Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuufikisha uchumi wa Zanzibar hadi asilimia 10, atakapopata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibari katika awamu ijayo.
Amesema wakati anaingia madarakani mwaka 2020, dunia ilikuwa imekumbwa na janga la maradhi ya Uviko – 19.
Amesema wakati huo, uchumi wa Zanzibar, ulikuwa asilimia nne, lakini sasa umefikia asilimia 7.4
Dk. Mwinyi, alitoa ahadi hiyo, katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, mjini Unguja.
Dk. Mwinyi aliweka wazi dhamira yake ya kuendelea kuukuza uchumi wa Zanzibar katika nyanja mbalimbali.
“Tunakwenda vizuri kiuchumi. Uchumi wetu umefika asilimia 7.4, hatuna shaka kwa mwendo huu.
“Tutafika hata asilimia 10, tunaomba mtuunge mkono tufanye kazi katika kipindi kijacho, tukuze uchumi zaidi,” alisema.
Alisema serikali inahimiza uwekezaji katika sekta zote na kujenga miundombinu, hivyo hakuna shaka kwamba, uchumi wa Zanzibar utakua kwa haraka.
DK. SHEIN
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema Dk. Mwinyi, amefanya mambo makubwa katika uongozi wake, hususani kukuza uchumi wa Zanzibar.
Alisema ameendeleza kazi kubwa ya kukuza uchumi kama walivyoanza wao, kila mmoja amefanya kwa wakati wake huku lengo likiwa moja.
“Katika miaka mitano ijayo atakapochaguliwa tena, hapana shaka atafika hadi zaidi ya asilimia nane, kutokana na kuifungua zaidi Zanzibar,” alisema.
Alieleza kuwa, miradi mikubwa ya kimkakati ambayo anaisimamia, inatarajiwa kuzalisha ajira ya watu 25,000, miradi ambayo ina thamani ya dola milion 6.2
Alisema Dk.Mwinyi ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza , katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, amefanya mambo makubwa na kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio.
Alisema Dk.Mwinyi, ametekeleza ilani ya uchaguzi na amethibitisha uwezo wake.
WACHUMI WANENA
Dk. Hafidh Ali ambaye ni Mhadhiri, alisema kuwa, mwaka 2020, kipindi ambacho Dk. Mwinyi anaingia madarakani, uchumi wa dunia, ulitetereka kutokana na janga la Uviko 19.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi, alisimama imara kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unapaa kwa kasi kubwa.
Alisema kama Dk. Mwinyi aliweza kuukuza uchumi wa Zanzibar kutoka asilimia 4 hadi 7.4 katika kipindi cha miaka mitano ambayo ilikuwa na changamoto za kutetereka kwa Uchumi, kwa miaka mitano ijayo, ataweza kuukuza zaidi.
Alisema kwa miaka mitano ijayo ya uongozi wake, akichaguliwa, atakuza uchumi wa Zanzibar zaidi ya asilimia 10.