Na Scolastica Msewa,
Kibaha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha Rose Migiro, amesema Tanzania imejipanga vyema katika uchaguzi mkuu ujao, na kusisitiza kuwa kila kitu kipo kuhakikisha taifa linadumisha amani wakati na baada ya uchaguzi.
Alisema hayo akizindua Programu za Shahada za Uzamili na Uzamivu kuhusu Utawala kwa mwaka wa masomo 2025/2026, zitakazoendeshwa kwa pamoja na Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha (MJNLS), iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na Shule ya Uongozi ya Renmin Global ya China.
Migiro, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Dk. Migiro alisema hatua hiyo ni kurefusha urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili na vyama viwili vya CCM na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambavyo vimethaminiwa na pande zote mbili.
“Pande hizi mbili zina historia ndefu ya urafiki ambayo imeleta mabadiliko chanya kwa pande zote mbili. Tukio la leo ni alama ya hatua nyingine muhimu ya uhusiano huu,” alisema.
Akimkaribisha Katibu Mkuu, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya MJNLS, alitoa wito kwa makundi ya vijana, kuelekezwa zaidi kwa mafunzo kuwawezesha kuwa viongozi wazuri wa baadaye.
Naye, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema kuwa, China iko tayari na imejitolea kudumisha uhusiano wa nchi hizo mbili na kubadilishana uzoefu na utaalamu katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
“China ina nia ya dhati ya kubadilishana uzoefu na maendeleo yake katika teknolojia kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ili kuziwezesha kupata maendeleo katika teknolojia ya kisasa na hasa matumizi ya Akili Mnemba katika nyanja za biashara, viwanda na nyinginezo kuongeza uzalishaji,”alibainisha.
Kwa upande wa Mkuu wa Taasisi ya Masomo ya Kifedha ya Chongyang katika Chuo Kikuu cha Renmin, Profesa Wang Wen, alisema chuo hicho ni mojawapo ya vyuo vikuu bora zaidi nchini China.
Mkuu wa Shule, Profesa Marcelina Chijoriga, alisema shule hiyo, imekuwa na uhusiano mzuri na Chuo Kikuu cha Renmin na kuongeza kuwa, kuanza kwa Programu za Uzamili na Uzamivu kutaimarisha urafiki.