Na MUSSA YUSUPH,
Singida
KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, amefunguka kuhusu ujasiri wa Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ulivyoliwezesha Taifa kuvuka katika kipindi kigumu alipoingia madarakani.
Dk. Bashiru ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni za Mgombea Urais Kanda ya Kati, alisema Dk. Samia kwa ujasiri, alifanikiwa kuivusha nchi salama baada ya kifo cha aliyekuwa Rais Dk. John Magufuli na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO -19.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa Bombadia, Singida Mjini, alisema hizo ni sababu za kutosha kumpa Dk. Samia, nafasi nyingine ya kuliongoza Taifa.
Katibu mkuu huyo mstaafu wa CCM, alisema alishiriki moja kwa moja katika vikao vya maamuzi ndani ya Chama ni shahidi namna Dk. Samia alivyoivusha nchi.
“Mnanijua mimi siyo mtu wa kupindisha. Hali haikuwa rahisi. Tulimpoteza kiongozi jasiri na wakati huo, tukakumbwa na COVID-19. Lakini, tulivuka salama. Huu ni ushahidi wa ujasiri wake.
“Nilikaa kimya kwa muda, lakini leo (jana), nimeibuka kwa nguvu mpya. Ushuhuda wangu ni wa wazi, Rais Samia ni kiongozi wa mfano.
“Msiwe na mashaka, ameshika nchi wakati mgumu na akatuvusha. Hiyo ni sifa tosha ya kuongezewa muda,”alibainisha.
Aliongeza kuwa, katika mazingira hayo, mataifa mengi huvurugika, ila Tanzania ilibaki yenye mshikamano kwa sababu ya utulivu wa Rais Dk. Samia na misingi imara ya Chama.
Dk. Bashiru, alisema uzoefu wake, unamtosha kusema wazi kwamba, Dk. Samia, ameonesha uongozi wa kiwango cha juu hasa katika usawa wa kijinsia na heshima ya binadamu.
“Usawa wa binadamu haumaanishi wote tuwe na kimo au rangi moja. Usawa ni kuheshimu utu wa kila mtu. Tajiri na maskini wakikosa maji au afya, wote wanadhalilika.
“Ndiyo maana CCM inajenga shule, zahanati na kusambaza maji kulinda utu wa kila Mtanzania,” alisema.
Dk. Bashiru, alisema kwa muda mrefu, nafasi ya mwanamke imekuwa ya pili, kupitia uongozi wa Rais Dk. Samia, hali imebadilika na wanawake sasa wanaongoza mikoa, wilaya na majimbo kwa mafanikio makubwa.
“Nilikuwa nazungumza na Mwenyekiti wa Mkoa (Martha Mlatha). Singida mna RC (Mkuu wa Mkoa) mwanamke, RAS (Katibu Tawala Mkoa) mwanamke, Mwenyekiti wa CCM ni mwanamke na hakuna kilichoharibika.
Hii ni dalili ya kuaminika kwa wanawake,” alieleza.
Alisema hata katika majimbo ya uchaguzi, wanawake wamepewa nafasi na wanaendelea kuthibitisha uwezo wao wa kiuongozi bila doa.
Alisisitiza kuwa, misingi ya usawa, mshikamano na amani, ndiyo msingi wa umoja wa kitaifa na kwamba, serikali ya CCM, chini ya Dk. Samia, imeendelea kuilinda misingi hiyo.