Na NJUMAI NGOTA,
Rukwa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetaja baadhi ya vipaumbele vyake vya maendeleo, itakavyotekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na uanzishwaji kongani ya viwanda vya kusindika samaki na mazao ya maziwa.
Pia, uboreshaji wa huduma za jamii na uimarishaji miundombinu ya uzalishaji.
Lengo la kuanzishwa viwanda hivyo ni kukuza uchumi wa wananchi kupitia sekta za kimkakati.
Hayo yalibainishwa na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wa hadhara wa kampeni, uliofanyika, wilayani Kalambo.
Chama, kilianza kampeni zake Agosti 28, mwaka huu na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2030 na kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030.
Aidha, kuwaombea kura za kishindo wagombea wanaotokana na Chama akiwemo Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Dk. Nchimbi, alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi, wamekusudia kuanzisha kongani ya viwanda vya kusindika samaki na mazao ya maziwa katika halmashauri hiyo.
“Katika eneo la viwanda, tumekusudia kuanzisha kongani ya viwanda vya kusindika samaki na mazao ya maziwa. “Kalambo ni eneo mojawapo linalopewa nafasi ya ujenzi wa kongani hiyo,” alisema.
Alisema hiyo ni hatua kubwa ya kuhakikisha uvuvi na mazao ya mifugo kama maziwa, yanapata thamani ya ziada.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, wamejipanga kikamilifu kuhakikisha maendeleo hayo, yanawafikia wananchi wa Kalambo.
Alitaja kipaumbele kingine kinachokusudiwa kutekelezwa katika halmashauri hiyo ni kujengwa mabwawa mapya ya uvuvi na vizimba vya kufugia samaki.
Alisema kitaanzishwa kituo cha ukuzaji viumbe vya majini na kuwa, mbegu za samaki zitapatikana katika kituo kipya cha kitakachojengwa Kalambo.
AFYA
Dk. Nchimbi, alisema serikali ijayo, imekusudia kujenga zahanati 16 mpya na vituo vya afya vitano ndani ya halmashauri hiyo, ukiwa ni mkakati wa kupeleka huduma karibu zaidi na wananchi.
ELIMU
Alisema katika sekta ya afya, wamedhamiria kujenga sekondari 14 mpya na madarasa zaidi ya 80 pamoja na kuboresha miundombinu ya shule zilizopo.
MAJI SAFI NA SALAMA
Dk. Nchimbi, alisema katika miaka hiyo ijayo, wanatarajia kupeleka maji safi na salama katika vijiji 83.
Hatua hiyo, itaongeza upatikanaji wa huduma hiyo, kutoka asilimia 62 hadi 92 na kuwezesha takriban watu 92 kati ya kila 100 kupata maji safi.
MIUNDOMBINU NA NISHATI
Pia, alisema kwa upande wa barabara na madaraja, watakamilisha na kuimarisha yote yaliyopo ndani ya wilaya hiyo.
Alisema serikali ijayo, imekusudia kukamilisha kituo cha kupoza umeme cha Kalambo, kukomesha tatizo la umeme wa mgawo na kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa nishati hiyo kwa shughuli za uzalishaji.
SIKU 100 ZA KWANZA
Vilevile, Balozi Dk. Nchimbi, alisema katika siku 100 za kwanza, Dk. Samia, ameweka dhamira ya dhati kuhakikisha kila Mtanzania, anasikilizwa na kupatiwa majibu ya changamoto zake kwa wakati, kupitia njia ya mtandao.
Alisema serikali ijayo, imejipanga kutekeleza mpango wa kuanzisha mfumo huo kutoka ngazi ya kijiji hadi taifa, lengo likiwa ni kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na serikali, kuongeza uwajibikaji kwa watendaji.
“Mgombea urais, anatuambia mara nyingi, Watanzania wana changamoto, wana kero, zinasikilizwa muda mrefu hazipati majibu.
“Dk. Samia Suluhu Hassan, katika siku 100 za kwanza, ameahidi atakwenda kutengeneza utaratibu, raia kuanzia ngazi ya kijiji, vitongoji watafikisha kero zao serikalini kwa njia ya mtandao.
“Pia, kuanzia ngazi zote, zitaona tatizo lililowasilisha saa ngapi, tarehe ngapi na ngazi zote, zitajua nani hakutimiza wajibu wake, kama ofisa tarafa, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mkurugenzi, mkuu wa mkoa kama waziri, tutaona hadi ngazi ya taifa,”aliseama.
Alisema njia hiyo itakuwa rahisi kuwaajibisha kwa kutotimiza wajibu wao kwa wananchi.
“Dk. Samia anataka serikali yake, iende ikawatumikie Watanzania, anataka serikali ya CCM iwatumikie Watanzania kwa haraka, wajue hii ni serikali yao,”alisema.