Na AMINA KASHEBA
UONGOZI wa Yanga umesema morali imepanda kushinda mechi nne za mwanzo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuchukua zawadi ya ‘Goli la Mama’ shilingi milioni 100.
Alisema hayo Dar es Salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema malengo yao ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo kwa lengo la kuwapa furaha mashabiki na kuchukua fedha za ‘Goli la Mama’ zinatolewa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
“Sisi msimu huu wa 2025/26, tunahitaji kitu cha tofauti katika aina ya uchezaji kwa kila mechi ambazo tutacheza katika michuano ya kimataifa,hamasa ya Rais kupitia ‘Goli la Mama’imeleta morali kubwa,”alisema.
“Kocha aina kama Folz wanapiga hesabu ya mbali ya kushinda kila mchezo na ndiyo malengo yetu hivi sasa ya kufanya vizuri kwa kila mechi ambayo tutacheza,” alisema Kamwe.
Ofisa huyo alifafanua kuwa mpira wa hivi sasa kila timu inakuwa na mpango kabambe wa kuhakikisha inafanya vyema katika mechi zao za kimataifa.
“Watu wanasema Yanga haijacheza vizuri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa, michuano hii tutaenda nayo mpaka mwisho kabisa kwa kutumia hesabu kali,” alisema.
Kamwe alisema miongoni mwa timu ambazo zimepata kocha mzuri ni Yanga kutokana na aina ufundishaji wake wa kisasa tofauti na mwalimu mwingine.
“Hivi sasa tunahitaji kucheza mechi na kushinda na kuendelea na mambo mengine, mchezo wetu Pamba ambao utafanya kesho utaona kitu cha tofauti kabisa,” alisema Kamwe.
Alisema kila timu ambayo itakutana na Yanga itegemee kupigwa mabao mengi bila kuonewa huruma ya aina yoyote ile.
Pia, ofisa huyo alimshukuru Rais Samia kwa kuweka hamasa ya fedha katika kila goli litalofungwa na timu za Tanzania kwa vile zimeongeza ushindani.
Kauli hiyo, imekuja baada ya mwishoni mwa wiki, Yanga ilianza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), kwa kuichapa timu ya Wiliete ya Angola kwa mabao 3-0.
Pambano hilo, lilipigwa katika Uwanja wa 11 de Novembro jijini Luanda.Lakini timu hizo zitarudiana Septemba 27, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na mshindi wa jumla atapambana na mshindi wa jumla kati ya Elgeco Plus ya Madagascar na Silver Strikers ya Malawi.
Ushindi huo umeipa Yanga kupata shilingi milioni 15 ikiwa ni zawadi kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan maarufu kama ‘Goli la Mama’, ikiwa ni motisha ya kila goli shilingi milioni tano katika hatua ya awali ya mashindano hayo.
Katika michuano hiyo, timu zote zinazoshiriki hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), zitavuna dola za Marekani 100,000 ambazo ni zaidi ya sh. milioni 244 za Tanzania.
Katika CAFCL, timu zitakazotinga hatua ya makundi zitakuwa na uhakika wa kuvuna dola za Marekani 700,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 1.7 za Tanzania.
Timu zitakazotinga robo fainali, kila moja itakuwa na uhakika wa kuvuna dola za Marekani 900,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 2.2 wakati zitakazoishia nusu fainali zikivuna dola za Marekani milioni 1.2 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 2.9 za Tanzania.
Bingwa wa CAFCL msimu huu, anatarajiwa kuondoka na dola za Marekani milioni 4 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 9.7 za Tanzania wakati mshindi wa pili ikiondoka na dola za Marekani milioni mbili ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 4.9 za Tanzania.