotayalishwa na msanii Lamata (Lamata Village).
Pindi kundi la wasanii hao likitimba jukwaani, shangwe zinaibuka kutoka kwa maelfu ya wananchi wakicheza midundo ya aina mbalimbali kutoka kwa madj waliokuwa wakiwasindikiza.
Makundi mengine ya wasanii ni Mama ongea na mwanao wakiongozwa na Steve Nyerere, Samia Queens na Samia Kings chini ya AY, Madee na Stan Bakora. Pia, wapo watu mashuhuli mitandaoni wakiwemo Mwijaku na Doto Magari maarufu kama Mtoto wa mama Kizimkazi.
BILNAS NA OKTOBA TUNATIKI
Ni Nenga boy kama kawaida yake mzee wa kuzingatia maokoto ambapo katika mikutano ya kampeni wimbo wake wa ‘Oktoba Tunatiki’ umeendelea kuwakosha mashabiki. Miongoni mwa mashairi ya wimbo huu ambao ukiimbwa wafuasi wake wanapita nao ni “Aibu kwa wapinzani maana hawana chao, Oktoba Tunatiki. Halohalooooo……halooooo mamaaa…!!.
Wimbo huo ndiyo uliomkaribisha Dk. Samia wakati akiwasili katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika viwanja vya Tandale wilayani Rungwe mkoani Mbeya. Huyo ndiyo Nenga, mara zote akipanda jukwaani lazima achafue uwanja kwa burudani zake pendwa.
SELFIE YA MAMA
Kibwagizo kingine kinachotawala katika burudani za mikutano hiyo ni “Selfie ya Mama” ambayo kila msanii lazima atupie picha ya selfie matata sana akiwa na mashabiki waliomiminika viwanjani.
Mzizi wa staili hiyo ni pale ambapo Rais Dk. Samia alipopiga picha ya selfie na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Picha hiyo ambayo imeendelea kutamba katika kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, imegeuka kuwa mtindo sasa kwa kila msanii kupiga picha na mashabiki.
KIHONGOZI NA STYLE YA HIPHOP
Nani kakwambia kwamba CCM hakuna vipaji, hebu pata picha Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi akitawala jukwaa kwa mtindo ‘hiphop.’ Na ujue kwamba mashairi yake siyo ya kumeza bali ni ile michano ya ‘freestyle’ ambayo ni kwa wababe wachache tu kama Chid Benz, Fid Q, Darasa, Godzilla, Young Lunya “Mbuzi” ndiyo wanauwezo wa kupita nayo.
Freestyle au michano huru ni kipaji ambacho siyo kila msanii ana uwezo wa kuwa nacho, wapo wasanii ambao ni waandishi wazuri wa mashairi ya muziki huo wa kizazi kipya lakini hawawezi kupiga freestyle.
Basi katika majukwaa ya kampeni za uchaguzi mkuu, Kihongosi amedhihirisha ubabe wake kwa kuchana mistari kuhamasisha vijana kushiriki uchaguzi mkuu na kulinda amani ya nchi.
Moja ya mistari yake iliyotikisa huku akisindikizwa mdundo wa Dk. Dre ‘Still.’ Kihongosi aliimba “Watanzania tunakuamini, hatuna shaka nawe. Mama wa Taifa, Mwenyezi Mungu awe nawe, amesema kazi iendelee. Ukimzingua, tunakuzingua kazi indelee. Tulianza kutamba, tukasimama na mama, kazi ameifanya, hatuogopi lawama.” alitema mistari hiyo huku shangwe likiibuka kutoka kwa mashabiki wakimtaka aendelee kushusha ‘verse’ za kijanja.
SINGELI YASEPA NA KIJIJI
Mziki wa singeli nao haujaacha kuwanyima utamu mashabiki kutoka kwa magwiji wa mziki huo Sholo Mwamba, Dulla Makabila na wengine wengi.
“Nasema woyo woyooo….nikisema mama wewe sema Samia…Mama….Samiaaa…,” huyo ni Dulla Makabila akisepa na kijiji chake huku akitupia kibwagizo cha “Zima Zote Washa Kijani.”

Yaarabi Ikubali dua, mwimbo mwingine kutoka kwa Dulla Makabila ambao ameuimba kwa mtindo wa kuomba dua kwa muumba wapinzani wasichukue nchi. Vumbi lilitibuka zaidi pale ambapo msanii wa maigizo Asha Boko alipotikisa jukwaa kwa burudani ya singeli.
WAFALME WA BONGO FLAVA
Ufalme wa muziki wa bongo flava umeendelea kutawala kwa wababe wa mziki huo, Diamond Platnamz, Ali Kiba na Harmonize maarufu kama Konde Boy.
Diamond kupitia wimbo wake maarufu wa ‘Namleta’ mara nyingi amekuwa akiongoza burudani ya muziki wakati wa kumpokea mgombea Urais, Dk. Samia.
KAPU LA MITANO TENA
Unalikumbuka lile kapu la magori la wazee wa klabu ya Simba, basi siyo hao tu bali lipo kapu la mitano tena.
Kapu hilo limekuwa likionekana katika mikutano mbalimbali ya CCM ambalo ni maalum la kubeba kura za shindi wa kishindo za CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Likiwa limepakwa rangi ya kijani na njano baadhi ya wakereketwa wa CCM hulibeba kapu hilo kuzunguka uwanja na katika jukwaa la burudani.